1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Afrika Kusini kuandaa mkutano wa BRICS wiki hii

Tatu Karema
21 Agosti 2023

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema nchi yake haitalazimishwa kuunga mkono taifa lolote lenye nguvu duniani, wakati inapojiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa mataifa yanayoinukia kiuchumi duniani BRICS

https://p.dw.com/p/4VOwm
Indien Goa | Treffen Präsident Putin, Premierminister Modi und Xi Jinping
Picha: Anupam Nath/AP/picture alliance

Katika hotuba yake kwa taifa kupitia televisheni Jumapili (20.08.2023), Rais Ramaphosa alisema nchi yake imepinga shinikizo la kuegemea taifa lolote kati ya mataifa yenye nguvu duniani au makundi ya mataifa yenye ushawishi. Ramaphosa aliongeza kuwa wakati baadhi ya wapinzani wao wanapendelea kuungwa mkono waziwazi kuhusu chaguo lao la kisiasa na kiitikadi, taifa hilo halitavutiwa katika ushindani kati ya mataifa yenye nguvu.

Soma pia: Rais Xi kuhudhuria mkutano wa BRICS Johannesburg

Uhusiano kati ya Afrika Kusini na Urusi waangaziwa

Kuandaliwa kwa mkutano huo nchini Afrika Kusini kumesababisha kuangaziwa kwa uhusiano wake na Ikulu ya Kremlin, hasa kwa vile imekataa kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Ramaphosa atajumuika katika mkutano huo wa BRICS na Rais Xi Jinping wa China, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva. Urusi itawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov, huku Rais Vladmir Putin akishiriki kupitia mtandao.

Tazama pia: 

Xi Jinping awasili Afrika Kusini

Putin aliamua kutohudhuria mkutano huo binafsi kwa sababu anaandamwa na waraka wa kukamatwa la Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, ambao kimsingi Afrika Kusini inapaswa kuitekeleza.

BRICS sio kundi bali uhusiano wa maendeleo

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa (Kushoto) na rais wa Urusi Vladmir Putin ( Kulia) wakati wa mkutano wa 11 wa BRICS katika ikulu ya Itamaraty mnamo Novemba 14, 2019
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa (Kushoto) na rais wa Urusi Vladmir Putin ( Kulia)Picha: Mikhail Metzel/ITAR-TASS/IMAGO

Akizungumzia uhusiano huo wa mataifa ya BRICS, Siyabonga Cyprian Cwele, balozi wa Afrika Kusini nchini China amesema kuwa 
BRICS sio kundi na hawashindani na makundi mengine yoyote ya kimataifa. Cwele ameongeza kuwa BRICS ni ushirikiano wa maendeleo na ingawa vyombo vya habari vinaweza kujaribu kuwatenganisha, wanaheshimiana sana kwa sababu wanajua kinachowaunganisha.

Soma pia: Afrika Kusini yapata ukakasi kumkamata Putin

Urusi na China kusaka kunufaika zaidi

Wakati wa mkutano huo wa kilele, Urusi na China zitakuwa zinasaka kunufaika zaidi kisiasa na kiuchumi katika mataifa yanaoyoendelea. Malalamiko ya pamoja dhidi ya mataifa ya Magharibi kutoka kwa mataifa hayo yanayoendelea huenda yakachukuwa mwelekeo mkali zaidi kwa kuileta karibu Saudi Arabia.

Mkutano huo wa kilele wa siku ya Jumatano na mikutano ya pembezoni siku ya Jumanne na Alhamisi, inatarajiwa kutoa miito ya jumla ya ushirikiano zaidi miongoni mwa mataifa ya Kusini huku kukiwa na ongezeko la kutoridhika kuhusu dhana ya uongozi wa mataifa ya Magharibi  katika taasisi za kimataifa.