1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
1 Aprili 2022

Yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika ni pamoja na kuhusu msimamo wa nchi za jumuiya ya BRICS katika vita vya Ukraine. Je amani imerejea nchini Ethiopia baada ya vita vya nchini humo kumalizika?

https://p.dw.com/p/49LLU
BRICS Virtuelles Gipfeltreffen 2021
Picha: BRICS Press Information Bureau/AP/picture alliance

Handelsblatt 

Gazeti la Handelsblatt limeandika kuhusu vita vya Ukraine mbapo linazungumzia juu ya msimamo wa nchi za jumuiya ya BRICS inayoijumuisha Urusi. Linauliza jee nchi za jumuiya hiyo ikiwa pamoja na Afrika Kusini zimesimama wapi katika vita vya nchini Ukraine. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba Afrika Kusini haikushiriki katika kupiga kura kwenye baraza kuu la Umoja wa Mataifa  lililolenga shabaha ya kupinga uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Jumuiya ya Brics inazileta pamoja, Urusi, China, India, Afrika Kusini na Brazil. Handelsblatt linasema ingawa nchi hizo hazijajitenga na Urusi kwa uwazi, haziungi mkono kwa uwazi uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesisitiza kwamba ingeliwezekana kuviepusha vita vya nchini Ukraine endapo jumuiya ya kijeshi ya NATO isingelijitandaza Ulaya ya mashariki.

Gazeti la Handelsblatt linakumbusha aliyosema waziri  wa mambo ya nje wa hapo awali wa Afrika Kusini, Maite Nkoana Mashabane kwamba historia ya nchi za Brics ni moja kutokana na harakati za kupinga ukoloni na katika harakati hizo Urusi iliziunga mkono nchi hizo.

Neue Zürcher 

Gazeti la Neuer Zürcher linauliza iwapo amani imerejea nchini Ethiopia baada ya vita vya nchini humo kumalizika? Gazeti hilo linatilia maanani kwamba serikali kuu ya Ehtiopia kwa upande wake imeamua kusimamisha mapigano baada ya mapambano ya miezi kadhaa na waasi wa jimbo la Tigray.

Gazeti la Neuer Zürcher limeikariri serikali ya Ehtiopia ikieleza kuwa  imesimamisha vita ili kuruhusu misaada ya mahitaji muhimu kupelekwa kwenye jimbo laTigray la kaskazini  mwa Ethiopia. Watu zaidi ya asilimia 90 yaani takriban watu milioni sita wa jimbo hilo wanategemea msaada wa chakula kutoka nje.

Gazeti linatilia maanani kwamba tangu mwezi Desemba mwaka uliopita misafara zaidi ya misaada ya chakula imekuwa inaongezeka inayokwenda kwenye jimbo la Tigray. Wakati huo huo gazeti linaripoti kwamba wapiganaji wa Tigray wamesema wao pia wapo tayari kusimamimisha mapigano.

die tageszeitung 

Gazeti la die tageszeitung linafuatilia matukio ya nchini Mali na linasema nchi hiyo inapiga hatua za haraka ili kurejea kwenye demokrasia. Linasema hayo yanatokana na juhudi zilizofanywa za kurejesha maelewano kati ya viongozi wa kijeshi wa Mali na jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi Ecowas. Mkutano maalumu umefanyika nchini Ghana kujadili mustakabali wa  kiongozi wa wanajeshi Kanali Assimi Goita. Gazeti la die tageszeitung linatukumbusha kwamba wanajeshi walitwaa madaraka miaka miwili iliyopita  nchini Mali na ndiyo sababu nchi hiyo ilisimamishwa  uanachama kwenye jumuiya ya Ecowas.

Die tageszeitung linaeleza kwamba baada ya ziara ya mjumbe wa Ecowas, wanajeshi waliotwaa mamlaka wamekubali kurejesha demokrasia haraka. Pamoja na kurejesha demokrasia gazeti hilo linasema jeshi la Mali pia linapaswa kuungalia uhusiano wake na mamluki kutoka nje. Gazeti la die tageszeitung linaeleza kwamba suala hilo ni muhimu katika uhusiano wa nchi hiyo na Umoja wa Ulaya.

Süddeutsche 

Gazeti la Süddeutsche linazungumzia juu ya ukame wa muda mrefu kwenye eneo la Afrika Mashariki. Gazeti linasema jumuiya ya kimataifa haiyatilii maanani maafa hayo. Linatahadharisha kwamba eneo hilo limo katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa. Gazeti la Süddeutsche limemnukulu mfanyakazi wa shirika la chakula duniani,WFP, akisema kuwa hapo zamani ilikuwapo mifugo kem kem kwenye sehemu ya Kenya kaskazini.

Mfanyakazi huyo Thomsom Phiri amesema wafugaji walimiliki kondoo, mbuzi, ngamia na ng`ombe wengi sana. Lakini gazeti linasema ukame tayari umeshasababisha maafa makubwa kwenye pembe ya  Afrika. Gazeti hilo linatuarifu kwamba akina mama  wanatembea umbali wa hadi kilometa 15 ili kuweza  kupata maji. Watu wapatao milioni 14 nchini Kenya, Ethiopia na Somalia hawapati chakula cha kutosha kutokana na mavuno hafifu hali iliyosababishwa na ukame.

Mavuno yalipungua kwa asilimia 87 katika eneo hilo la pembe ya Afrika. Gazeti la Süddeutsche linasema mabadiliko ya tabia nchi yamechangia kwa kiasi kikubwa katika maafa hayo lakini linasema hali inaweza kuwa mbaya zaidi kutokana na macho ya dunia kuangazia kwenye vita vya nchini Ukraine.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen