Clinton azidi kuishinikiza Sudan | Matukio ya Afrika | DW | 04.05.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Clinton azidi kuishinikiza Sudan

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton, ameitaka Sudan ya kaskazini iheshimu ahadi yake ya kuacha mashambulizi dhidi ya Sudan Kusini. Clinton pia ameiomba China kuongeza shinikizo kwa mshirika wake huyo.

Athari za mapigano baina ya Sudan mbili.

Athari za mapigano baina ya Sudan mbili.

Sudan ilisema siku ya Jumatano kuwa iko tayari kushirikiana na Umoja wa Afrika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro baina yake na Sudan Kusini, lakini Sudan kusini ilisema Alhamis kuwa Sudan iliendelea na mashambulizi.

Akizungumza katika Mkutano wake na viongozi wa China, Clinton amesema ipo haja kwa mataifa kushirikiana na kutuma ujumbe wa pamoja kwa serikali ya Sudan kwamba inapaswa kusitisha mara moja na bila masharti yoyote mashambulizi yake ndani ya mipaka ya Sudan Kusini, hasa mashambulizi ya kichokozi ya angani.

Ushirika wa mashaka
Clinton alikuwa akishiriki mazungumzo ya kila mwaka na China, ambayo imezidi kukosolewa na Marekani katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kumuunga mkono rais wa Sudan, Omar Hassan el Bashir, ambaye alitolewa hati ya kukamatwa na mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC, ya mjini The Hague, kwa tuhuma za mauaji ya kimbari.

Clinton alikaribisha hatua ya China ya kuipatia Sudan Kusini msaada wa kisiasa na kiuchumi. Sudan inadhibiti asilimia kubwa zaidi ya maeneo yenye utajiri wa mafuta na China ni mnunuzi mkubwa wa nishati hiyo.

Rais Salva Kiir wa Sudan akiwa na mwenzake wa China, Hu Jintao.

Rais Salva Kiir wa Sudan akiwa na mwenzake wa China, Hu Jintao

China iliungana na Marekani katika kupitisha azimio la pamoja la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililozitaka Sudan mbili kuacha mapigano mara moja na kurudi kwenye meza ya mazungumzo, kufuatia mgogoro uliodumu kwa zaidi ya mwezi mmoja na kutishia kuzipeleka nchi hizi katika vita.

Sudan ilisema jana kuwa itaacha mashambulizi kama azimio hilo linavyotaka, lakini ina haki ya kijitetea endapo itaendelea kuchokozwa na Sudan Kusini.

Madai mapya ya Sudan Kusini
Siku ya Alhamis majeshi ya pande zote yalisema kulikuwa na hali ya utulivu katika mipaka yoke, lakini baadaye majeshi ya Sudan Kusini yakadai kuwa ndege za Sudan zimeshambulia tena ndani ya mipaka yake.

Madai hayo yaliyotolewa na Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini, Philip Aguer, hayakuweza kuthibitishwa mara moja, na majeshi ya Sudan yalikanusha kufanya mashambulizi yoyote dhidi ya jimbo la Unity, lenye utajiri mkubwa wa mafuta nchini Sudan Kusini.

Rais Omar Hassan el Bashir wa Sudan.

Rais Omar Hassan el Bashir wa Sudan.

Aguer alisema ndege za Sudan aina ya MiG ziliangusha makombora sita katika eneo la Panuakach wakati ndege za kivita na makombora ya masafa marefu zilishambulia kambi ya kijeshi iliyoko eneo la Lalop lililoko kilomita 25 nyuma.

Alisema nchi yake sasa inahofia kuanza tena kwa mgogoro, na kwamba Khartoum haitatekeleza matakwa ya Umoja wa Mataifa. Alisema matamshi tu hayatoshi na kwamba Umoja wa Mataifa unapaswa kutuma waangalizi wasimamie kusitishwa mapigano mpakani. Kila upande unaushtumu mwingine kwa kuwasaidi waasi wanaopambana na mwingine.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE
Mhariri: Othman Miraji