1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich yajiimarisha kileleni mwa ligi ya Bundesliga

Sekione Kitojo
17 Februari 2020

Bayern Munich imeendelea kukalia kiti cha usukani  wa ligi  licha  ya  kuwa  katika  mchezo huu  wa  22, inaongoza  kwa  pointi moja  tu, ikiwa  na  pointi  46, baada  ya jana Jumapili  kuirarua  FC Koln kwa  mabao 4-1.

https://p.dw.com/p/3XuBd
Bundesliga 1. FC Köln gegen Bayern München
Picha: Getty Images/Bongarts/L. Baron

Bayern Munich ikifukuzia ubingwa  wake  wa  nane  mfululizo katika  Bundesliga , inafuatiwa  na  RB Leipzig ambayo  ilikandika  Werder Bremen mabao 3-0 siku  ya  Jumamosi na  kuendelea  na  mbio  za  kuifukuza Bayern Munich  kileleni.Mlinda  mlango  wa  Bayern  Manuel Neuer amesema  wangeweza  kupachika  hata  mabao 10 lakini  hata  sisi tungefungwa mabao  kiasi. Mshambuliaji  wa  Bayern Munich Thomas Mueller  alikuwa  na  haya  ya  kusema.

Bundesliga 1. FC Köln gegen Bayern München
Wachezaji wa FC Koln Picha: Reuters/W. Rattay

"Tulianza  vizuri sana, tulifurahia  kiuchezaji. Mwanzoni tulifanya kazi nzuri sana, na  kabla  ya  mapunziko kiukweli tungeweza  kuwa na mabao matano, au sita kwa  sifuri. Ndio sababu kimsingi tumefurahi sana, na kazi yetu uwanjani  tumeitimiza  kikamilifu, tumerejea tena kuwa  vinara wa  ligi. Ugenini hapa Koln , bila  shaka tumekuwa  timu iliyotamalaki, lakini  kila  mara  ugenini  ni  lazima kupata  pointi  tatu. Kipindi  cha  pili  bahati  mbaya  ni  kama  baadhi  ya  vipindi  vya  pili huko  nyuma. Tulikuwa  mbali  na  hali  tuliyokuwa  nayo , baada  ya kuongoza  kwa  mabao 4-0 tulitakiwa  kuweka  mbinyo  zaidi.Na  hili katika michezo iliyopita kila  mara  tulishindwa  kuendelea na mchezo wetu hadi  mwisho."

Kocha  wa  FC Koln Markus Gisdol  amesema katika  kipindi  cha kwanza unaweza  kuona  kuwa  bado  tumo  katika  awamu  ya kujijenga." Bayern ilitumia uwezo wake  vizuri sana, Tulikuwa  wenye kusita sita sana, tuliwapa  eneo  kubwa  la  kufanya  watakavyo na hatukwenda  mbele  kwa  kujiamini  vya kutosha. Huyu hapa Markus Gisdol.

Bundesliga 1. FC Köln gegen Bayern München
Mshambuliaji wa Bayern Munich Serge GnabryPicha: Imago-Images/Kirchner-Media/Neundorf

"Ndio nafikiri  ilikuwa  kipindi chote cha  kwanza, ambapo tulikuwa  na matatizo  makubwa, kuweza  kuwadhibiti. Bayern walikuwa  katika kiwango  cha  juu  kabisa kuanzia  mwanzo. Katika  kipindi  cha kwanza  hatukuweza  kupata njia  muafaka, na  tulitoa  nafasi  kubwa , na  hatukufanya  vizuri  katika  kila  nafasi. Na ndio Bayern  ikiwa katika  kiwango  cha  juu  kwa  sasa waliweza kutimiza  kila wanalotaka, na hii ilitokea  kwa  haraka  sana."

RB Leipzig - SV Werder Bremen
Kocha wa RB Leipzig Julian NagelsmannPicha: picture-alliance/dpa/R. Michael

Werder Bremen  ambayo  iliiondoa  Borussia  Dortmund  katika kinyang'anyiro  cha  kombe  la  shirikisho DFB Pokal, na  kucheza kandanda  safi , haifanyi  vizuri  hata  hivyo  katika  ligi  ya Bundesliga. Ikiwa  katika  nafasi ya 17  na  pointi 17  tu imo  katika hatari  ya  kurejea  katika  daraja  la  pili msimu  ujao. Jumamosi ilikumbana na  timu  iliyoko  katika  nafasi  ya  pili  ya  Bundesliga RB Leipzig  na  ulikuwa  mtihani  mkubwa  kwa  kocha  Florian Kohfeldt kuweza  kubadilisha majaaliwa  ya  timu  hiyo. Lakini  ikiwa ugenini  Werder  Bremen  ilipokea  kipigo  cha  mabao 3-0. Kocha wa  RB Leipzig  Julian  Nagelsman anasema.