Burkina Faso haitowekewa Vikwazo | Matukio ya Afrika | DW | 11.11.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Burkina Faso haitowekewa Vikwazo

Umoja wa Afrika umehimiza haja ya jeshi la Burkina Faso kukabidhi madaraka kwa raia, lakini umesimamisha kitisho chake cha kuliwekea vikwazo jeshi hilo iwapo hatua hiyo haitafanyika ndani ya kipindi cha wiki mbili.

Kulingana na mjumbe wa Umoja wa Afrika nchini Burkina Faso, Edem Kodjo hakutakuwepo na vikwazo vyovyote kwa sasa, na kwamba nchi hiyo itapewa muda wa kupanga kipindi cha mpito.

Mazugumzo juu ya kipindi hicho sasa hivi yanaendelea huku vyama vya upinzani na makundi ya mashirika ya kiraia yakilikabidhi jeshi pendekezo lao la serikali ya mpito.

Pendekezo hilo linasema rais wa kipindi cha mpito ni lazima awe raia na serikali inapaswa kuwa na wingi wa raia na kujumuisha wanachama wa jeshi. Lakini pendekezo hilo pia bado lina mambo mengi yanayopaswa kutatuliwa, kwa mfano, nani atapewa jukumu la kuongoza kama rais wa mpito pamoja na namna ya kuvigawa viti vya bunge la mpito.

Rais wa Zamani wa Burkina Faso Blaise Compaore

Rais wa Zamani wa Burkina Faso Blaise Compaore

Hata hivyo jeshi limekuwa likisema mara kwa mara kwamba halina nia ya kushikilia uongozi.

Henri Ye, Mkuu wa kamisheni ilioandika pendekezo lililokabidhiwa kwa kiongozi wa jeshi amethibitisha kuwa jeshi limepokea pendekezo lao na anaamini kazi itaanza mara moja kujua kipi kinafuata baada ya hilo. Amesema hivi karibuni kutafanyika mkutano wa kufikia maelewano.

Mwenyekiti wa AU asema suluhu inapaswa kutafutwa haraka

Katika ziara yake mjini Ouagadougou siku ya Jumatatu Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Mohammed Ould Abdel Aziz ambaye pia ni rais wa Mauritania, amesema hakufanya ziara hiyo kuweka vitisho au kulazimisha kitu chochote.

"Tuko hapa kuwa pamoja na wenzetu wa Burkinafaso ili waweze kupata suluhu ya matatizo yao, lakini suluhu hiyo inapaswa kutafutwa haraka," alisema rais Ould Abdel Aziz.

Mwenyekiti huyo wa Umoja wa Afrika ameongeza kuwa tayari Burkina Faso imechukua hatua muhimu za kuhakikisha demokrasia zaidi inakuwepo nchini humo. Awali Ould Abdel Aziz alitishia Umoja wa Afrika utaliwekea vikwazo taifa hilo la Afrika Magharibi iwapo kiongozi wa Kijeshi Luteni Kanali Issac Zida asingekabidhi madaraka kwa raia katika kipindi cha wiki mbili.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Mohammed Ould Abdel Aziz

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Mohammed Ould Abdel Aziz

Hata hivyo kiongozi wa Jeshi Luteni Issac Zida alitupilia mbali muda aliyowekea huku akisema kwamba ni muhimu kwanza kufikia maelewano ya kupanga kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi unaopangiwa kufanyika baadaye mwaka ujao.

Maandamano nchi BurkinaFaso taifa lililo na idadi ya watu milioni 17 yalipamba moto wakati Rais BlaiseCompaore alipoonesha nia ya kubadilisha katiba ili aendelee kuiongoza nchi hiyo baada ya miaka 27 ya utawala wake.

Rais huyo wa zamani alilazimika kujiuzulu na kukimbilia nchi jirani ya Cote D Ivoire.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com