1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich yatumai kuipiku Union Berlin

Josephat Charo
17 Mei 2020

Bayern Munich wanaanza tena mbio za kuliwinda taji la nane la Bundesliga mfululizo wakiwa ugenini Jumapili (17.05.2020) Union Berlin.

https://p.dw.com/p/3cM2U
Fußball Bundesliga Bayern München v Union Berlin
Picha: Reuters/M. Dalder

Vijana wa kocha Hansi Flick wanakwenda Berlin wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa pointi moja, wakifuatiwa na Borussia Dortmund ambao waliigaraza Schalke magoli 4-0 katika ngarambe ya watani wa jadi iliyochezwa uwanja wa Signal Iduna Park mjini Dortmund.

Bayern wanakabiliwa na mtihani wa kucheza katika uwanja wa Alten Foersterei ambako kumeshuhudiwa timu kubwa zikishangazwa na wenyeji Union Berlin, timu iliyopanda daraja ikitokea daraja la pili.

Union imefanikiwa mara mbili kuzishinda timu mbili zilizokuwa zikiongoza ligi, ikiishinda Borussia Dortmund 3-1 mwezi Agosti mwaka uliopita na kuipiku Borussia Moenchengladback 2-0 miezi mitatu baadaye. Sasa ni zamu ya Bayern.

Kocha wa Bayern Flick hana uhakika na uwezo wa timu yake kucheza mechi kamili baada ya kuruhusiwa kuanza mazoezi ya kikosi kizima wiki iliyopita. "Hatujui kama timu inaweza kumudu kucheza kwa zaidi ya dakika 90," alisema Flick.

"Tumefanya mazoezi vizuri na kucheza mechi tatu za dakika 20 Jumapili iliyopita. Zilichezwa kwa kasi ya hali ya juu, lakini hatufahamu hasa tumesimama wapi. Tunalazimika kuikabili hali."

Bundesliga ndiyo ligi ya kwanza kubwa barani Ulaya kurejea viwanjani tangu janga la virusi vya corona liliposababisha ligi kusimamishwa miezi miwili iliyopita na imerejea na orodha ndefu ya masharti magumu ya afya, mojawapo kubwa likiwa mashabiki kutoruhusiwa viwanjani.

Hii ina maana Union Berlin haitawategemea mashabiki wao wanaokuwa na jazba katika uwanja wao wa nyumbani mashariki mwa mji mkuu wa Ujerumani, Berlin. Hawatakuwa pia na kocha wao Urs Fischer ambaye alilazimika kuondoka karantini ya timu hiyo kufuatia kifo cha baba mkwe.

(afp)