Bashir asema maandamano dhidi yake ni halali | Matukio ya Afrika | DW | 01.04.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

AFRIKA

Bashir asema maandamano dhidi yake ni halali

Rais wa Sudan Omar al-Bashir amekiri leo kuwa madai ya waandamanaji wanaoipinga serikali ni halali, lakini amesema yalielezwa kinyume cha sheria na kusababisha vifo vya watu kadhaa.


Bashir amesema mgogoro wa kiuchumi umeathiri sehemu kubwa ya raia wa nchi hiyo, katika hotuba ya kwanza kwa wabunge tangu kutangazwa kwa hali ya dharura mnamo Februari 22 kwa lengo la kuzima maandamano hayo.

Ameongeza kuwa baadhi waliingia mitaani kuelezea matakwa yao ya halali, lakini baadhi ya waliokusanyika walitumia njia haramu kuharibu mali.

Katika siku za mwanzo za maandamano hayo yalioanza Desemba 19, ofisi kadhaa na majengo ya chama tawala cha Bashir vilichomwa moto wakati wa maandamano.

Maafisa wanasema watu 31 wameuawa mapaka sasa katika maandamano hayo, huku shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch likisema idadi ya vifo ni 51.

Bashir mwenye umri wa miaka 75 ambaye aliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi mwaka 1989, awali alitangaza hali ya dharura kwa mwaka mmoja lakini bunge liliipunguza hadi miezi sita.