Atletico Madrid kupamana na Real Madrid | Michezo | DW | 28.05.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Atletico Madrid kupamana na Real Madrid

Mshambuliaji hatari wa Real Madrid Cristiano Ronaldo anasisitiza malengo binafsi yatawekwa kando wakati Real Madrid ikiwania kuimarisha rekodi yake Ulaya kwa kuishinda Atletico Madrid katika fainali ya Champions League

Ronaldo, mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka duniani mara tatu , hajafunga bao katika uwanja wa San Siro lakini ana fursa ya kufikia na kuipiku rekodi yake ya kufunga mabao 17 katika Champions League katika msimu mmoja.

Hata haivyo miaka miwili baada ya mlinzi wa Real Sergio Ramos kusawazisha dakika za mwisho kabisa na kulazimisha timu mbili zilizokuwa zinapambana siku hiyo katika fainali kuingia katika dakika za nyongeza na kunyakua taji la kumi mjini Lisbon, mchezaji huyo nyota Mreno anasisitiza kuwa ushindi wa 11 wa taji hilo ni muhimu zaidi kuliko nani anazifunia nyavu katika uwanja huo wa San Siro mjini Milan.

Ushindi utashuhudia Real Madrid ikiimarisha hadhi yake kuwa klabu yenye mafanikio makubwa barani Ulaya baada ya kushinda kombe hilo lilipoanzishwa , wakati huo likiifahamika kama kombe la mabingwa wa Ulaya , mwaka 1956 wakati Hector Rial wa Argentina alipofunga bao la ushindi katika ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya vigogo ambao wamesambaratika hivi sasa Stade Reims mjini Paris.

UEFA Champions League Atletico Madrid vs. Bayern München

Diego Simeone anataka Atletico Madrid kulipiza kisasi

Mafanikio ya Atletico huenda ni dhaifu kwa kufananisha na Real , lakini kitisho kutoka kwa vijana wa Diego Simeone ambao wamefanikiwa kuibana Real na kuweza kushinda mchezo mmoja tu katika mapambano yao 10 yaliyopita tangu mwaka 2014, si cha kubeza.

Kabla ya kushinda mataji mawili ya Ligi ya Ulaya, Europa League mwaka 2010 na 2012, kikosi hicho kinachojulikana kama "Rojiblancos" kilinyakua ubingwa wake wa mwisho wa kombe la bara hilo kwa vilabu mwaka 1962 ambapo walinyakua kombe la washindi barani Ulaya, Cup Winners Cup.

Mji wa Milan imefurika mashabiki kutoka kila pembe ya dunia kushuhudia pambano hilo kubwa la mwisho kwa vilabu msimu huu katika bara la Ulaya. Meya wa jiji la Milan Giuliano Pisapia amesema amefurahishwa na ukweli kwamba pambano hilo linafanyika katika mji wake. "Tumefanyakazi kwa miaka kadhaa ili kuweza kuwa wenyeji wa fainali ya kombe la Champions League, tumefanikiwa kuileta fainali hii mjini Milan. Tumeshinda. Ni furaha kuu kwa wakaazi wa Milan na watalii wengi na mashabiki ambao watakuwapo mjini Milan katika siku hizi.

Daniel Carvajal Real Madrid

Real iliishinda Atletico 4-1 mwaka wa 2014

Miaka miwili iliyopita Atletico ilikuwa karibu na kulipiza kisasi kwa kipigo walichopata kutoka kwa Bayern Munich katika fainali ya Champions League mwaka 1974 kwa kufungwa mabao 4-0 baada ya Diego Godin kuwapa vijana wa Simeone kifungua kinywa katika mchezo huo katika dakika ya 39.

Bao la Sergio Ramos katika dakika ya 93, hata hivyo, lilisababisha mchezo huo kuingia katika dakika za nyongeza, ukiwa ni mwanzo mpya kabisa katika mchezo huo, ambapo Gareth Bale, Marcelo na Ronaldo , walipachika mabao na kuiacha Atletico Madrid ikiwa imeduwaa.

Hivi sasa ni Ronaldo, Bale na mshambuliaji wa Ufaransa Karim Benzema ambao wanaweza kuziona juhudi zao zikitulizwa, wakati Ramos na Pepe , ambao wanapendelewa na Zinedine Zidane kuwa walinzi wa kati , watakuwa na wasi wasi wa kujirudia kwa historia.

Atletico Madrid imeweza kutoka uwanja bila kuchafuliwa katika michezo 35 kati ya 56 msimu huu, ikiwa ni pamoja na kupigiana mikwaju ya penalti katika ligi ya nyumbani La Liga nyumbani kwa Barcelona na Bayern Munich ambapo timu hizo zilifungishwa virago nje ya kinyang'anyiro hicho.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com