1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
4 Februari 2022

Jaribio la kuiangusha serikali nchini Guinea Bissau, Kufunguliwa mpaka baina ya Uganda na Rwanda ni baadhi ya masuala na matukio yalivyozingatiwa kwenye magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii.

https://p.dw.com/p/46ViV
Guinea-Bissau | Präsident Umaro Sissoco Embalo mit Militär
Picha: Iancuba Danso/DW

Neue Zürcher Zeitung

Makala ya gazeti la Neue Zürcher inazungumzia juu ya Jaribio la kuiangusha serikali nchini Guinea Bissau. Gazeti hilo linasema rais wa nchi hiyo Umaro Sissoco Embalo aliponea chupuchupu kupinduliwa. Watu waliokuwa na silaha walijaribu kulivamia kasri la rais ambamo rais Sissoco Embalo alikuwa anakutana na baraza lake la mawaziri. Hata hivyo jaribio hilo lilizimwa na majeshi ya usalama baada ya mapigano ya saa kadhaa.

Gazeti la Neue Zürcher limemnukulu rais Sissoco Embalo akieleza kwamba watu waliojaribu kuipindua serikali ni wale wanaopinga juhudi za serikali yake za kupambana na biashara ya mihadarati na pia juhudi za kupambana na ufisadi. Gazeti la Neue Zürcher linakumbusha kwamba mnamo miezi ya hivi karibuni Guinea Bissau ilikabiliwa na mvutano mkubwa baina ya rais na waziri mkuu. Linasema mvutano huo ulisababisha kuachishwa kazi kwa waziri mkuu na kuvunjwa kwa bunge.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung limeandika habari njema juu ya mapatano yaliyofikiwa baina ya Uganda na Rwanda juu ya kufungua mpaka baina yao baada ya kufungwa kwa muda wa takriban miaka mitatu. Gazeti linasema mapema wiki hii daraja la Gatuna lilifunguliwa kwa sherehe kubwa. Awali kila upande uliulaumu mwengine kwa kufungwa kwa daraja hilo la mpakani. Rwanda ilidai kwamba Uganda ilikuwa inawauanga mkono waasi wanaoipinga serikali ya Rwanda. Lakini Uganda iliyakanusha madai hayo. Hata hivyo gazeti la die tageszeitung linasema kufungwa kwa mpaka huo kulisababisha hasara ya dola zaidi ya milioni 200. Usafirishajai wa bidhaa kati ya nchi hizo mbili ulisimamishwa.

Gazeti hilo linatilia maanani kwamba juhudi za upatanishi zilizofanywa na viongozi wa Kenya, Jamuhuri  ya Kidemokrasia ya Kongo na Angola zilishindikana. Hata hivyo gazeti linasema baada ya ziara ya mtoto wa rais Yoweri Museveni mambo yalibadilika na kuwa mazuri. Muhoozi Kainerubaga ambaye pia ni kiongozi wa jeshi nchini Uganda alipokewa kwa moyo mkunjufu na rais Paul Kagame. Gazeti la die tageszeitung limemnukulu rais Kagame akisema nchi yake pamoja na Uganda zinaweza kuyasuluhisha masuala mengi ikiwa zitafanya juhudi.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankurter Allgemeine lnaizungumzia juu ya mvutano wa kidiplomasia baina ya Mali na Ufaransa. Linasema mvutano huo umepamba moto baada ya balozi wa Mali kuambiwa aondoke Ufaransa. Hapo awali balozi wa Ufaransa nchini Mali alifungishwa virago. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema hiyo ni mara ya kwanza kwa balozi wa Ufaransa kufukuzwa nchini Mali tangu nchi hiyo ijipatie uhuru mnamo mwaka 1958.

Gazeti hilo limemnukulu waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa akilalamika juu ya uwepo wa mamluki wa Urusi nchini Mali ambao kwa sasa wanapambana na magaidi. Ufaransa pia imelalamika juu ya uamuzi wa Mali wa kuahirisha uchaguzi, linasema kwa upande wake Mali nayo imelalamika juu ya tabia za kikoloni za Ufaransa.

Serikali ya Mali pia inapinga Ufaransa kujipa mamlaka ya kuamua juu ya kuwekwa kwa askari nchini Mali wanaotoka nchi nyingine za Umoja wa Ulaya. Gazeti linafahamihsa kwamba wanajeshi 53 wa Ufaransa wameshauawa tangu kuanza kutekeleza jukumu la kupambana na magaidi nchini Mali mnamo mwaka 2013. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema baadhi ya wanasiasa nchini Ufaransa wanataka majeshi yote ya nchi yao yaondolewe kutoka Mali baada ya kuzuka kwa mvutano wa kidiplomasia.

Handelsblatt

Gazeti la masuala ya kibiashara la Handelsblatt limechapisha makala juu ya ushirikiano baina ya bara la Ulaya na Afrika katika uzalishaji wa nishati. Mwandishi wa makala hiyo Werner Hoyer ambaye ni mwenyekiti wa benki ya Ulaya ya vitega uchumi anasema Ulaya na Afrika zishirikiane katika ulinzi wa mazingira. Hoyer anasema juhudi za pamoja zinapaswa kuchukuliwa tangu mwanzo kabisa wa mradi huo wa kuzalisha nishati endelevu. Amesema malengo yote ya bara la Ulaya ya kulinda mazingira hayataleta matunda ikiwa watu barani Afrika wataendelea kutumia makaa ya mawe na gesi kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao ya nishati.

Katika makala hiyo mwandishi anatilia maanani kwamba takriban nusu ya watu barani Afrika hawapati huduma ya umeme. Pia ameziambia nchi za Ulaya kwamba zitaweza kukidhi mahitaji yao yote ya nishati ikiwa zitazalisha nishati hizo barani Afrika na kuzisafirisha hadi Ulaya. Mwenyekiti huyo wa benki ya Ulaya ya vitega uchumi Werner Hoyer ameandika makala hayo kabla ya mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya na wa Umoja wa Afrika utakaofanyika mjini Brussels, Ubelgiji baadae mwezi huu.

Vyanzo:Deutsche Zeitungen