Bayern yaendelea kuvunja rekodi | Michezo | DW | 30.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Bayern yaendelea kuvunja rekodi

Bayern Munich imeendelea kuvunja rekodi katika Bundesliga kwa ushindi wa 13 katika michezo 14 ya ligi hiyo baada ya kuishinda Bertha Berlin kwa mabao 2-0. Hivyo wanaongoza kilele ni pointi 40

Bayern ina pointi nane zaidi ya Borussia Dortmund iliyojiimarisha katika nafasi ya pili jana , baada ya kuikandika VFB Stuttgart kwa mabao 4-1, ambapo mshambuliaji wake Pierre-Emerick Aubameyang amezifumania nyavu mara mbili, na kufikisha mabao 17 katika michezo 14.

Kocha wa VFB Stuttgart Jürgen Kramny amekiri kwamba hakuwa na la kufanya kwa mashambulizi ya Dortmund. "Kilikuwa ni kipigo kikubwa. Sijui, iwapo ilikuwa ni lazima kwa kiwango hicho , lakini Dortmund ina uwezo mkubwa sana. Na iwapo utawaachia kuchiza mchezo wao na kufanya makosa kila mara, watakuadhibu bila huruma. Leo katika kipindi cha kwanza walikuwa katika kiwango cha juu kabisa, hali ambayo haikuwapo katika mchezo wao uliopita. Na kwa kuwa tulifungwa bao mwanzoni kabisa, inavunja moyo".

VLF Wolfsburg imeporomoka pointi saba nyuma ya Dortmund ikiwa katika nafasi ya tatu baada ya kutoka suluhu bila kufungana na Augsburg. lakini kocha wa Augsburg Markus Weinzierl anasema matokeo hayo ni kutokana na timu yake kutoa upinzani mkubwa dhidi ya Wolfsburg. "Tulipambana , tulilinda vyema lango letu, tulitengeneza nafasi za kupata bao, mara tatu, na walikuwa na nafasi chache. Nafikiri , wapinzani wetu hawakupata nafasi za wazi, mbali ya mashuti mawili , matatu ya hatari yaliyopigwa mbali. Lakini hilo ni jambo la kawaida kutokana na ubora wao, na tunaridhika na pointi moja na tunasonga mbele".

Schalke 04 na Bayer Leverkusen 04 , ziliridhika na sare pia kwa kufungana bao 1-1 jana Jumapili, baada ya mchezaji wa ulinzi Schalke 04 kujifunga dakika chache kabla ya mpira kumalizika. Kocha wa Schalke nafafanua zaidi. "Inaumiza sana kufungwa goli tena la kujifunga wenyewe dakika chache kabla mchezo kumalizika. Pamoja na hayo , hata hivyo nikiangalia mchezo huo wote nadhani ni matokeo halali ya bao 1-1. Kuweza kupata pointi dhidi ya timu inayoshiriki katika Champions League , na kucheza vizuri , inatupa hali ya kujiamini kwa mchezo ujao".

Wakati huo huo mwenyekiti wa klabu ya Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge analenga makubaliano ya fedha za mapato ya televisheni ambayo yataongezeka kwa dola bilioni 1.05 kwa msimu , lakini amedai kwamba timu za juu zipate gawio kubwa zaidi amesema hayo katika mahojiano yaliyochapishwa leo na gazeti la Kicker.

Mapato ya hivi sasa ya Bundesliga kupitia michezo hiyo kuoneshwa katika televisheni inafikia dola bilioni 2.65 hadi mwaka 2017, lakini mapato hayo ni madogo ukilinganisha na yale inayopata ligi ya Uingereza ya euro bilioni 6.9 kwa timu 20 za Premier League.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae /afpe / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com