1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Borussia Moenchengladbach bado iko kileleni mwa Bundesliga

Sekione Kitojo
9 Desemba 2019

Borussia Moenchengladbach  bado yang'ang'ania  kileleni mwa msimamo wa  Bundesliga,  mabingwa watetezi Bayern wapapaswa,

https://p.dw.com/p/3UVJu
1. Bundesliga | Borussia Mönchengladbach vs Bayern München (2:1) | Jubel
Picha: Imago Images/Wiechmann

 

 

Ligi  ya  Ujerumani  Bundesliga, imeendelea  katika  mchezo wake wa  14 na viongozi  Borussia Moenchengladbach wamedhihirisha  nia  yao  ya  kutoroka  na  taji hilo  msimu  huu, baada  ya  kung'ang'ania  kileleni  mwa  msimamo wa  ligi, baada  ya  kuwapiga  mweleka  mabingwa  watetezi  Bayern Munich  kwa  mabao 2-1  nyumbani. Katika  mchezo  huo Bayern walifanya  kila  waliloweza  kupata  ushindi , baada  ya  kupapaswa tena  katika  mchezo  uliopita  dhidi  ya  Bayer Leverkusen  wiki iliyopita, wakitaka  kusahihisha  mkosa  yao. Lakini  walijikuta wanagonga  mwamba  kwa  kikosi cha  kocha  Marco Rose na kuangukia  pua. Nini  kilitokea huyu  hapa  kocha wa  mpito  wa bayern Hansi Flick:

1. Bundesliga | Borussia Mönchengladbach vs Bayern München (2:1) | Enttäuschung
Wachezaji wa Bayern Munich wakiwa wameduwaa hawajui kilichotokea baada ya kuchapwa mabao 2-1 na GladbachPicha: picture-alliance/SvenSimon/F. Hoermann

"Bila  shaka tuliudhibiti mchezo, tulitengeneza  nafasi  nyingi  za kufunga. Kwa bahati  mbaya  mwishowe  hatukuweza  kuuweka mpira wavuni. Na  baada  ya  kuwa  sare  ya  1-1 Gladbach ilionesha , ni  kwanini  wako hapo walipo, kwani  wanacheza kwa kushambulia. Kwasababu  wana  nguvu  kubwa  katika  ushambuliaji. Na tulishindwa  kuutawala  mchezo, kama  tulivyofnya  katika  kipindi cha  kwanza. Hatujaridhishwa  na  hali  hiyo, kwa  kile  ambacho tumekifanya  katika  michezo yote miwili bila  kupata  pointi."

Nae kocha  wa  Borussia Moenchengladbach Marco Rose  anasema timu  yake imepigana kiume  hadi kuuangusha  mbuyu.

1. Bundesliga | Borussia Mönchengladbach vs Bayern München (2:1) | Marco Rose und Hansi Flick
Kocha wa Gladbach Marco Rose (kushoto) akisalimiana na kocha wa mpito wa bayern Hansi FlickPicha: picture-alliance/dpa/Revierfoto

"Na ningependa  kuipongeza sana timu yangu. Hii inaonesha , kwanini tuko juu. Hatukudhibitiwa, badala  yake  tuliweza kucheza kwa  nia  ya  kupata  ushindi. Hadi dakika  ya  90 tulijaribu, kile ambacho wiki na  miezi iliyopita  tulikionesha na  mwishowe tulizawadiwa penalti."

Timu zilizofaidika  na  mchezo  wa  14  wa  Bundesliga , ni  pamoja na  Borussia  Dortmund, baada  ya  kupata  ushindi wa  kibarua  wiki iliyopita  dhidi  ya  Hertha Berlin , siku  ya  Jumamosi  ilionesha kuwa  bado  ina  makali, baada  ya  kuirarua  Fortuna  Dusseldorf kwa  mabao 5-0. Mchezaji wa  kati wa  Dortmund Julian Brandt anaelezea  hisia  zake  baada  ya  muda  mrefu  kikosi  hicho kutumbukia  katika  ukosoaji  mkubwa  kuhusu uchezaji  wake.

"Kimsingi  mtu  alitambua, kwa mara nyingine kutokana na mchezo ule tulioonesha, ambapo  tulidhibiti kila  eneo, bila  shaka  mabao mengi yangepatikana. Hii inatokea  katika  mchezo wa  mpira.  Na pia unaona, kwamba  mwishoni  pia  tulikuwa  tunajisikia  raha uwanjani."

Fußball Bundesliga Borussia Dortmund - Fortuna Düsseldorf
Wachezaji wa Dortmund, Axel Witsel , Piecsek , na Marco Reus wakishangilia baoPicha: Reuters/L. Kuegeler

Leverkusen  ilipata  ushindi  mwingine dhidi  ya Schalke wa  mabao 2-1, Union Berlin ikajiimarisha  kubakia  katika  daraja  la  kwanza kwa  kuikandika  FC Kolon kwa mabao 2-0 ,  RB Leipzig  inashika nafasi ya  pili katika  msimamo wa  ligi baada  ya  kuishinda Hoffenheim kwa  mabao 3-1. Kocha  Julian Nagelsmann aliwakaribisha  waajiri  wake  wa zamani , lakini  hakutoa  nafasi kwao kuondok  na  pointi.