1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yaanza kampeni ya kunyakua tena ubingwa

12 Septemba 2016

Barcelona yaonja kipigo , Pep Guardiola na Jose Mourinho wafufua uhasama na ushindani wao,Manchester City yaizidi kete United wakati Bayern Munich yazidi kupeta katika Bundesliga.

https://p.dw.com/p/1K0n4
Fußball Bundesliga FC Schalke 04 - FC Bayern München
Kikosi cha Bayern Munich kinachowania kulinyakua taji la Bundesliga kwa mara ya tano mfululizoPicha: Getty Images/AFP/P. Stollarz

Mchezaji wa akiba raia wa Finnland Joel Pohjanpalo alipachika mabao matatu katika dakika 11 za mwisho za mchezo kuiwezesha Bayer Leverkusen kushinda kwa mabao 3-1 dhidi ya hamburg SV siku ya Jumatatu katika Bundesliga.

Freiburg iliyorejea tena katika Bundesliga msimu huu ilipachika m,abao mawili katika dakika za mwisho na kuishinda Borussia Moenchengladbach kwa mabao 3-1, wakati timu inayocheza kwa mara ya kwanza katika Bundesliga ya RB Leipzig iliishangaza Borussia Dortmund makamu bingwa wa msimu uliopita kwa kuikandika bao 1-0 kwa goli la dakika ya 89 na Darmstadt ilipata ushindi wa dakika za mwisho pia kwa kuiangusha Eintracht Stuttgart kwa bao 1-0.

Fußball Bundesliga 2. Spieltag RB Leipzig - Borussia Dortmund
Borussia Dortmund makamu bingwa wa Bundesliga walilizwa na vijana wa RB Leipzig kwa bao 1-0Picha: Getty Images/AFP/R. Michael

Mario Gomez na kikosi cha FVL Wolfsburg , walikabwa koo na FC Koln kwa kutoka sare tasa bila kufungana , wakati Hertha BSC Berlin iliishinda FC Ingolstadt kwa mabao 2-0 na kuiweka timu hiyo pamoja na Bayern Munich kuwa timu mbili pekee ambazo zina pointi sita kutokana na michezo miwili ya Bundesliga.

Fußball Bundesliga 2. Spieltag Borussia Mönchengladbach - SC Freiburg
Borussia Moengchengadbach katika mpambano wao dhidi ya Freiburg ambapo walilala kwa mabao 3-1Picha: Getty Images/T. Kienzle

Bayern Munich iliishinda Schalke 04 kwa mabao 2-0 siku ya Ijumaa.

Pep Guardiola na Jose Mourinho wamefufua uhasama wao ambapo Guardiola , kama anavyofanya mara nyingi alimpiku hasimu wake huyo wakati Manchester City ikiiangusha Manchester United kwa mabao 2-1 na kutochafua rekodi yake safi katika kuanza msimu huu wa Premier League kwa ushindi katika michezo yote minne ya mwanzo wa ligi.

Fußball Bundesliga 2. Spieltag RB Leipzig - Borussia Dortmund
Vijana wa RB Leipzig wakishangiria kuitungua Dortmund kwa bao 1-0Picha: Getty Images/Bongarts/A. Hassenstein

Premier League

Diego Costa alipachika mabao 2 lakini hakuweza kuizuwia Chelsea kupoteza rekodi yake ya asilimia 100 ya kutoshindwa tangu mwanzoni mwa msimu huu baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Swansea City jana Jumapili.

Arsenal ilikuwa na bahati na kutoroka na pointi tatu katika pambano ya nyumbani dhidi ya Southampton wakati Santi Carzola alipofanikiwa kufuinga bao la kusawazisha katika dakika ya 94 kwa njia ya penalti na kushinda kwa mabao 2-1, wakati mashambulizi bila kuchoka ya Liverpool yaliisaidia timu hiyo kupata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya mabingwa watetezi Leicester City.

Großbritannien Manchester Fußball Premier League Trainer Mourinho und Guardiola
Pep Guardiola na Jose Mourinho kabla ya pambano la watani wa jadi Manchester City na Manchester UnitedPicha: Reuters/C. Recine

Mario Balotelli afanya vitu vyake

Mario Balotelli alichachua pambano la watani wa jadi kwa kufunga mabao mawili wakati akiichezea kwa mara ya kwanza Nice na kuipatia ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Olympique Marseille jana Jumapili, goli lake la kwanza katika ligi kwa mwaka nzima.

