Bayern yaonja kichapo kwa mara ya kwanza | Michezo | DW | 07.12.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Bayern yaonja kichapo kwa mara ya kwanza

Mabingwa watetezi wa Bundesliga Bayern Munich wamepokea kipigo chao cha kwanza katika ligi hiyo msimu huu, baada ya siku ya Jumamosi kukandikwa mabao 3-1 na Borussia Moenchengladbach

Kipigo hicho kimepunguza mwanya wa pointi na timu inayoifuatia kutoka pointi nane hadi tano, baada ya Borussia Dortmund iliyoko katika nafasi ya pili kupata ushindi wa kutoa jasho wa mabao 2-1 dhidi ya VFL Wolfsburg iliyoporomoka hadi nafasi ya tano kutokana na kipigo hicho.

Nahodha wa Bayern Munich alizungumzia kuhusu kipigo hicho cha kwanza msimu huu dhidi ya Gladbach. "Nafikiri , tulikuwa na nafasi katika kipindi cha kwanza kuwa mbele kwa mabao 2-0 ama 3. na baada ya hapo naamini, mchezo huo ungemalizika tofauti kabisa. Kwa muda wa dakika tano kwa kweli tuliweza kupoteza mchezo huo".

Naye mshambuliaji mahiri wa Bayern Munich Thomas Mueller amesema haikupaswa timu hiyo kubweteka kama ilivyotokea. "Hii haipaswi kutokea kwa timu yenye uzoefu na uwezo kama wetu. Wakati katikati ya kipindi cha pili mabao kusomeka tatu bila kwa wapinzani wetu, basi hakukuwa na jingine ila kujibwaga tu chini".

Naye kocha wa Moenchengladbach Andre Schubert hata hivyo ameimwagia sifa Bayern. "Kwangu mimi , Bayern Munich inafurahisha kuiona ikicheza. Lakini pamoja na hayo tunajivunia, kwamba leo kwa kweli tulionesha mchezo mzuri sana".

Kwa upande wa VFL Wolfsburg meneja wa michezo Klaus Allofs alizungumzia kuhusu kipigo ilichopata timu yake dhidi ya Borussia Dortmund. "Leo ulikuwa mchezo muhimu dhidi ya wapinzani , ambao wako juu yetu na hizi ni pointi muhimu. Tulipata taabu kucheza mchezo wetu na tulibahatika , kwamba hatukuishia kupata kipigo cha juu. Lakini katika kipindi cha pili tulipambana na tulistahili kupata bao la kusawazisha mapema. Lakini kwa kushindwa kama tulivyoshindwa, kwa kweli ni bahati mbaya sana".

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / ape / dpae
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com