1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Kongo lamchagua Vital Kamerhe kuwa spika

Jean Noël Ba-Mweze
23 Mei 2024

Bunge la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limemchagua Vital Kamerhe, ambaye makaazi yake yalishambuliwa mwishoni mwa wiki iliyopita, kuwa spika katika kura iliyocheleweshwa.

https://p.dw.com/p/4gCcw
Mbunge na waziri wa uchumi wa Kongo Vital Kamerhe
Mbunge na waziri wa uchumi wa Kongo Vital KamerhePicha: Arsene Mpiana/AFP

Bunge la kitaifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hatimaye lina ofisi ya kudumu.

Ofisi hiyo itaongozwa na Vital Kamerhe ambaye ni mzoefu wa wadhifa huo aliowahi kuushikilia. Katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni wa muungano wa kisiasa wa Rais Félix Tshisekedi, Kamerhe alitajwa kuwa mgombea wa muungano huo kwenye kiti cha Spika.

Alichaguliwa bungeni jana Jumatano na ofisi kasimikwa mapema leo. Baada ya uchaguzi uliofanyika bungeni wakati wa jioni, Vital Kamerhe alichaguliwa kuwa Spika wa bunge.

Soma pia: Kamerhe aunda muungano mpya wa kisiasa 

Kamerhe anajuwa vizuri majukumu ya wadhifa huo aliowahi kuushika wakati Kongo ilipokuwa ikiongozwa na rais Joseph Kabila.

Aliahidi kuleta mabadiliko. Uchaguzi wa ofisi ya kudumu umefanyika siku tatu tu baada ya makao ya Kamerhe kushambuliwa na watu waliovaa sare za kijeshi wakimiliki silaha kabla watu hao kujaribu kuipindua serikali ya Kongo. Jambo ambalo Kamerhe ameligusia baada ya kuchaguliwa.

"Tunalaumu shambulio lililofanywa hivi karibuni na kundi lililomiliki silaha nzito likijaribu kuhatarisha taasisi za Jamhuri na kutulenga mimi na familia yangu. Tulipona kwa neema ya Mungu."

Upinzani wapata nafasi moja

Mwanasiasa wa upinzani Moise Katumbi
Mwanasiasa wa upinzani Moise KatumbiPicha: Nicolas Maeterlinck/picture alliance

Wabunge walichagua pia wanachama wengine. Jean-Claude Tshilumbayi ni makamu wa kwanza, Christophe Mboso makamu wa pili, Jacques Djoli ni katibu, Chimène Polipoli mweka hazina, na Grâce Neema naibu mweka hazina. Hao wote ni kutoka muungano wa rais Tshisekedi ulio na wingi bungeni.

Upinzani umepewa tu kiti cha naibu katibu ambapo wabunge walichagua Dominique Munongo kutoka chama cha Moïse Katumbi.

Soma pia: Mahakama DRC yamhukumu Kamerhe kwenda jela miaka 20

Lakini baadhi ya wabunge kutoka muungano wa rais Tshisekedi hawakuridhishwa na uchaguzi huo ambao wanaamini umefanywa kinyume cha sheria. Mbunge Willy Mishiki alieleza kwamba walikuwa wamefikisha malalamiko hayo mbele ya baraza la serikali ili kudai uchaguzi kusimamishwa.

"Tupo tukikiuka katiba na sheria ya nchi wakati sisi tunakuza demokrasia. Tulikuwa tayari tumefikisha malalamiko mbele ya baraza la serikali dhidi ya jinsi wagombea walivyotajwa. Wakati malalamiko yetu yalipokuwa yakichunguzwa ilibidi kusubiri."

Ofisi ya kudumu ya bunge la kitaifa tayari imesimikwa maepma leo Alhamisi na hivyo inaanza kazi yake. Kinachotarajiwa sasa ni serikali mpya kutangazwa karibu miezi miwili baada ya Judith Suminwa kuteuliwa kuwa Waziri mkuu.