1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Alain Le Roy

1 Julai 2008

Mjumbe mpya anaeongoza vikosi vya kuhifadhi amani vya UM.

https://p.dw.com/p/EUJ6

Mjumbe wa kibalozi wa kifaransa Alain Le Roy, jana alikabidhiwa jukumu zito la kuongoza vikosi vya kuhifadhi amani vya Umoja wa Mataifa.

Ametwikwa jukumu hilo katika wakati ambao askari wa kuhifadhi amani wa UM wanahitajika zaidi duniani kuliko wakati wowote ule kabla.

Alain Le Roy anachukua wadhifa ulioachwa na Jean-Marie Guehenno,mfaransa mwengine alieongoza Idara ya UM ya juhudi za kuhifadhi amani mnamo miaka 8 iliopita.Chini ya uongozi wake,juhudi za kuhifadhi amani za UM ziliongezeka mno kuliko wakati wowote kabla.Kumekuwapo vikosi 20 zaidi vya kuhifadhi amani kila pembe ya dunia vikijumuisha hadi askari laki moja.

Tangu Septemba mwaka jana,Le Roy,mwenye umri wa miaka 55,amekuwa balozi wa Ufaransa mwenye dhamana ya mradi aliouanzisha rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa wa kuunganisha Umoja wa Ulaya na nchi 6 za Afrika ya kaskazini zenye kupakana na bahari ya Mediterranean.

Le Roy, ni mwanadiplomasia anaetumika muda baada ya muda.Aliwahi kutumwa Balkan kuongoza juhudi za kujenga upya huduma za umma baada ya kumalizika vita vya Bosnia.Alitumika kama naibu wa katibu mkuu wa UM 1995.

Kati ya 1999-2000,Le Roy aliteuliwa mtawala wa eneo la Pec,magharibi mwa Kosovo, iliokua sehemu ya utawala wa mpito wa UM.Hii na baada ya kutimuliwa huko kwa vikosi vya Serbia na vile vya shirika la ulinzi la magharibi (NATO).

Mwezi Mei, mwaka huu, Umoja wa Mataifa uliadhimisha mwaka wake wa 60 tangu kuazinshwa kikosi cha kuhifadhi amani.licha ya mashtaka yaliotolewa kwa baadhi ya maafisa wake ya kuhusdika na ngono na rushua,vikosi vya kuhifadhi amani vya UM vinatakiwa sehemu mbali mbali za dunia.

UM hauna jeshi lake,bali vikosi huchangiwa na nchi zanacahama.Leo hii ,wanachama 120 wa Umoja huo wamechangia askari hadi 110.000 tangu wake hata wakiume. Nchi iliochangia askari wengi zaidi ni Pakistan,Bangladesh,India,Nigeria na Nepal.Kwa pamoja nchi hizo zinachangia 40% ya askari wote wa kuhifadhi amani wa UM.

Umoja wa Ulaya,Marekani na japan ndizo usoni kabisa katika kubeba gharama zake ambazo sasa zimefikia jumla ya dala milioni 7.5.

Gueheno,mwenye umri wa miaka 58 alipongeza sherehe za maadhimisho ya hapo Mei ya vikosi vya kuhifadhi amani vya UM kwa kujitoa mhanga na kujitolea kutekeleza malengo matukufu ya UM.

Alitaja kwamba askari 90 wa kuhifadhi amani wa UM waliuwawa katika kazi zao mwaka jana na hii imefanya jumla ya waliofariki tangu kuasisiwa kwa kikosi hiki miaka 60 iliopita kufikia zaidi ya 2,400.

Idara ya mjumbe huyo wa zamani Guehenno, imeongoza zadi ya mipango 63 ya kuhifadhi amani tangu ule wa kwanza kabisa wa Mei 29,1948.Wakati ule, kikosi kisicho na silaha kilipewa jukumu la kusimamia amani katika ardhi za wapalestina.

Vikosi vya kuhifadhi amani vya UM vinatumika leo nchini Haiti,Timor ya Mashariki na kuanzia Georgia hadi Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Duru za UM zinaarifu sio tu mipango ya kuhifadhi amani ya vikosi hivi imeongezeka,bali imezidi kutatanisha.Mpango mkubwa wenye kutatanisha zaidi kati ya yote hadi sasa, ni kikosi cha pamoja cha kuhifadhi amani cha Ushirika baina ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa (UNAMID) kwa ufupi.

Hiki ni kikosi kinachowahifadhi wakaazi wa Dafur, magharibi mwa Sudan.

Kuwekwa huko kwa kikosi cha askari 26,000-mojawapo ya vikosi vikubwa kabisa vya aina hii ulimwenguni,kunazusha changamoto kubwa za kiufundi,kimipango na kisiasa.

Kwani, miezi 6 tangu kuanzishwa, kimejipatia askari 9,000 tu.

Huu ndio mzigo mzito anaujitwika ,mwanabalozi wa kifaransa Alain Le Roy kama mkuu wa kikosi cha kuhifadhi amani cha UM.