Champions League:Barca yatinga fainali | Michezo | DW | 04.05.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Champions League:Barca yatinga fainali

Barcelona, imefanikiwa kuingia fainali ya Champions League,baada ya hapo jana kutoka sare ya 1-1 na Real Madrid, na hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-1, kufuatia yale mawili ya pambano la wiki iliyopita.

default

Washabiki wa FC Barcelona wakishangilia

Lilikuwa ni pambano kali ambalo linachukuliwa kama fainali.Real Madrid walianza kwa nguvu huku wakitaka kupata mabao ya haraka haraka, lakini haikuwa rahisi.

FC Barcelona gegen Real Madrid

Pedro Rodriguez wa FC Barcelona akifunga bao dhidi ya Real Madrid

Barca, ambayo sasa wanaingia fainali kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka mitatu, ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 54 kupitia kwa Pedro lakini dakika kumi baadaye Marcelo alifufua matumaini ya Real Madrid kwa kusawazisha bao hilo.

Kocha wa Barcelona Pep Guardiola akizungumza mara baada ya mechi hiyo alisema vijana wake walifanya kazi kubwa kwani wachezaji wengi hawakuwa na muda wa kupumzika mara baada ya kurejea kutoka fainali za kombe la dunia mwaka jana nchini Afrika Kusini.

Barca ina wachezaji wengi waliyokuwa katika timu ya taifa ya Uhispania iliyotwaa ubingwa wa dunia.

Alipoulizwa juu ya utata uliyojitokeza katika mechi ya kwanza wiki iliyopita, Gardiola kwa ufupi alisema kwa sasa ni wakati wa kufurahia tiketi ya kwenda Wembley.

Uhasama mbaya umejengeka kati ya miamba hiyo miwili ya kandanda nchini Uhispania kufuatia mechi nne walizokumbana ndani ya kipindi cha siku 18.

Kocha wa Real Madrid Jose Mourinho hakuwa kwenye benchi kufuatia kadi nyekundu aliyopewa wiki iliyopita baada ya kupinga kadi nyekundu aliyopewa mchezajiwake.

Mourinho baadaye alisema kuwa Barca inapendelewa.Timu hizo mbili zimeshtakiana katika shirikisho la soka barani Ulaya ambapo shirikisho hilo linatarajiwa kutoa uamuzi Ijumaa wiki hii.

Nahodha wa Madrid mlinda mlango Casillas ambaye aliokoa mabao kadhaa ya wazi alisema walijitahidi na kwamba ni lazima watoke uwanjani vichwa juu.

Huku wachezaji wa Barca wakishangilia uwanjani kwa kufuzu kwao kwenda Wembley, Casillas alisema lolote watakalosema linaweza kugeuzwa na kuwa dhidi yao, hapo akimaanisha utata uliyojitokeza katika mechi ya kwanza.

kwa upande wake kocha msaidizi wa Real Madrid ambaye ndiye alikuwa katika benchi Aitor Karanka, ambaye ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo, alisema kuwa bosi wake Mourinho alikuwa sahihi kwa yale aliyoyasema katika mechi ya kwanza.

Barcelona sasa wanasubiri mshindi wa leo usiku huko Old Trafford ambapo wenyeji Manchester United wanapigiwa upatu kuweza kufuzu kwa fainali mbele ya Schalke 04 ya Ujerumani.

United wataingia uwanjani wakiwa na mtaji wa mabao 2 iliyoyapata katika mechi ya kwanza mjini Geselkirschen hapa Ujerumanai pale ilipowachapa Schalke mabao 2-0.

Kocha wa Barca Guardiola mwenye umri wa miaka 40 alisema kuwa ni heshima kucheza fainali tena katika uwanja wa Wembley na kuongeza kuwa anategemea watakumbana na Manchester United.

Akizungumzia wimbo wa Uingereza wakati wa fainali za kombe la Ulaya mwaka 1996 unaosema soka limerejea nyumbani yaani Uingereza, Guardiola alikataa na kusema soka liko Uhispania, na kwamba watawaonesha wapinzani nwao, soka la kusisimua na kuvutia.Fainali hiyo imepangwa kufanyika Tarehe 28 mwezi huu.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters/DPA