Bayern Munich wahifadhi taji la Bundesliga | Michezo | DW | 27.04.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Bayern Munich wahifadhi taji la Bundesliga

Kama ilivyotarajiwa Bayern Munich imetawazwa rasmi jana kuwa mabingwa msimu huu wa Bundesliga kwa mara ya 25. Lakini kocha Pep amesema hawastahili kusherekea sana maana kazi bado ipo

Mabingwa hao watetezi wamevalishwa taji hilo bila ya kusukuma gozi uwanjani baada ya mchezo wa jana kati ya timu mbili zinazoifuata Bayern kileleni , Borussia Moenchengladbach na VFL Wolfsburg inayoshika nafasi ya pili baada ya Bayern. Wolfsburg iliingia uwanjani ikiwa na matumaini ya kuichafulia Bayern sherehe za ubingwa iwapo ingeshinda mchezo huo. Lakini ilikuwa ni Borussia Moenchengladbach iliyofanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wolfsburg na kusababisha shangwe mjini Munich na kila mahali mashabiki wa Bayern waliko. Bayern ina pointi 15 zaidi ya timu inayoifuatia Wolfsburg na kufungwa kwa timu hiyo kuna maana kwamba hakuna tena timu inayoweza kufikia pointi hizo wakati ikibakia michezo minne Bundesliga ifunge pazia lake msimu huu.

Fußball 1. Bundesliga 27. Spieltag Borussia Dortmund - Bayern München

Bayern wana kibarua dhidi ya Dortmund katika nusu fainali ya DFB Pokal

Kwa kucheza vizuri namna hii , sina hofu ya watu wengi kuipenda michezo. Kwa upande mwingine , kwa kiasi fulani shauku inabidi kurejea katika bundesliga. Ukiangalia mchezo wa leo , Gladbach dhidi ya Wolfsburg , timu namba tatu na namba mbili, timu zote zimecheza kama wanafunzi. Iwapo hali ni hiyo, unapata hofu juu ya soka la Ujerumani kwa jumla.

Bayern ambayo inacheza katika nusu fainali ya Champions League barani Ulaya na pia kombe la Ujerumani iliishinda Hertha Berlin kwa bao 1-0 siku ya Jumamosi na imefikisha pointi 76 kutokana na michezo 30 , wakati Wolfsburg ina pointi 61 katika nafasi ya pili.

Paderborn iliyoko katika nafasi ya pili kutoka mwisho ilipoteza uongozi wake wa mabao 2-0 dhidi ya Werder Bremen na kutosheka na sare ya mabao 2-2 jana.

Kocha Bruno Labbadia wa SV Hamburg amepata ushindi muhimu kwa timu yake ambayo imo katika hatari ya kushuka daraja baada ya kuishinda FC Augsburg inayowania nafasi ya kucheza katika ligi ya Ulaya msimu ujao kwa mabao 3-2. Wakati michezo minne imebakia katika msimu huu wa Bundesliga , SV Hamburg ina pointi 28 ikiwa katika nafasi ya 16 , ikiwa na maana ni nafasi ya tatu kutoka mwisho wa msimamo wa ligi. Lakini shangwe zilikuwa hazina mipaka jana mjini Hamburg.

Fußball Bundesliga SV Werder Bremen vs. Hamburger SV

Bruno Labbadia alipata ushindi wake wa kwanza tangu alipojiunga na Hamburg

Imeonekana baada ya mchezo uwanjani. Hii ni hisia, kama vile tumeshinda ubingwa. Ulikuwa ni ushindi muhimu sana, kwa kuwa tuko mkiani mwa ligi. Wiki iliyopita pia tulicheza vizuri lakini tukashindwa, kiakili hii inaumiza sana. Lakini leo tumecheza vizuri na tulistahili kushinda. Utagundua jinsi maisha yalivyo hapa Hamburg. Matokeo mengine yalikuwa pia mazuri, kwa hiyo bado kuna uhai.

Borussia Dortmund timu ambayo msimu huu umekuwa wa kusua sua , hatimaye inaonesha uhai, baada ya kuishinda Eintracht Frankfurt kwa mabao 2-0 siku ya Jumamosi. Kocha Jürgen Klopp baada ya kutangaza kuachana na klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu, amesema hofu ya kushuka daraja sasa haipo tena na ni wakati wa mpambano wa kucheza katika kinyang'anyiro cha Ulaya.

Kama ingekuwa tunaongoza kwa pointi tatu , tusingejisikia salama pia. Kwasasa tuko pointi tatu nyuma ya Schalke na Augsburg. Sasa tunahitaji kusonga mbele. Tunahitaji kujaribu kila kitu kinachowezekana. Tunalazimika kutumia kila kilichoko katika uwezo wetu, ili kuweza kukamilisha msimu huu vizuri. Wakati fursa inakuwapo, kuweza kufanya kitu kidogo kuelekea kileleni, basi tutajaribu.

VFL Stuttgart ambayo bado inainamiwa na jinamizi la kushuka daraja ilishindwa kupata matokeo mazuri na iliridhika na sare ya mabao 2-2 dhidi ya SC Freiburg siku ya Jumamosi , nayo Bayern Leverkusen haikuweza kutamba mbele ya FC Kolon baada ya kutoka sare pia ya bao 1-1 katika mchezo wa watani wa jadi (Derby).

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / ape / rtre
Mhariri: Yusuf , Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com