1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yairarua Frankfurt katika Super Cup

Sekione Kitojo 13 Agosti 2018

Bayern Munich  yaonesha  makucha  yake na  kuirarua Eintracht Frankfurt mabingwa  wa  kombe la  chama  cha  mpira  wa  miguu nchini  Ujerumani  DFB  katika  mpambano  wa  Super Cup kwa kuwazaba mabao matano kwa sifuri.

https://p.dw.com/p/335zc
Fußball DFL Supercup Eintracht Frankfurt - FC Bayern
Picha: Reuters/R. Orlowski

 

Robert Lewandowski  alipachika  wavuni  mabao  matatu  wakati Bayern Munich ikinyakua  kombe  la  Super Cup  la  Ujerumani  jana Jumapili kwa  kuirarua  Eintracht  Frankfurt  kwa  mabao 5-0  katika mwanzo  mzuri  kwa  kocha  Niko  Kovac , ambaye  msimu  uliopita alikuwa  akiifunza  timu  hiyo  ya  frankfurt  na  kunyakua  kombe  la DFB Pokal  kwa  kuishinda  Bayern  kwa  mabao 3-1  mjini  Berlin mwishoni  mwa  msimu  uliopita.  Mshambuliaji  huyo  kutoka  Poland , ambaye  hakufanya  vizuri  katika  fainali  za  kombe  la  dunia , 2018, alizima  purukushani  za  timu  ya  zamani  ya  Kovac kwa kupachika  mabao  mawili  katika  muda  wa  dakika  tano katika kipindi  cha  kwanza.

Fußball DFL Supercup Eintracht Frankfurt - FC Bayern
Robert Lewandowski wa Bayern MunichPicha: Reuters/R. Orlowski

Ligi  ya  England Premier League  imeanza  rasmi mwishoni  mwa wiki  hii  na  timu  zilizomaliza  katika  nafasi  tano  za  juu  zimepata ushindi bila  taabu, ambapo mabingwa  watetezi  Manchester City iliichapa  Arsenal  London  kwa  mabao 2-0  jana  Jumapili. Hata hivyo kocha  wa  Arsenal  Unai Emery  amesema  timu  yake inahitaji  kukubaliana  zaidi  na  mbinu  zake  lakini  ameeleza  pia kwamba  kuna  ishara  nzuri  alizoona  katika  mchezo  huo  wa ufunguzi  licha  ya  kufungwa  mabao 2-0 dhidi  ya Manchester City.

Fußball Premier League Arsenal -  Manchester City
raheem Sterling wa Man City akipambana na Mesut Ozil wa Arsenal (kulia)Picha: Reuters/J. Sibley

Kocha  wa  Manchester  City Pep Guardiola  anataka  Raheem Sterling  kuitumikia  timu  hiyo  kwa  muda  mrefu  zaidi baada  ya mshambuliaji  huyo  kuonekana  kuchukua  jukumu  kubwa  la kuiongoza  timu  hiyo  katika  ushindi  wa  mchezo  wa  ufunguzi katika  Premier League dhidi  ya  Arsenal. Mchezaji  huyo  mwenye umri  wa  miaka  23  ambaye  amebakiza  miaka  miwili  katika mkataba  wake , alipachika  bao lake  la  50  la  ligi  jana  Jumapili wakati  mabingwa  hao  watetezi  wakianza  kampeni  ya  msimu mpya  kwa  ushindi  wa  mabao  2-0 ugenini.

Paris Saint Germain, Unai Emery, Trainer
Kocha wa Arsenal London Unai EmeryPicha: picture-alliance/abaca/C. Liewig

"Tunafurahia  kile  anachokifanya  na  tungependa  abakie, Guardiola aliwaambia  waandishi  habari. Vyombo  vya  habari  vya  Uingereza vimeripoti  kwamba wasimamizi  wa  Sterling wanataka  mkataba mpya  ambao atalipwa  pauni 300,000 kwa  wiki , ambao  utanfanya kuwa  mchezaji  anayelipwa  fedha  nyingi  katika  klabu  hiyo.

Premier League - Trainer Pep Guardiola
Kocha wa Man City Pep GuardiolaPicha: picture alliance/empics/M. Rickett

Paris St. Germain  imeanza  msimu  mpya  jana  kwa  ushindi  wa mabao  3-0  dhidi  ya  Caen, kwa  magoli  ya  Neymar, Adrien Rabiot na  Tomothy Weah. Kocha  mpya  wa  PSG Thomas Tuchel aliwaweka  nje  Kylian Mbappe, Edson Cavani  na  Marco Verratti wakati  akianza  msimu  wake  wa  kwanza  na  klabu  hiyo  maarufu ya Uufaransa  na  kuwatumia  chipukizi Colin Dagba, Stanley N'Soki na  Antoine Bernede. PSG ilimaliza  mchezo  huo  ikiwa  na wachezaji  sita waliochini  ya  umri  wa  miaka  20.

 

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / dpae / afpe

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman