Borussia Dortmund bado yangan´gania uongozi Bundesliga | Michezo | DW | 17.01.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Borussia Dortmund bado yangan´gania uongozi Bundesliga

Bayern Munich mambo si mazuri na mashabiki waingia kiwewe,wakati huko Uingereza Manchester City yawakaa kooni watani wao Manchester United.

Borussia Dortmund Fußball Mannschaft Bayer Leverkusen Flash-Galerie

Borussia Dortmund siku ya pambano lao na Bayer Leverkusen mjini Leverkusen .

Ligi kuu ya Ujerumani, Bundesliga, ilirudi tena mwishoni mwa juma baada ya mapumziko ya msimu wa baridi. Itakumbukwa dimba lilifunguliwa Ijumaa usiku kwa mchezo wa kwanza kati ya Borussia Dortmund na Bayer Leverkusen huku wengi wakijiuliza jee Leverkusen itamudu kuwazuwia Dortmund kutamba. Lakini matokeo yakawa Dortmund au ukipenda Borussia kutoa onyo kwamba msimu huu imekusudia moja tu nalo ni kuondoka na ubingwa . Leverkusen, ikicheza nyumbani, ikakubali mabao 3-1, ikiwaacha Borussia Dortmund wakiendela kukamata uongozi wa Bundesliga kwa kishindo. Miongoni mwa michuano iliokua ikisubiriwa kwa hamu mwishoni mwa juma baada ya fungua dimba ya Dortmund na Leverkusen ni ule wa mabingwa watetezi Bayern Munich waliingia kibaruani ugenini kutoana jasho na Wolfsburg. Pambano hilo likadhihirika kuitoa jasho jembamba Bayern na hatima kuambulia sare ya bao moja kwa moja. Bayern Munich iko nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo ikitanguliwa na Bayer Leverkusen. Hannover 96 ambayo inaiandama Dortmund ikishika nafasi ya pili kwa tafauti ya pointi 12, ilikiona cha mtema kuni ilipojikuta ikikungutwa na Eintracht frankfurt mabao 3-0 na hivyo kurudi nyumbani ikitafakari wapi mambo yalikwenda kombo yalikwenda kombo.Mbali na Hannover kipigo pia kiliikumba Mainz iliokandikwa pia ugenini na Stuttgart bao 1-0 na Mainz kukosa nafasi ya kuchupa hadi nafasi ya pili kwani ina tafauti ya pointi moja tu na Hannover .Stuttgart iko nafasi ya 17 moja kutoka mkiani.

Matokeo mengine ni kama ifuatavyo:

Werder Bremen iliilaza Hoffenheim 2-1,Borussia M`gladbach inayokamata mkia katika nafasi ya 18 ikaibwaga Nürnberg nyumbani kwao bao moja kwa bila,FC Cologne inayoandamwa na janaga la kushuka daraja ikiwa nafasi ya 16 na pointi 16 ikatoka sare jana na Kaiserslautern bao 1-1.Hamburg ilirudi nyumbani na ushindi wa mabao1-0 baada ya kukaribishwa na Schalke , wakati timu nyengine ya kaskazini St Pauli ilikuta ikitoka sare ya 2-2 na wageni wao Freiburg.Wakati Bundesliga ikisubiriwa mwishoni mwa juma lijalo,bado kumzo ni kasi ya Borussia Dortmund, huku wengi wakiamini itatwaa ubingwa msimu huu, swali likiwa jee mabingwa watetezi Bayern Munich watafanikiwa kuingia mashindano ya vilabu bingwa ya Ulaya Champions League ? Ili kufanikiwa kuingia moja kwa moja italazimika kunyakua ubingwa au kumaliza nafasi ya pili katika ligi kuu.Ama nafasi ya tatu na kujaribu bahati yake kwa kucheza awamu ya mchujo kwa mtindo wa mtoano. Jee kwanini Bayern Munich ianaonekana kususua sua kidogo.

Ligi nyengine za Ulaya:

Katika ligi nyengine kuu za Ulaya , huko Uingereza Manchester United iko uongozini baada ya jana kwenda sare na Tottenham Hotspur inayoshika nafasi ya nne bila kufungana.

Fußball Manchester United Sir Alex Ferguson

Kocha wa MANU Sir Alex Fergusen

United sasa ina pointi 45 sawa na mahasimu wao wa mjini Manchester City. Lakini City imecheza mechi mbili zaidi ya United. Zikiwa zote zimecheza mechi 22 kila moja, Arsenal iko nafasi ya tatu katika Premier League ikiwa na pointi 43 na Chelsea nafasi ya nne kwa pointi 38. Kocha wa MANU kama inavyojulikana Manchester United Sir Alex Ferguson ana matumaini ya kuutwaa ubingwa safari hii. Huko Uhispania ligi kuu La Liga, usukani bado umo mikononi mwa Barcelona ambayo ilijizatiti zaidi baada ya Real Madrid kushindwa kufua dafu mbele ya Almeria na kugawana pointi baada ya kutoka sre 1-1, wakati Barcelona iliiadhibu Malaga mabao 4-1. Barca ina pointi 52 wakati Real Madrid ina 48. Villarreal ilijiongezea pointi nyengine 3 kibindoni kwa kuitandika Osasuna mabao 4-2 kuendelea kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo

Mchezaji wa kimataifa wa Ghana Sulley Muntari huenda akaihama Inter Milan ya Italia. Mkurugenzi wa ufundi wa kilabu hiyo Marco Branca alifichua hayo kaika tevisheni ya italia aikisema mchezaji huyo aliyekuwemo katika kikosi cha timu ya taifa ya Ghana Black stars wakati a mashindo ya kombe la dunia mwaka jana Afrika kusini, amewe kwa katika orodha ya wanaotaka kuhamishwa. Wakati wa enzi ya Jose Mourinho katika Inter kabla ya kuhamia Real Madrid ya Uhispania, Muntari alikua ni chaguo la kwanza uwanjani katika nafasi yake ya kiungo. Lakini mchezaji huyo alipoteza nafasi hiyo msimu uliopita na amekua akiingia uwanjani kwa nadra msimu huu, mara nyingi akiwa mchezaji wa akiba. Pamoja na hayo Branca alimsifu Muntari akisema ni mchezaji mwenye ushirikiano, ingawa baadhi ya wakati hutoa matamshi yanayofanana na mtu anayetaka kuwemo uwanjani. Alisema Muntari sasa ameonyesha nia ya kuwa tayari kuhamia kilabu nyengine. Barani Afrika mashindano ya kuwania kombe la Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 yanayoendelea nchini Rwanda yameingia nusu fainali zikibakia timu nne kati ya 8, ambazo pia sasa zitaiwakilisha Afrika katika fainali za kombe la dunia la vijana. Timu hizo ni wenyeji Rwanda, Burkina Faso, Cote d´Ivoire na Congo Brazzabille.  

Kombe la matifa ya Asia:

Asian Cup Khalifa-Stadion

Uwanja wa michezo wa Khalifa mjini Doha

Barani Asia , kocha wa Qatar Mfaransa Bruno Metsu amesema kwamba timu yake sasa inaweza kushinda kombe la mataifa ya Asia mashindano yanayoendelea huko Qatar, baada ya kuafanikiwa kuingia robo fainali jana. Matokeo hayo yanatokana na ushindi wake wa mabao 3-0 dhidi ya mabingwa wa Ghuba-Kuwait hapo jana, na Uzbekistan kutoka sare na China mabao 2-2. China imemaliza nafasi ya kwanza katika kundi hilo na Qatar kushika nafasi ya pili. Ni mara ya kwanza inafanikiwa kuvuka raundi ya pili baada ya majaribio yake katika mashindano 7 ya kombe hilo kushindwa. Qaatar ni mwaandalizi wa kombe la dunia 2022 na itakumbukwa kocha Metsu aliwahi kuifundisha Senegal na kufanikiwa kushiriki katika mashindano ya kandanda ya kombe la dunia 2002. 

Mwandishi:Mohamed Abdul-Rahman/dpa,rtr,afp

Mhariri: Miraji Othman