City yaichapa Watford 8-0, Barca hali tete. | Michezo | DW | 23.09.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

City yaichapa Watford 8-0, Barca hali tete.

Timu ya Manchester City inayoshiriki ligi kuu ya Premier imeichabanga magoli 8-0 timu vibonde na wanaoburuta mkia kwenye ligi hiyo Watford kwa mabao.

Timu ya Manchester City inayoshiriki ligi kuu ya Premier, hawakuonyesha huruma pale ilipowatia adabu vibonde wanaoburuta mkia kwenye ligi hiyo Watford kwa mabao 8-0. City wameandika rekodi ya kufunga mabao 5 kwa muda mfupi zaidi wa dakika 18 kwenye ligi hiyo. Lakini hata hivyo haikuvunja rekodi ya Manchester United iliyowahi kuwafunga Ipswich mabao 9-0.

Bernado Silva, alifunga mabao matatu na ni mchezaji aliyefunga Hat Trick nyingi kwenye PL sawa sawa na Christiano Ronaldo. 

City ambayo pia ilitoka kifua mbele kwa mabao 3-0 ugenini kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Champions League dhidi ya Shakhtar Donetsk, katikati ya wiki iko nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ya PL, ikiwa na pointi 13, ikitanguliwa na Liverpool yenye pointi 18 baada ya mtanange wa jumapili uliowakutanisha na Chelsea na kutoka na ushindi wa mabao 2 kwa 1.

Washika Bunduki, Arsenal walifanikiwa kutoka nyuma na kupata ushindi wa mabao 3 kwa 2 dhidi ya Aston Villa. Manchester UnitedDe Gea asaini mkataba mpya na United ilifungwa mabao 2 kwa 0 ilipocheza na West Ham United, na kupata ukosoaji mkubwa. Meneja wa zamani wa Manchester United, Jose Mourinho amekiponda kikosi cha United akisema ni kibovu kuliko alichokuwa nacho wakati alipotimuliwa, huku kiungo wa zamani wa timu hiyo Roy Keane akisema anguko la kikosi hicho limefikia pabaya sana. Lakini kocha Ole Gunnar Solskjaer anasema bado ana imani na kikosi chake.

UEFA Champions League | Borussia Dortmund - FC Barcelona (Reuters/T. Schmuelgen)

Pamoja na kuingizwa ili kuokoa jahazi, Lionel Messi hukuwa na faida yoyote kuisaidia timu yake ilipofungwa mabao 2-0 na Granada.

Kwingineko, huko Uhispania, Granada iliyopanda daraja msimu uliopita iliwaduwaza mabingwa watetezi Barcelona, wakati walipowashindilia mabao 2-0 nyumbani. Pamoja na jitihada za kocha Ernesto Valverde za kuwaingiza Leonel Messi na kinda, Ansu Fati kuokoa jahazi, lakini hazikufua dafu baada ya Alvaro Vadillo kugongelea msumari wa mwisho, kufuatia mkwaju wa penati uliosababishwa na makosa ya Arturo Vidal.

Matokeo haya ni ya mabaya zaidi katika mechi za mwanzo wa ligi kwa Barcelona katika kipindi cha miaka 25. Imetoka sare mara tatu na kupoteza mara nane ugenini, ikiwa ni pamoja na kipigo kitakatifu kutoka kwa Liverpool cha mabao 4-0 katika mechi ya nusu fainali msimu uliopita wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, Champions League. Barcelona inashika nafasi ya 8 ikiwa na pointi 7. Kocha Valverde amekiri wasiwasi wake kuhusu matokeo ya mechi za ugenini, aliyosema kwa kiasi kikubwa ni mabovu.

Athletico Bilbao wanaongoza katikamsimamo wa ligi wakiwa na alama 11 ikifuatiwa na Real Madrid katika nafasi ya 2 pia ikiwa na pointi 11. Atletico Madrid ilikosakosa nafasi ya kuongoza ligi, baada ya kutoshana nguvu ya bila kufungana na Celta Virgo. Granada iko katika nafasi ya tatu na pointi 10.

Na katika Serie A, Romelu Lukaku alifunga bao lake la kwanza kwenye derby ya Milan, wakati Inter ilipoondoka na ushindi wa bao 2-0 dhidi ya watani wao AC Milan. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester United amefunga bao lake la tatu katika mechi nne za ligi ambazo zote walishinda. Kikosi hicho cha Antonio Conte sasa kinaongoza ligi kwa pointi 12, mbele ya mabingwa watetezi Juventus wenye pointi 10, baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Verona. Bologna inashika nafasi ya tatu, ikiwa na pointi 7.
 

DW inapendekeza