1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
19 Novemba 2021

Yaliyozingatiwa na magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika mnamo wiki hii ni pamoja na mashambulio ya kujitoa mhanga nchini Uganda. Mgogoro wa nchini Ethiopia na juu ya juhudi za kurejesha demokrasia nchini Sudan.

https://p.dw.com/p/43FrY
Uganda Explosion in Kampala
Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

die tageszeitung:

Gazeti la die tageszeitung ambalo limeandika juu ya mashambulio ya kujitoa mhanga nchini Uganda. Watu kadhaa walikufa baada ya mabomu mawili kulipuka kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Kampala. Katika mashambulio hayo watu 30 wengine walijeruhiwa ikiwa pamoja na polisi 15. Polisi ya Uganda imesema magaidi wamefanya mashambulio hayo kwa kujitoa mhanga. Gazeti la die tageszeitung limelinukulu shirika la upelelezi la Uganda likisema  magaidi wa ndani wanaohusiana na kundi la kigaidi la ADF ndio waliotenda uhalifu huo wa mauaji.

Msemaji wa polisi ya Uganda amekaririwa na gazeti hilo akitahadharisha kwamba watu wote wa Uganda wanakabiliwa na tishio kubwa la magaidi. Gazeti hilo linasema hofu kubwa imetanda nchini Uganda kwa sababu uhalifu huo umetendeka wiki moja baada ya kufanyika mashambulio kadhaa ya kigaidi nchini humo. Gazeti la die tageszeitung linatilia maanani kwamba kundi la kigaidi lanalojiita Dola la Kiislamu IS limedai kuhusika na mashambulio hayo! Kundi hili limejitandaza katika nchi kadhaa barani Afrika, kuanzia Somalia, Msumbiji hadi Kongo.

Neue Zürcher Zeitung:

Nalo gazeti la Neue Zürcher linatilia maanani kwamba mashambulio hayo ni ya tatu kufanyika katika muda mfupi. Linakumbusha kwamba mwishoni mwa mwezi Oktoba mtu mmoja aliuliwa kwenye mkahawa baada ya bomu kulipuka. Watu wengine kadhaa walijeruhiwa katika shambulio hilo. Siku chache tu baada ya hapo watu kadhaa pia walijeruhiwa baada ya bomu kulipuka ndani ya basi karibu na mji mkuu, Kampala. Gazeti la Neue Zürcher linasema kundi la kigaidi ADF limedai kuhusika na mashambulio hayo na linatanabahisha kwamba kundi hilo limejiunga na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS. Gazeti hilo linaeleza kuwa magaidi hao wanafanya mashambulio katika nchi za Afrika ambazo zilijunga na juhudi za kimataifa za kupambana na kile ambacho magaidi hao wanakiita Dola la Kiislamu.

Die Welt:

Gazeti la Die Welt wiki hii linauzungumzia mgogoro wa nchini Ethiopia. Linasema vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muda mrefu vinanyemelea nchini humo. Gazeti hilo limeelezea wasi wasi juu ya kuenea kwa mgogoro huo kwenye ukanda wa Pembe ya Afrika. Limemnukuu waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken akisema mapigano ya nchini Ethiopia yanaweza kuzihusisha nchi za jirani vilevile. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba mgogoro wa nchini Ethiopia unaweza kuchukua muda mrefu kwa sababu jeshi la Tigray, TPLF lina wapiganaji wengi na kwa sasa wapiganaji hao wanadhibiti miji kadhaa na wanasonga mbele kuelekea upande wa mji mkuu Addis Ababa.

Gazeti la Die Welt linasema serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed haikupiga hesabu zake vizuri juu ya nguvu za jeshi la waasi wa Tigray wa jimbo la kaskazini mwa Ethiopia. Sasa makundi mengine ya waasi yamejiunga na jeshi la TPLF. Gazeti la Die Welt linasema njama za serikali ya Ethiopia za kujaribu kuwadunisha wapiganaji wa TPLF hazitafua dafu. Gazeti hilo linasema barani Ulaya mgogoro wa nchini Ethiopia unafuatiliwa kwa wasi wasi mkubwa kutokana  na nchi hiyo kwa mara nyingine kuwa njia kuu ya wakimbizi wanaoingia barani Ulaya.

Der Tagesspiegel:

Gazeti la Der Tagesspiegel linasema juhudi za kurejesha demokrasia nchini Sudan zinaendelea kutatizika baada ya nchi za magharibi kushindwa kumshawishi kiongozi wa wanajeshi waliotwaa madaraka nchini Sudan Abdel Fattah al Burhan kugeuza uamuzi wake. Badala yake jenerali Fattah al Burhani anaendelea kuimarisha utawala wake wa kijeshi kwa kuwateua wajumbe wapya bila ya kuzingatia maslahi ya jumuiya za kiraia zilizotoa mchango mkubwa katika kumng'oa dikteta Omar al Bashir.

Gazeti la Der Tagesspiegel linasema jenerali Fattah al Burhani ameshawaweka watu wake kwenye sehemu muhimu za uongozi nchini Sudan. Hata hivyo, linatilia maanani kwamba wapinzani wa utawala wa kijeshi nchini humo wanaendelea na juhudi za upinzani kwa kufanya maandamano kila siku kila mahala.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen