Bundesliga:Bremen yainyemelea Schalke hadi pointi 3 | Michezo | DW | 19.03.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Bundesliga:Bremen yainyemelea Schalke hadi pointi 3

Mabingwa Bayern Munich watandikwa tena mara hii na Frankfurt.Schalke yaondoka na pointi 3 kutoka Stuttgart na Bremen yailaza Mainz na kutoroka na ushindi.

Schalke yaizaba Stuttgart bao 1:0

Schalke yaizaba Stuttgart bao 1:0

Wakati mabingwa wátetezi Bayern Munich walizabwa bao 1:1 na Frankfurt na kukatishwa matumaini ya mwisho ya ubingwa msimu huu,Weder Bremen imeupunguza mwanya wake kutoka pointi 6 na kufanya pointi 3 kati yake na viongozi wa Ligi –Schalke.Schalke ilioitimua nje Stutgart hapo jumamosi kwa bao 1:0.Stuttgart inanyatia sasa nafasi ya tatu nyuma ya Schalke na Bremen.

Kocha wa Bremen, Thomas Schaaf akieleza changamoto ya jana na Mainz ilivyokwenda alisema:

“Lazima kuwa na subira.Wenyewe tuliyatatiza mambo.tulipata fursa nzuri kutandika mikwaju langoni mwa adui,lakini hatukutumia njia rahisi kufunga mabao.Hatahivyo,tumeridhika na matokeo.”

Katika Premier League-ligi ya Uingereza Manchester united na Chelsea zilitamba kweli mwishoni mwa wiki na kuseleleza mwanya wa pointi 6 kati yao.Katika changamoto za kombe la klabu bingwa barani Afrika, TP Mazembe ya J.K.Kongo iliichezesha AS Adama ya Madagascar kindumbwendumbwe mjini Kinshasa jana ilipoizaba mabao 4:1.

Tresor Mputu alitamba kipindi cha pilim alipoufumania mlango wa AS Adema kwa mabao yake 3.Hii ni mara ya pili kwa Mputu kutia mabao 3-hattrick- mwaka huu.Ameshatia mabao 9 katika kinyan’ganyiro hiki.

Sasa TP Mazembe Engelebert ina miadi duru ijayo na Royal Armed Forcves ya Morocco mwezi ujao.Wanajeshi hao wa Morocco ni miongoni mwa klabu 7 mabingwa wa zamani waliotamba na kuingia duru ya 3 ya kombe hili.Wao waliitimua Ashanti-gold ya Ghana kwa mabao 7-6.

Zamalek ya Misri ilipiogwa kumbo nje ya mashindano kwa mudu sare tu 2-2 nyumbani Cairo na Al hilal ya Sudan.Mabingwa Al ahli pia ya Misri walitoka nyuma waliizaba Highlanders ya Zimbabwe mabao 2:0.Esperence ya Tunisia imeweka miadi na younga Africans ya Tanzania kwa kuwatimua mahasimu wao 4-1 sawa na ilivyofanya Etoile du sahel.Yanga ya Tanzania, ilizabwa mabao 2:0 na Petro Atletico ya Angola, lakini ushindi wao wa duru ya kwanza umewakatia tiketi ya duru ijayo wakiwa na miadi na na Esperence.Hautakua mteremko kwa Yanga.

Ama APR ya Rwanda ilitoka uwanjani dakika 3 kabla ya firimbi ya mwisho mjini Lome, Togo ikilalamika juu ya mkwaju wa penalty dhidi yake.Hivyo, wanajeshi hao wako hatarini kutimuliwa nje ya kinyan’ganyiro hiki.APR FC ilikua sare na Maranatha ya Togo hadi pale watogo walipotunukiwa mkwaju huo wa adhabu mnamo dakika ya 87 ya mchezo.APR haikuridhika na ikatoka nje ya uwanja.Kwanza, waliwazuwia watogo kupiga mkwaju huo wa penalty.

Wiki ijayo ujumbe kutoka Chuo kikuu cha michezo cha Cologne ukiongozwa na Prof.Carl Weber na naibu wa kocha wa zamani wa DFB-shirikisho la dimba la Ujerumani, Eric Reutmueller,utafunga safari ya Dar-es-salaam, Tanzania.Huko utakua na warsha katika chuo kikuu cha Dar-es-salaam, kitovu cha michezo.Pia utakutana na TFF-shirikisho la dimba la Tanzania bara.Ujumbe huo unafuatana na mtanzania aliehetimu kutoka chuo hicho, Salehe Mpanduzi.

KOMBE LA DUNIA LA CRICKET:

Kombe la dunia la cricket likiendelea huko Carribean, timu zinazoshiriki zitaombwa kuvaa utambi mweusi mkononi kuomboleza kifo cha kocha wa Pakistan, Bob Woolmer aliefariki dunia ghafula jana –hii ni kwa muujibu wa Baraza la Cricket la kimataifa.Leo India, iliolazwa na Bangladesh katika mpambano wake wa kwanza ,ina miadi na Bermuda huko Trinidad, na wenyeji West Indies wanaumana na Zimbabwe kisiwani Jamiaca.Viwanja vyote 2 vitapepea bendera zao nusu-mlingoti na kutakua na dakika moja ya kunyamaa kimya kabla kuanza mchezo.Mpango huu utarudiwa itakapocheza Pakistan mechi yake ya mwisho dhidi ya Zimbabwe huko Sabina Park, Jamiaca keshokutwa jumatano.

Mwishoe, tujitose katika ringi ya mabondia kati ya Muhammad Ali na George Foreman,mjini Kinshasa:

Mzee George Foreman alietandikwa na Ali katika duru ya 8 mjini Kinshasa,1974 huku wazaire wakipaza sauti “Ali boumaye” jana alikuwa miongoni wa wale waliotoa pongezi na heshima zao kwa Muhammad Ali katika maonesho ya video ilioitwa “Rumble in the Jungle”-tamba msituni inayokumbusha zahama ya wababe hao 2 barani Afrika.

Ali akiwa sasa na umri wa miaka 65 hakuhutubia jana ingawa alikuwa akitia saini kwa mashabiki wake na aliwaamkia mashabiki hao wengine walitoka nchi mbali kama Ujerumani na Australia.