Brahimi akutana na Assad mjini Damascus | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Brahimi akutana na Assad mjini Damascus

Rais wa Syria, Bashar al Assad, amesisitiza ni watu wa nchi hiyo tu watakaoamua hatima ya mkutano wa kimataifa wa kutafuta amani Syria ujulikanao kama Geneva II, alipokutana na mjumbe wa amani Lakhdar Brahimi

Rais huyo wa Syria amerudia msimamo wake kuwa, ili amani irejee Syria basi nchi za kigeni sharti zisitishe msaada kwa waasi wanaotaka kumng'oa madarakani. Assad amesema ni watu wa Syria walio na haki ya kuamua hatima ya siku za usoni ya taifa lao na suluhisho au makubaliano yoyote lazima yakubalike na raia wake na yawe ya manufaa kwao.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na jumuiya ya nchi za kiarabu kwa mzozo wa Syria, Lakhdar Brahimi, amekutana na Assad kama sehemu ya ziara yake katika kanda hiyo inayolenga kutafuta uungwaji mkono wa kuandaliwa kwa mkutano wa kimataifa unaoandaliwa na Urusi na Marekani kwa ajili ya Syria unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao mjini Geneva.

Katika mkutano huo wa leo, Assad ameonya dhidi ya muingilio wowote kutoka nje katika mchakato wa kutafuta suluhisho la mzozo wa Syria ambao umesababisha vifo vya takriban watu 115,000 katika kipindi cha miezi 31 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuongeza kuwa lazima msaada kwa magaidi; neno ambalo utawala wake unalitumia kuashiria waasi, kukoma kama hatua muhimu ya kuafikia suluhu.

Visa vya ugonjwa wa Polio vimethibitishwa katika maeneo kadhaa nchini Syria

Visa vya ugonjwa wa Polio vimethibitishwa katika maeneo kadhaa nchini Syria

Kituo cha televisheni cha serikali Syria pia kimeripoti kuwa Brahimi alikubaliana na Assad kuwa wasyria wenyewe ndiyo wanastahili kutafuta suluhisho la vita vinavyowazonga vilivyoiharibu nchi yao. Katika mkutano huo wa kwanza kati ya Brahimi na Assad tangu Desemba mwaka jana, mjumbe huyo maalumu wa umoja wa Mataifa amesema mkutano wa Geneva unanuia kuhakikisha Wasyria wanapata ufumbuzi wa mzozo huo haraka iwezekanavyo.

Huku hayo yakijiri, kiasi ya raia 800 ambao wengi wao ni wanawake, watoto na wazee waliokuwa wamekwama katika mji wa Moadamiyet al Sham uliokuwa chini ya mashambulizi makali wamehamishwa. Hayo ni kulingana na wanaharakati wa eneo hilo la kusini mwa mji mkuu Damascus.

Raia hao waliokolewa kutoka mji huo uliokuwa ukishikiliwa na waasi kufuatia usimamizi wa shirika la msalaba mwekundu ukishirikiana na pande zote zinazozozana. Picha za video za televisheni zinaonyesha watu hao wakihamishwa wakiwa wamebeba mali zao kidogo na kuondoka kutoka mji huo wakisaidiwa na maafisa wa msalaba mwekundu.

Mji huo wa Moademiyet al Sham umekumbwa na mapigano makali kwa karibu mwaka mmoja. Makundi ya kutetea haki za binadamu yameripoti utapia mlo hasa miongoni mwa watoto katika mji huo kutokana na kukatizwa kwa njia za kupitisha misaada ya kibinadaamu. Kulingana na wanaharakati, kiasi ya raia wengine 6,000 wamesalia katika eneo hilo. Waliohamishwa sasa watapelekwa katika kambi za wakimbizi viungani wma Damascus, kujiunga na mamilioni ya wasyria wengine waliobaki kuwa wakimbizi nchini mwao.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com