Nice ni ya pili katika League 1, nyuma ya viongozi wa ligi hiyo Monaco kwa tofauti ya magoli.

Mabingwa watetezi wa ligi ya Uhispania Barcelona walionja " joto ya jiwe" baada ya kushangazwa na timu iliyopanda daraja msimu huu ya Alaves uwanjani Camp Nou siku ya Jumamosi wakati Lionel Messi , Luis Suarez na Andres Iniesta , walikuwa wamepumzishwa na kocha Luis Enrique baada ya kurejea kutoka katika michezo yao ya timu za taifa, safari za masafa marefu kwa ndege pamoja na kuwa majeruhi, walikuwa wanaangalia wakiwa katika benchi.

Großbritannien Manchester - Fussball Premier League - Manchester City vs Manchester United
Wachezaji wa Manchester City wakipongezana baada ya ushindi dhidi ya manchester UnitedPicha: Getty Images/A. Livesey

Wakati huo huo Cristiano Ronaldo alirejea tena uwanjani baada ya kuwa nje miezi miwili kwa maumivu kuisaidia Real Madrid kuichakaza Osasuna kwa mabao 5-2 na kujiwreka pointi mbili juu ya msimamo wa ligi.

UEFA njia panda

UEFA shirikisho la kandanda katika mabara ambalo lina utajiri mkubwa na lenye nguvu , linamchagua rais wake mpya wiki hii wakati likikabiliana na ongezeko la changamoto katika ng'ombe wake wa maziwa anayeleta fedha nyingi , Champions League.

Shirikisho hilo lenye wanachama 55 barani Ulaya linapaswa kumchagua rais wake baina ya Aleksander Ceferin, mwenye umri wa miaka 48, na mtaalamu wa masuala ya utawala raia wa Uholanzi Michael van Praag , mwenye umri wa miaka 68, ili kukamilisha muda wa Michel Platini ambaye hadi yake imechafuliwa katika mkutano maalum mjini Athens siku ya Jumatano baada ya kampeni kali.

Italien Mario Balotelli Europameisterschaft 2012 Halbfinale
Mario Balotelli wa NicePicha: Getty Images/AFP/F. Leon

Ceferin anaungwa mkono na zaidi ya vyama 20 ikiwa ni pamoja na Ujerumani, Ufaransa, Ureno na Urusi , kwa mujibu wa shirikisho la kandanda nchini Slovenia.

Uingereza, Ubelgiji na Uhloanzi zinamuunga mkono Praag. "Tunahitaji kiongozi muaminifu. Mwanasiasa asiyekuwa mroho wa madaraka," Van Praag alisema katika ukurasa wake wa Tweeter wiki iliyopita.

Lakini kutokuwapo kwa Platini mwaka huu wakati akipoteza pambano lake dhidi ya kuzuiwa na FIFA kuhusiana na malipo ya dola milioni 2 kumeshuhudia ongezeko la changamoto dhidi ya Champions League kutoka miongoni mwa nchi ndani ya Ulaya na nje, ambapo kampuni kubwa la China la Wanda linaripotiwa kufadhili kinyang'anyiro mbadala.

Cristiano Ronaldo Fußball Spanien
Cristiano Ronaldo wa Real MadridPicha: picture-alliance/dpa/J.Martin

Si Ceferin ama Van Praag ameshasema hadharani jinsi watakavyoliongoza jahazi hilo linaloyumba yumba.

UEFA ilitangaza mwezi uliopita kwamba imeamua kuanzia mwaka 2018-2021 kwamba ligi kuu nne za Ulaya , Uhispania, Uingereza, Ujrumani na Italia , zitapata nafasi nne za kudumu katika Champions League.

Michael van Praag 2013
Michael van Praag kutoka Uholanzi anayewania kuwa rais wa UEFAPicha: Dean Mouhtaropoulos/Getty Images

Lakini shirikisho la ligi za kandanda za Ulaya EPFL limeshutumu hatua hiyo kuwa haik ubaliki na lilitishia wiki iliyopita kuanzisha ligi hasimu wakati huo huo wa mashindano ya UEFA.

EPFL imedai kuwa na sauti kubwa katika maamuzi muhimu na kujadili upya makubaliano yake na UEFA wakati Ceferin ama Van Praag akiingia madarakani.

EPFL inadai kupewa kiti katika baraza la utendaji la UEFA.

Wakati huo huo rais wa UEFA aliyepigwa marufuku Michel Platini amepewa ruhusa kuzungumza katika kikao kijacho cha shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA ambako mrithi wake atachaguliwa siku ya Jumatano.

UEFA ilisema Jumatatu kwamba kamati ya maadili ya shirikisho la kandanda duniani FIFA imemruhusu Platini kuwahutubia wajumbe wa mkutano huo mjini Athens.

Zürich UEFA Pressekonferenz Michel Platini Korruptionsskandal
Michel Platini ameruhusiwa kuwahutubia wajumbe wa mkutano watakaomchagua mrithi wa kiti chakePicha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Katika Champions League:

Real Madrid ina lenga kuwa klabu ya kwanza kushinda kombe la Champions League mwaka mmoja baada ya mwingine mfululizo wakati kampeni za msimu wa mwaka 2016-17 zitakapoanza. Real Madrid inaanza kampeni yake dhidi ya Sporting Lisbon siku ya Jumatano, klabu ambayo nyota wake Ronaldo alianzia kucheza soka.

Hakuna timu ambayo ilifanikiwa kushinda kombe hilo mfululizo tangu mfumo wa Champions League kuanzishwa mwaka 1992, na Real sasa inafanya juhudi nyingine ondoa mkosi huo, ambapo ipo katika kundi F ambalo pia lina jumuisha makamu bingwa wa Champions League mwaka 2013 Borussia Dortmund na Legia Warsaw.

Mahasimu wao Barcelona pia watakuwa nyumbani , kesho Jumanne dhidi ya Celtic baada ya kuwapumzisha Andres Iniesta , Lionel Messi na Luiz Suarez.

Fußball Bundesliga FC Schalke 04 - FC Bayern München Trainer Ancelotti
Carlo Anceloti kocha wa Bayern MunichPicha: Imago/mika

Manchester City inaongoza kwa poinzi mbili katika msimamo wa ligi ya Uingereza Premier League baada ya kuwaangusha watani wao wa jadi Manchester United kwa mabao 2-1 mwishoni mwa juma, lakini kocha Guardiola hakutaka kutoa matumaini makubwa kabla ya mchezo dhidi ya Gladbach nyumbani.

Pambano kubwa katika kundi A kesho Jumanne ni kati ya mabingwa wa Ufaransa Paris St. Germain na Arsenal ya Uingereza uwanjani Parc des Princes , wakati Basel inakwaana na Ludogorets ya Bulgaria katika mchezo mwingine.

Jioni hiyo hiyo Carlo Anceloti anaanza juhudi zake kushinda taji la Champions League na klabu ya tatu, kufuatia mafanikio katika vilabu vya Real Madrid na AC Milan, wakati mabingwa wa mwaka 2013 Bayern Munich inawakaribisha Rostov ya Urusi katika kundi D kundi ambalo pia lina timu za PSV Eindhoven na Atletico Madrid timu iliyoikatalia Bayern kuingia fainali katika pambano la nusu fainali msimu uliopita.

Siku ya Jumatano kutashuhudiwa pambano la kwanza la Champions League la mabingwa wa Uingereza Leicester City kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo wakati watakapoitembelea timu ya Brugge nchini Ubelgiji.

Leicester iko katika kundi E, ambalo lina pambanisha timu za Tottenham dhidi ya Monaco na Bayer Leverkusen inatiana kifuani na CSKA Moscow, na kundi la H kuna mpambano kati ya Olympique Lyon dhidi ya Dynamo Zagreb na makamu bingwa wa mwaka 2015 Juventus Turin ina miadi na mabingwa mara tatu mfululizo wa kombe la Europa League Sevilla.

Mwandishi : Sekione Kitojo / ape / dpae / rtre / afpe