Bundesliga yaanza kwa kishindo | Michezo | DW | 13.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Bundesliga yaanza kwa kishindo

Baada ya mabingwa Stuttgart kuachana suluhu 2:2 na maka mo-bingwa Schalke,jana Duisburg na Karlsruhe zilizopanda daraja ya kwanza ziliondoka kila moja na ushindi.

Bundesliga-Ligi ya Ujerumani, imeanza kwa mshindo mkubwa pale mwishoni mwa wiki-mabingwa Stuttgart na makamo-bingwa Schalke wakiondoka suluhu 2:2 na klabu 2 zilizopanda daraja ya kwanza Duisburg na Karlsruhe zikizitia munda zile za daraja ya kwanza.

Dolphin FC ya Nigeria imeilaza Enugu Rangers mabao 3-2 na kutwa kombe la chama cha mpira cha Nigeria.Na Kikosi cha Kenya kwa mashindano ya ubingwa wa riadha wa dunia huko Osaka,Japan kinajinoa kambini Kasarani.Taifa Stars wa Tanzania wanajinoa huko Sweden na Denmark kabla ya mkutano wao na Msumbiji.

Bundesliga ilianza kwa vishindo ijumaa na kumaliza duru ya kwanza pia kwa vishindo jana jumapili:Baada ya mabingwa Stuttgart, kugawana pointi na makamo-bingwa Schalke hapo ijumaa, Bayern Munich ikitamba na mastadi wake 3-mtaliana Luca Toni, mfaransa Ribery na mjerumani Klose, waliizaba Hansa Rostock mabao 3:0 bila majibu.

Wakati Rostock ndio timu pekee kati ya 3 zilizopanda daraja ya kwanza msimu huu ni pekee ilioteleza, wenzake 2-Duisburg na Karlsruhe.

Karlsruhe, waliwasangaza mabingwa wa kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani, Nüremberg walipowatandika mabao 2:0 wakati Duisburg tena bila ya jogoo lao jipya Ailton kutoka Brazil, waliikomea Borussia Dortmund 3-1.

Kocha wa Nüremberg-Hans Mayer, hakusangazwa na kuanza vibaya kwa timu yake ya Nüremberg:

“Sikusangazwa kama vile mashabiki wengine kwa matokeo hayo.Kwani nikijua wakati wa maandalio yetu timekuwa na matatizo ya kuumia wachezaji wetu lakini nina matumaini mambo yatatengenea kama msimu uliopita.”

Kura imepigwa kwa duru ijayo ya kombe la shirikisho la Ujerumani ambamo Nuremberg ni mabingwa.Nüremberg itakumbana na Carl Zeiss Jena wakati bayern Munich ina miadi na Borussia Moenchengladbach.Bremen inakutana na Wolfsburg wakati Stuttgart iliolazwa finali ya kombe hilo na Nüremberg itaumana na Paderborn.

Premier League-ligi ya Uingereza imeanza halkadhalika kwa vishindo lakini pia kwa kuumia wachezaji kadhaa mashuhuri-Rooney wa Manchester united, Essien wa Chelsea na Beni McCathy aliepelekwa hospitali baada ya changamoto kati ya Blackburn Rovers na Middlesbrough.Rovers ilitamba kwa mabao 2:1.

Mabingwa Manchester united walizimwa 0:0 na Reading.Chelsea inayopania kuipokonya kombe Manchester,iliondoka na pointi 3 kutoka Stamford Bridge kutokana na bao la kipindi cha pili la Mghana Michael Essien.

Madhambi ya kipa wa taifa wa Ujerumani langoni mwa Arsenal London ,Jens Lehmann, liliipa Fulham fursa ya kutangulia haraka dakika ya kwanza ya mchezo.Kocha wa Arsenal ,Arsene Wenger akivuta pumzi kwa ushindi mwishoe wa Arsenal, alisema bora uchelewe lakini, ufike.

Wakati Taifa Stars timu ya kabumbu ya Tanzania ,iko bado huko Danmark ikijiandaa kwa changamoto ijayo na Msumbiji,mashabiki nyumbani wamebanwa na Premier League-ligi ya Uingereza.

August 25 hadi Septemba 2, wanariadha wa Afrika mashariki watateremka uwanjani mjini Osaka,Japan kuania medali za dhahabu,fedha na shaba katika ubingwa wa dunia:

Kenya,ikichuana na ethiopia katika masafa marefu imeingia kambini huko Kasarani,Nairobi,lakini wakenya hawakuridhika mno na matokeo yao katika michezo ya karibuni ya all-Africa Games, mjini Algiers.

 • Tarehe 13.08.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHbK
 • Tarehe 13.08.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHbK