1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern mabingwa mara ya 6 mfululizo

14 Mei 2018

Msimu wa Ligi Kuu ya Ujerumani ulikwisha Jumamosi na Bayern Munich wakamuaga kocha wao Jupp Heynckes ambaye alitoka kwenye kustaafu na kuchukua nafasi ya Carlo Ancelotti mwanzoni mwa msimu.

https://p.dw.com/p/2xhxt
Bayern München Bundesliga Meisterfeier Schale Heynckes
Picha: Reuters/M. Dalder

Heynckes alichukua uongozi wakati ambapo Bayern walikuwa wanasuasua wakiwa pointi tano nyuma ya vinara wa ligi wakati huo Borussia Dortmund, ila Heynckes aliyabadilisha yote hayo na kulirejesha taji la Bundesliga Allianz Arena. Wamemaliza msimu pointi 21 mbele ya timu iliyoshika nafasi ya pili Schalke.

Bayern Munich lakini walitandikwa magoli mane kwa moja na VfB Stuttgart katika dimba lao la nyumbani katika mchuano huo wa mwisho.

Heynckes mwenye umri wa miaka 73 anaondoka akiwa ameweka rekodi ya kushiriki mechi 1,038 kama mchezaji na kama kocha pia, hiyo ikiwa ni mechi moja zaidi ya Otto Rehhagel, ila ana kibarua kimoja zaidi wikendi ijayo katika fainali ya kombe la Ujerumani DFB Pokal ambapo atapambana na Eintracht Frankfurt inayofunzwa na kocha mpya wa Bayern Niko Kovac na ni baada ya mechi hiyo ndipo atakapomkabidhi mikoba yote Kovac.

FC Cologne wanaongoza walioshuka daraja

Timu zilizofuzu kwenye mashindano ya Ulaya msimu ujao ni Bayern Munich, Schalke waliomaliza wa pili, Hoffenheim na Borussia Dortmund waliomaliza kwenye nafasi ya nne. Timu hizo nne zitashiriki Ligi ya vilabu bingwa Ulaya Champions League. Watakaocheza Europa League ni RB Leipzig ambao waliwazaba Hertha Berlin magoli sita kwa mawili. Stuttgart wao watacheza katika ligi hiyo ila iwapo Bayern Munich watashinda kombe la DFB Pokal.

Bayern München Verabschiedung von Trainer Jupp Heynckes
Jupp Heynckes akiwaaga mashabiki wa BayernPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Schrader

Timu zilizoshuka daraja katika Bundesliga zinaongozwa na FC Cologne ambao walizidiwa nguvu magoli 4 - 1 na VfL Wolfsburg katika mechi ya mwisho, kisha timu ya pekee ambayo ilikuwa haijashushwa daraja katika Bundesliga Hamburg hatimaye imesalimu amri msimu huu baada ya kuponea ponea katika misimu iliyopita. Kuna saa maarufu katika uwanja wa Hamburg ambayo inaonyesha kipindi ambacho klabu hiyo imekuwa katika Ligi ya Ujerumani na wakati kipenga cha mwisho wa mechi yao ya Bundesliga dhidi ya Borussia Moenchengladbach kilipokuwa kinapigwa Jumamosi, saa hiyo ilikuwa inaonyesha miaka 54 siku 261 dakika 36 na sekunde 2. Kwa hiyo sasa hivi hiyo itakuwa historia  kwa Hamburg.

VfL Wolfsburg wao baada ya kumaliza ligi kwenye nafasi ya kumi na sita watajua iwapo watasalia kwenye Bundesliga au watashuka na kushiriki ligi ya daraja la pili baada ya kucheza mechi ya muondoano na Holstein Kiel.

Kutoka daraja la pili timu zilizopanda daraja ni Fortuna Düsseldorf ambao waliebuka mabingwa na Nurnberg halafu Holstein Kiel iwapo watawabwaga Wolfsburg basi watakuwa miongoni mwa timu kumi na nane za Bundesliga msimu ujao.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/DPAE/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga