Bayern waonja kichapo cha kwanza nyumbani | Michezo | DW | 23.03.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Bayern waonja kichapo cha kwanza nyumbani

Anasifika sana kwa kuwa mlinda mlango nambari moja wa Ujerumani na mmoja wa walinda mlango mahiri ulimwenguni lakini Manuel Neuer alikuwa kama kichekesho tu katika mlango wa Bayern Munich

Viongozi hao wa Bundesliga walipewa kichapo cha tatu cha msimu hapo jana kwa kuduwazwa katika ngome yao mabao mawili kwa bila na Borussia Moenchengladbach. Magoli yote ya Gladbach yalitiwa wavuni na Mbrazil Raffael.

Kilikuwa kichapo cha kwanza msimu huu cha Bayern katika uwanja wao na ushindi wa tatu pekee wa Gladbach mjini Munich katika mechi 47 za Bundesliga. Sasa vijana hao wa kocha Lucien Favre wamerudi katika nafasi ya tatu kwenye ligi. Na baada ya mchuano huo, Manuel Neuer wa Bayern alijitetea "Nadhani ttaizo ni kuwa nilitaka kuudaka mpira. Kawaida mimi huenda na kisha badaye kuukinga, lakini ilikuwa ni hatari kubwa. Bila shaka mpira ulipigwa kwa kasi kutoka mita 11, 12 hivi na nilipojaribu kuupangua ukavuka mstari. Ningekuwa kama inchi 20 mbele, haungeingia".

Fußball Bundesliga 26. Spieltag Bayern München gegen Borussia Mönchengladbach

Pigo kubwa kwa Bayern baada ya Arjen Robben kuumia

Licha ya kichapo hicho, Bayern bado wanaongoza kileleni na pengo la pointi kumi na wanakaribia kushinda taji lao la tatu la Bundesliga mfululizo. Patrick Herrmann ni kiungo wa Gladbach "Nadhani bayern hawajawahi kushindwa nyumbani msimu huu. Ndiyo tumecheza vyema leo hata kama hatukufayna hivyo kwa kuumiliki mpira. Tulifunga mabao mawili kupitia mashambulizi ya kushtukiza na mra nyingine unahitaji mbinu hiyo kushinda".

Nambari mbili kwenye ligi Wolfsburg walitekwa na Mainz kwa sare ya goli moja kwa moja matokeo ambayo mchezaji wa Wolfsburg Andre Schurrle alikiri yalitokana na makosa yao wenyewe. "Bila shaka inahusiana na namna ilivyo kichwani kwa sababu kama uko tu pale uwanjani haitalingana na mchezo wako. Hilo halihusiani kwa vyovyote na ubora wa mchezo bali ni kiasi gani unajiandaa na ndio maana leo tumefanya kosa hilo".

Fußball Bundesliga FSV Mainz 05 vs. VfL Wolfsburg

Wolfsburg walizembea dhidi ya Mainz

Bayer Leverkusen wako katika nafasi ya nne baada ya ushindi wao muhimu wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Schalke 04. Kocha wa Schalke Roberto di matteo alikasirishwa sana na kichapo hicho ambacho kiliiweka timu yake katika hali ngumu ya kufuzu katika Ligi ya Mabingwa msimu ujao lakini kiungo wa Leverkusen Simon Rofles anasema bado kazi ipo. "Ndilo lengo letu kuu. Lakini tuna siyo tu Schalke kama washindani lakini Moenchengladbach bado ipo. Tunataka kuwa timu ya tatu, hivyo lengo letu lilikuwa kushinda leo na kusonga mbele ya Schalke. Na tumefanya hilo vyema".

Kwingineko, Borussia Dortmund ilirejea kwa ushindi wa mabao matatu kwa mawili dhidi ya Hanover, ikiwa ni ushindi wao wa kwanza katika mechi nne.

Ushindi huo umewaweka katika nafasi ya kumi wakati Hanover ikijikuta katika nafasi ya 14, pointi mbili juu ya kushushwa ngazi. Werder Bremen wanasalia katika nafasi ya tisa baada ya kukabwa sare ya moja moja na Cologne.

Freiburg ilijiondoa katika nafasi tatu za mkia kufuatia ushindi wake wa mbili sifuri dhidi ya Augsburg. Paderborn imesalia katika nafasi ya pili kutoka nyuma baada ya sare ya kutofungana goli na Hoffenheim, nayo Stuttgart inaendelea kushika mkia licha ya kutoka nyuma na kupata ushindi wa tatu moja dhidi ya Eintracht Frankfurt.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com