1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Arsenal na Liverpool wabeba bendera ya England Ulaya

19 Machi 2026

Arsenal na Liverpool pekee ndizo zimebaki kuiwakilisha Premier League baada ya Manchester City, Chelsea, Newcastle na Tottenham kutolewa hatua ya 16‑bora, huku wachambuzi wakilaumu uchovu na ratiba ngumu ya EPL.

https://p.dw.com/p/5AhQB
Champions League 2026 |
Kwa sasa, Arsenal na Liverpool zimebaki kubeba bendera ya England barani Ulaya.Picha: Dennis Ewert/RHR-Foto/IMAGO

Hatua ya 16-bora ya Ligi ya Mabingwa imeweka rekodi isiyo ya kawaida kwa timu za ligi ya Premier. Kati ya timu sita za England zilizofuzu hatua hiyo, ni Arsenal na Liverpool pekee ndizo zilizofanikiwa kusonga mbele.

Kwa mara ya kwanza katika historia, timu zote sita za Premier League zilifika hatua ya mtoano, huku tano zikimaliza ndani ya nafasi nane za juu kwenye hatua ya makundi. Hata hivyo, mafanikio hayo hayakudumu.

Manchester City, Chelsea, Newcastle United na Tottenham Hotspur zote zilitolewa — ikiwa ni mara ya kwanza timu nne kutoka taifa moja kutolewa kwa pamoja katika hatua ya 16 bora. Kwa pamoja, ziliruhusu mabao 28, ishara ya udhaifu mkubwa katika safu zao.

Hali hii inapingana na mwenendo wa miaka ya karibuni. Kati ya 2018 na 2023, timu za England zilifika angalau fainali moja katika misimu mitano kati ya sita, zikitawala nusu fainali na kushinda taji mara tatu.

Uchovu na Ratiba Ngumu

Ligi ya Premier inaendelea kuwa ligi yenye ushindani mkali zaidi barani Ulaya. Ratiba nzito, muda mdogo wa kupumzika na presha ya kila wiki huwafanya makocha kuchezesha vikosi kamili bila nafasi ya kupumzisha wachezaji.

UEFA Champions League
Liverpool imefanikiwa kutinga kwa robo fainali licha ya matokoe ya kusuasua katika ligi ya England.Picha: Richard Sellers/Sportsphoto/IMAGO

Kocha wa Chelsea, Liam Rosenior, alisisitiza hilo baada ya kutolewa:

"Wamecheza zaidi ya mechi 100 ndani ya miezi 18… wasipodhibitiwa muda wao wa kucheza, uwezekano wa kuumia unaongezeka sana.”

Tofauti na England, timu kubwa za Ulaya bara zina uwezo wa kupumzisha wachezaji mara kwa mara kutokana na ligi zao kuwa na ushindani mdogo. Mfano mzuri ni Real Madrid, ambayo msimu huu imetumia wachezaji 32 katika La Liga.

Athari za uchovu zilionekana wazi kwa Newcastle, ambao walidhoofika vibaya kipindi cha pili kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Barcelona, wakafungwa 4–1 na kutolewa kwa jumla ya mabao 8–3.

Mchezaji wa zamani wa Liverpool, Stephen Warnock, alieleza tofauti ya kipaumbele:

"Kwa Real Madrid, kila kitu ni kuhusu Ligi ya Mabingwa, ilhali England ni kuhusu kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa msimu unaofuata.”

Mtazamo wa Kiufundi

Soka la England linategemea kasi na nguvu, lakini hatua za mtoano za Ligi ya Mabingwa zinahitaji utulivu, udhibiti wa mchezo na uzoefu wa kimataifa. Hili ndilo eneo ambalo timu nyingi za Premier League zimeonekana kupwaya msimu huu.

Kwa sasa, Arsenal na Liverpool ndizo zimebaki kubeba bendera ya England barani Ulaya. Safari yao itategemea uwezo wa kudhibiti mchezo na kuepuka kujiamini kupita kiasi - jambo ambalo linaweza kuwa tofauti kati ya mafanikio na kutolewa mapema.