Burundi: Msako bila waranti waruhusiwa | Matukio ya Afrika | DW | 20.04.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Burundi: Msako bila waranti waruhusiwa

Bunge nchini Burundi limepiga kura kuruhusu vikosi vya usalama kufanya msako wakati wa usiku bila ya kuwa na waranti, katika nchi hiyo iliyoko katika hali ya wasiwasi mkubwa wa kisiasa.

Hatua hiyo inayotarajiwa  kuidhinishwa na Rais Pierre Nkurunzinza inakuja katika wakati ambapo inaandaliwa kura ya maoni itakayomfungulia rais huyo mlango wa kuendelea kubakia madarakani hadi 2034.

Mswada wa sheria wa mageuzi ya sheria ya uhalifu ulipitishwa jumatano usiku katika bunge la nchi hiyo ambapo wabunge 90 walikubaliana na mpango huo 22 wakaupinga. Hatua ya kupitishwa muswaada huo wa sheria mpya ilifikiwa baada ya masaa manane ya mjadala mkali bungeni. Muswaada huo hivi sasa unalazimika kufikishwa mbele ya baraza la seneti kabla ya kuidhinishwa rasmi na Rais Nkurunzinza.

Waandamanaji dhidi ya haki za binadamu

Waandamanaji dhidi ya haki za binadamu

Mashirika ya kibinadamu yamkosoa Nkurunzinza 

Mwanachama mmoja wa ngazi ya juu kutoka chama tawala cha CNDD FDD ameliambia shirika la habari la AFP kwamba mswada huo unalazimika kuidhinishwa haraka iwezekanavyo na baraza hilo la Seneti. Mashirika ya haki za binadamu yameukosoa muswaada huo unaotajwa na wapinzani kwamba unalenga kuendeleza ukandamizaji dhidi ya wanaoikosoa serikali. Lewis Mudge ni mtafiti mkuu katika shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch, ambalo linaishutumu serikali ya Burundi kwa kuwatisha wananchi, mauaji, na utesaji, anasema Sheria hiyo ina lengo moja tu:

"Mwezi Mei tarehe 17, raia wa Burundi watashiriki kura ya maoni ya ndio au la, kumruhusu rais wa sasa Pierre Nkurunzinza kutawala kwa kipindi kingine cha miaka 14, na kumfanya asalie mamlakani hadi mwaka 2034."

Anaongeza, "kura hii ya maoni inafanyika katika mazingira ya hofu, hawataki mtu yeyote kujadili mabadiliko hayo ya katiba na wanatumia jeshi la polisi kutisha; kudhulumu na wakati mwengine kuua watu ambao wanaonekana kuwa kinyume cha mpango huo. Nadhani serikali inataka kuonesha kuwa hayo yanayofanyika  yanazingatia sheria."

Hatua ya kupitishwa muswaada huo wa sheria inachukuliwa katika wakati ambapo kuna mazingira ya wasiwasi, ambapo matukio ya watu kukamatwa pamoja na matumizi ya nguvu yameongezeka tangu Nkurunzinza kuamua kugombea kwa mara nyingine 2015 katika uchaguzi uliozusha mvutano mkubwa.

Serikali yasema pana haja ya sheria mpya

Waziri wa Burundi Aimee Laurentine Kanyana

Waziri wa Burundi Aimee Laurentine Kanyana

Nkurunzinza ameitawala Burundi tangu 2005 baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoiharibu nchi hiyo. Waziri wa sheria, Aime-Laurentine Kanyana, amewaambia wabunge wakati akiwasilisha mswada huo kwamba kutokana na kubadilika kwa vitendo vya uhalifu nchini Burundi miaka ya hivi karibuni, pana haja ya kutunga sheria mpya itakayopambana na hali hiyo.

Hata hivyo, shirika la Human Rights watch linasema mswada huo mpya wa sheria hauna tafauti na hali ya ukandamizaji uliokuwa tangu hapo inaendelezwa na utawala wa Nkurunzinza.

Mudge anasema,"sheria hii mpya ambayo imewasilishwa kwa bunge, linahitaji kupitishwa na rais na bunge, bila shaka itapitishwa, lakini ni muhimu kutambua kuwa hatua hizo ni sawa na kuhalalisha maovu ambayo yamekuwa yakifanyika nchini humo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita."

Vikosi vya usalama vitakuwa na  mamlaka ya kuendesha upekuzi na misako ikilenga mkoa mzima na pia wataruhusiwa kukamata mitambo ya kompyuta na kuifanyia uchunguzi wa data. Inadaiwa na serikali ya Burundi kwamba sheria hiyo mpya itahusika katika visa vya ugaidi, biashara ya binadamu na umiliki wa silaha kinyume na sheria au madawa ya kulevya.

Wabunge kutoka muungano wa upinzani wa Amizero YAbarundi unaojumuisha wanasiasa walioko karibu na kiongozi wa zamani wa waasi ,Agathon Gwasa, waliupinga muswada huo wakisema unakwenda kinyume na katiba. Msemaji wa kundi hilo bungeni, Pierre Celestin Ndikumana, anasema chama tawala kimeizika kabisa demokrasia.

Mwandishi: Saumu Yussuf
Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com