1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bashir kuhojiwa kuhusu "kufadhili ugaidi"

Bruce Amani
3 Mei 2019

Mwendesha mashitaka mkuu nchini Sudan ameamuru kuhojiwa kwa Rais aliyeondolewa madarakani Omar al Bashir kuhusu madai ya "utakatishaji fedha na kufadhili ugaidi"

https://p.dw.com/p/3Hqn6
Erneut Großdemnonstration der Opposition im Sudan
Picha: picture-alliance/dpa/S. Basheer

Chini ya Utawala wa Bashir, Sudan iliwekwa kwenye orodha ya Marekani ya mataifa yanayofadhili ugaidi kutokana na mahusiano yake na kundi la itikadi kali. Muasisi wa al-Qaeda Osama bin Laden, aliyehusika na mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 mijini New York na Washington mwaka wa 2001, aliishi Sudan kati ya mwaka wa 1992 na 1996.

Jenerali Abdel-Fattah Burhan, mkuu wa baraza la kijeshi, alisema mwezi uliopita kuwa zaidi ya dola milioni 113 pesa taslimu zilipatikana katika makazi ya al-Bashir. Amri hiyo ya kaimu mwendesha mashitaka mkuu Al Waleed Sayyed Ahmed imetolewa wakati mamia kwa maelfu ya waandamanaji wakiendelea kupiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi kulitiaka likabidhi madaraka kwa raia.

Al-Bashir aliondolewa madarakani na kukamatwa na jeshi la Sudan mnamo Aprili 11 baada ya miezi kadhaa ya maandamano ya kupunga utawala wake wa miaka 30. Jeshi na viongozi wa upinzani sasa wanafanya mchakato wa kuunda serikali ya mpito.