1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

De Gea asaini mkataba mpya na United

Lilian Mtono
16 Septemba 2019

Mlinda lango wa Manchester United David de Gea amesaini mkataba mpya na Mashetani hao wekundu na ataendelea kukipiga Old Trafford hadi mwaka 2023. Klabu ya Manchester United imetangaza leo Jumatatu.

https://p.dw.com/p/3PgHS
Frankreich UEFA EURO 2016 Spanischer Torhüter David De Gea
Picha: picture-alliance/dpa/EFE/E. Naranjo

Baada ya kuwepo kwa hatihati ya kusalia klabuni hapo na tetesi kwamba anataka kwenda Real Madrid sasa ni dhahiri kwamba kipa huyo mwenye miaka 28 ataendelea kubaki United.

Baada ya kusaini mkataba huo, De Gea aliyekuwa akicheza mwaka wake wa mwisho na United amenukuliwa "Imekuwa ni fursa nzuri ya kukaa miaka minane nikiwa na klabu hii nzuri lakini pia kupata nafasi ya kuendelea na kibarua changu hapa Manchester United ni heshima ya kweli".

Mlinda lango huyo wa kimataifa wa Uhispania amecheza mara 367 tangu alipojiunga na klabu hiyo mwaka 2011.

Meneja wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer amesema amefurahishwa sana na hatua hiyo ya De Gea, lakini pia namna alivyonuia kukisaidia kikosi hicho kusonga mbele. "Katika miaka ya hivi karibuni De Gea amejitanabaisha mwenyewe kwamba ni bora duniani" alisema Mnorway huyo.

Rodri Cascante Fußball
Rodri aliipatia klabu yake ya Manchester City bao la pili waliporaruriwa mabao 3-2 na NorwichPicha: picture alliance/dpa/S. Stacpoole

Na kwenye ligi ya Premier mabingwa watetezi Machester City waliachwa midomo wazi baada ya Norwich kuwacharaza mabao 3-2. Mabingwa hao watetezi wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 10.

Liverpool inayoongoza ligi imeendeleza rekodi ya ushindi ilipowafunga Newscastle mabao 3-1 na kujiwekea kibindoni pointi tano mbele ya Manchester City. Vijana hao wa kocha Jurgen Klopp ndio pekee ambao hawajapoteza mechi hata moja mpaka sasa kwenye ligi. Chelsea ilishinda mabao 5-2 dhidi ya Wolves huku Totenham Hotspur ikiivuruga Crystal Palace kwa jumla ya mabao 4-0 nyumbani.

Manchester United iliibana kwenye kona Leicester City kwa ushindi mwembamba wa 1-0, ikiwa Old Trafford huku Arsenal na Watford wakitoshana nguvu ya mabao 2-2. Lakini gumzo limeendelea kutawala kuhusu bao la Pierre Emmerick Aubameyang lililofungwa baada ya pasi 20 na kuvunja rekodi ya goli lililotengenezwa kwa pasi nyingi zaidi kwenye EPL msimu huu.