Biden amesema Xi amekubali kutii makubaliano ya Taiwan | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.10.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Biden amesema Xi amekubali kutii makubaliano ya Taiwan

Rais wa Marekani Joe Biden amesema amezungumza na Rais wa China Xi Jinping kuhusu Taiwan na baada ya China kutuma idadi kubwa ya ndege za jeshi katika anga ya taiwan.

Biden amesema katika mazungumzo yake na Xi, wamekubaliana kuheshimu makubaliano ya Taiwan, huku mivutano ikiwa imepamba moto kati ya mataifa hayo mawili ya Asia.

Nimezungumza na Xi juu ya Taiwan. Tumekubalian, kuheshimu makubaliano ya Taiwan, hapo ndipo tulipo, na nimemwambia wazi kwamba sidhani kama anapaswa kufanya kitu kingine chochote isipokuwa kutii makubaliano hayo," amesema Biden.

Soma zaidiTaiwan na Marekani kuanza upya mazungumzo ya biashara

Anachokizungumzia Biden ni kile kinachojulikana kama "sera ya China moja” ambayo inatambua rasmi China badala ya Taiwan, na Sheria ya Uhusiano ya Taiwan, ambayo imeweka wazi kwamba uamuzi wa Marekani wa kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na China badala ya Taiwan unasisitiza kwamba mustakabali wa Taiwan utaamuliwa kwa njia za amani.

China inadai Taiwan kuwa ni eneo lake, na lina haki ya kulichukua kwa nguvu. Taiwan inasema kuwa ni nchi huru na itatetea uhuru wake na demokrasia, na kwamba China ndiyo ya kulaumiwa kwa mivutano iliyojitokeza. Waziri wa Ulinzi wa Taiwan Chiu Kuo-cheng amesema leo kwamba China itakuwa na uwezo wa kukivamia na kisiwa hicho ifikapo mwaka 2025.

Taiwan Symbolbild Konflikt mit China

Bendera za Taiwan na China

Katika kipindi cha siku nne kuanzia Ijumaa iliyopita, Taiwan iliripoti kuwa karibu ndege 148 za jeshi la China ziliingia kwenye anga yake.

Biden ametuma mshauri wake kuzungumza na China

Aidha Marekani imeitaka China kusitisha shughuli zake za kijeshi karibu na Taiwan.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani, Ned Price, amesema Marekani inatiwa wasiwasi sana na shughuli za kijeshi za China karibu na Taiwan, ambazo zinatishia amani ya eneo hilo.

Biden pia aligusia juu ya mazungumzo yake na Xi ya Septemba 9, ambayo yalikuwa ni ya kwanza katika kipindi cha miezi saba. Wakati wa mazungumzo hayo ya dakika 90, viongozi hao wawili walijadili haja ya kuhakikisha kwamba ushindani kati yao haugeuki kuwa mgogoro.

Soma zaidi: China yatumia lugha kali kuionya Taiwan kuhusu uhuru

Wakati huo huo, Rais Joe Biden amemtuma mshauri wake wa usalama wa kitaifa Jake Sullivan kwenda kufanya mazungumzo na mshauri wa sera za kigeni wa China Yang Jiechi nchini Uswizi. Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa ni mvutano wa kibiashara kati ya China na Marekani pamoja na swala hilo la  Taiwan.

Mkutano huo wa leo Jumatano , unaofanyika baada Marekani kuikosoa China kwa siku kadhaa juu ya unyanyasaji wa kijeshi unaoufanya dhidi ya kisiwa kinachojitawala cha Taiwan.