1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Algeria yashindwa kulitetea taji lake AFCON

Grace Kabogo
21 Januari 2022

Vigogo wa soka wanazidi kuyaaga mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON baada ya Ivory Coast kuwafunga mabingwa watetezi wa kombe hilo, Algeria mabao 3-1.

https://p.dw.com/p/45rqk
AFCON Algerien vs Elfenbeinküste
Picha: Themba Hadebe/AP Photo/picture alliance

Franck Kessie aliifungia Ivory Coast goli la kwanza katika dakika ya 22 na Ibrahim Sangare alifunga bao la pili katika dakika ya 39 kwenye mchezo huo uliofanyika mjini Douala, huku Nicolas Pepe akiifungia Ivory Coast bao la tatu baada ya kipindi cha mapumziko katika dakika ya 54 na kushika nafasi ya kwanza katika kundi E.

Algeria ilijipatia bao lake katika dakika ya 60 baada ya Riyad Mahrez kufunga katika kipindi cha pili kwa mkwaju wa penalti uliotolewa baada ya Youcef Belaili kuchezewa rafu.

Kocha aridhishwa na mchezo

Kocha wa Ivory Coast, Mfaransa Patrice Beaumelle, ambaye ameshinda mara mbili mashindano ya AFCON kama kocha msaidizi amesema ameridhika namna timu yake ilicheza jana. Hata hivyo, ameelezea kusikitishwa na kushindwa kwa Algeria kutetea taji lake.

Guinea ya Ikweta imeshika nafasi ya pili katika kundi E baada ya kuifunga Sierra Leone bao 1-0 katika mchezo uliochezwa mjini Limbe. Pablo Ganet aliipatia ushindi Guinea ya Ikweta katika dakika ya 38. Kei Kamara alikosa penalti dhidi ya timu yake Sierra Leone.

Matokeo hayo ya kundi E yanaiwezesha pia Comoro kutinga katika hatua ya 16 bora na itacheza na wenyeji Cameroon.

Africa Cup Mali und Mauretanien
Wachezaji wa Mali, Massadio Haidara na Moussa DoumbiaPicha: Charly Triballeau/AFP/Getty Images

Kwa upande wa kundi F Mali inaongoza baada ya kuifunga Mauritania mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa mjini Douala, huku Massadio Haidara akiipa ushindi katika dakika ya pili, kabla ya Ibrahima Kone hajaongeza bao kwa mkwaju wa penalti mwanzoni mwa kipindi cha pili. Mauritania inarejea nyumbani bila ya kuwa na pointi wala kupata hata bao moja la faraja.

16 bora kuanza Jumapili

Wakati Sierra Leone inaondoka, Guinea ya Ikweta inabaki Limbe ambapo itacheza na Mali Januari 26 katika hatua ya 16 bora.

Bao la Ablie Jallow iliipatia Gambia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tunisia katika mchezo uliopigwa mjini Limbe. Gambia sasa itacheza na Guinea katika hatua ya 16 bora mjini Bafoussam Jumatatu ijayo. Timu ya Tunisia iliwakosa wachezaji wake 12 ambao waliambukizwa virusi vya corona sikua moja kabla ya mchezo huo, akiwemo nyota wa timu hiyo Wahbi Kahzri.

Mechi za hatua ya 16 bora zitaanza siku ya Jumapili kwa Burkina Faso kucheza na Gabon mjini Limbe na Nigeria kucheza na Tunisia mjini Garoua.

(AFP, Reuters)