Bunge lamtafakari Mandela | Matukio ya Afrika | DW | 09.12.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Bunge lamtafakari Mandela

Bunge la Afrika Kusini Jumatatu(09.12.2013) linakutana Cape Town kwa kikao maalum kwa heshima ya kumkumbuka shujaa wa uhuru wa nchi hiyo Nelson Mandela ambaye aliongoza nchi yake baada ya kifungo cha miaka 27 gerezani.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela.

Mara ya mwisho Mandela alijitokeza kwenye jengo la bunge hilo hapo mwezi wa Februari mwaka 2010 ikiwa ni wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya kuachiliwa kwake kutoka gerezani.

Mke wake wa zamani Winnie Madikizela- Mandela na mjukuu wake Mandla wote ni wabunge wa chama tawala cha Afrika Kusini ANC lakini bado haiko wazi iwapo watashiriki kikao hicho au la. Msemaji wa ANC Moloto Mothano amesema wanataraji kwamba baadhi ya ndugu wa familia ya Mandela watahuhduria kikao hicho.Rais wa zamani wa Afrika Kusini FW de Klerk ambaye alitunukiwa kwa pamoja na Mandela Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 1993 pia amealikwa kuhudhuria kikao hicho.

Winnie na Mandla wote wawili walihudhuria misa ya kanisa la Kimethodisti mjini Johannesburg hapo jana Jumapili ikiwa ni sehemu ya ibada ya taifa kwa Mandela ilioendeshwa kwenye makanisa,misikiti,masinagogi ya Kiyahudi na mahekalu nchini kote.

Ndoto ya Mandela idumishwe

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini.

Rais Jacob Zuma ambaye pia alihuhuria misa hiyo ametowa wito mzito wa hadhara kwa wananchi wa Afrika Kusini kuungana na kutetea fikra za Mandela za usawa,uhuru na haki na kuiweka hai milele ndoto yake.

Marais wa hivi sasa na wale wa zamani,viongozi mashuhuri duniani halikadhalika watu mashuhuri wameanza kuelekea Afrika Kusini leo hii kutowa heshima zao katika misa ya kumbukumbu na maziko ya kitaifa ya rais mstaafu wa Afrika Kusini aliyepambana kuutokomeza utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo.

Maombolezo ya Mandela kanisani Afrika Kusini (08.12.2013).

Maombolezo ya Mandela kanisani Afrika Kusini (08.12.2013).

Zaidi ya watu 80,000 watahuhuria ibada ya kutowa heshima zao kwa rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo hapo kesho katika uwanja wa mpira wa FNB ulioko Soweto ambapo Mandela alionekana hadharani mbele ya umati mkubwa kwa mara ya mwisho wakati wa fainali ya michuano ya soka Kombe la Dunia hapo mwaka 2010.

Misa kuu Jumanne

Maombolezo ya Mandela kanisani Afrika Kusini

Maombolezo ya Mandela kanisani Afrika Kusini

Misa hiyo ni fursa ya mwisho kwa waombolezaji wa Afrika ya Kusini kuungana pamoja katika misa ya pamoja ya kumbukumbu ya maisha ya Mandela kabla ya kufanyika kwa mazishi rasmi ya kitaifa kwenye kijiji alichokulia cha Qunu hapo Novemba 15.

Rais Barack Obama wa Marekani na mke wake Michelle pamoja na marais watatu waliomtangulia ni miongoni mwa takriban viongozi sabini wa nchi na serikali watakaokwenda Afrika Kusini kutoka kila pembe ya dunia kuhudhuria mazishi ya Mandela.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman