Boni Yayi ataka Mali kuingiliwa kijeshi | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.11.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Boni Yayi ataka Mali kuingiliwa kijeshi

Rais wa Umoja wa Afrika amemuandikia barua Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akitaka kuharakishwa kwa operesheni ya kuingilia kijeshi mzozo wa Mali.

Rais wa Benin Boni Yayi, kushoto

Rais wa Benin Boni Yayi, kushoto

Boni Yayi, ambaye ni Rais wa Benin na ambaye pia anaongoza Umoja huo wa Afrika kwa kipindi cha mwaka mmoja, amesema iwapo jambo hilo halitafanyika basi itachukuliwa kuwa ishara ya udhaifu wa jumuiya ya kimataifa na waasi ambao wanadaiwa kuwa na mafungamano na kundi la kigaidi la al-Qaida, ambao kwa sasa wanalidhibiti eneo la kaskazini mwa Mali.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon

Katika ripoti iliyopelekwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema mpango uliopendekezwa na Umoja wa Afrika, yaani kuingilia kijeshi nchini Mali, unahitaji kujadiliwa zaidi.

Ban amesema maswala kama vile uongozi wa vikosi hivyo vya kijeshi, mafunzo na silaha za kutosha ni jambo ambalo hadi sasa halijajibiwa.

Barua ya Rais Yayi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imesisitiza kwamba Umoja wa Afrika unategemea sana uamuzi wa Umoja wa Mataifa kuwapa waasi waliolizingira eneo la kaskazini mwa mali muda wa kuondoka na pia kuweka wazi umuhimu wa kuingilia kijeshi eneo hilo.

Rais wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz

Rais wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz

Huku hayo yakiarifiwa Rais Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania amesema nchi yake haitashiriki katika mpango huo. Rais Abdel Aziz amesema hatua ya kuingilia kijeshi nchi ya Mali itakuwa na madhara mabaya. Amesema kutakuwa na matatizo zaidi kwa kuwa waasi hao wana silaha za kutosha na wakiondoka Mali watakwenda katika majangwa na huko wataendeleza shughuli zao za kigaidi.

Mauritania na Mali zinatumia mpaka mkubwa wa pamoja na pia viongozi kadhaa wakuu wa tawi la al-Qaida la Kaskazini mwa Afrika wanaaminika kuwa na uraia wa Mauritania na kuwa ndani ya nchi hiyo.

Waasi kaskazini mwa Mali

Waasi kaskazini mwa Mali

Kwa upande wake, kamanda wa kundi hilo, Abu Mosaab Abdulwadood, amewahimiza raia wa Mali kutokubali kuingiliwa na mataifa ya nje kama njia moja ya kusuluhisha mzozo wa Mali.

"Kwa watu wazuri na Waislamu wa Mali, tunasema kuwa matatizo ya Mali ni swala kati ya Waislamu na linaweza kusuluhishwa kindani kwa mazungumzo kati ya Waislamu bila ya kumwaga tone la damu," alisema kamanda huyo.

Miezi minane iliyopita baada ya serikali nchini humo kupinduliwa na wanajeshi walioasi, makundi kadhaa ya waasi, wengine wakihusishwa na kundi la kigaidi la al-Qaida, walichukuwa udhibiti wa kaskazini mwa Mali.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com