1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKosovo

Bado hali ni tete Kaskazini mwa Kosovo

Amina Mjahid
31 Mei 2023

Hali imeendelea kuwa tete Kaskazini mwa Kosovo wakati mamia ya watu wa jamii ya Serb kwa mara nyengine tena, wakikusanyika nje ya afisi za baraza la jiji baada ya kukabiliana na Ujumbe wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

https://p.dw.com/p/4S0Xo
Zvecan, Kosovo | erneut Proteste von Serben
Picha: Bojan Slavkovic/AP/picture alliance

Waandamanaji waliokuwa watulivu walikuwa wamebeba bendera ya Serbia iliyokuwa na ukubwa wa mita 200 iliyotokea katika baraza la jiji hadi katikati ya mji wa zvecan. Magari matatu ya wanajeshi wa Kosovo ambao uwepo wao ni kati ya mambo yanayoleta uhasama katika eneo hilo la Kaskazini linalokaliwa na idadi kubwa ya watu wa kabila la serbs,  yalibakia yameegeshwa nje ya jengo hilo. Nao ujumbe wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO nchini Kosovo, ulilizunguka baraza la jiji mjini humo na kulizungushia uzio wa nyaya za senyeng'e.

Serbia yaagiza wanajeshi kuukaribia mpaka na Kosovo baada ya makabiliano ya waandamanaji

Waandamanaji hao wa jamii ya Serb walisusia uchaguzi wa serikali za mitaa Kaskazini mwa Kosovo mwezi Aprili na kutoa nafasi kwa watu wa jamii ya Albania kuchukua udhibiti wa mabaraza ya jiji licha ya idadi ndogo ya watu iliyojitokeza kushiriki katika uchaguzi huo. Waserbia wengi wanataka wanajeshi maalum wa kosovo waondolewe pamoja na ma meya wa jamii ya Albania wanaosema hawawawakilishi.

Marekani kupitia waziri wake wa mambo ya kigeni Anthony Blinken imemkosoa mshirika wake Kosovo na kuilaumu serikali ya Waziri Mkuu Albin Kurti kuchochea mzozo uliopo, kwa kuwaweka ma meya wa jamii ya Albania katika mabaraza ya jiji. Marekani pia imeisimamisha Kosovo kwa muda katika zoezi  lao la pamoja la kijeshi. Blinken ametoa wito kwa pande zote Kosovo na Serbia kuzungumza na kutafuta njia ya haraka ya kusitisha uhasama.

NATO yasema shambulio dhidi ya wanajeshi wake halikubaliki

Stoltenberg in Norwegen
Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg Picha: Heiko Junge/IMAGO

Huku hayo yakiarifiwa ujumbe wa kijeshi wa Jumuiya ya kujihami ya NATO nchini Kosovo KFOR, umetangaza kuwapeleka wanajeshi wake zaidi ya 700 Kaskazini mwa Kosovo,  baada ya wanajeshi wake wengine 30 kujeruhiwa katika maandamano ya jana yaliyojaa vurugu.

Wanajeshi hao walipurwa mawe baada ya kujaribu kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakikabiliana na polisi. Kamanda wa ujumbe wa KFOR jenerali Angelo Michele, amesema mashambulizi dhidi ya ujumbe wake hayakubaliki na kwamba Ujumbe huo utaendelea kutekeleza wajibu wake chini ya sheria ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Nae Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg ameunga mkono tamko hilo.

NATO kutuma wanajeshi 700 zaidi Kosovo, kukabili maandamano

Kosovo ilijitangaza kuwa Huru kutoka kwa Serbia mwaka 2008 lakini Serbia na washirika wake Beijing na Moscow wamekataa kutambua hilo. Wa Serbia walioko Kosovo wanabakia kuwa watiifu kwa taifa lao hasa upande wa Kaskazini walioko kwa wingi na kwa kawaida wanapinga hatua yoyote ya Kosovo kujaribu kuwadhibiti.

Chanzo: afp/ap/dpa