1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Babu Abdalla
10 Septemba 2021

Miongoni mwa yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika ni pamoja na matukio ya nchini Guinea. Jacob Zuma atolewa jela kutokana na afya yake mbaya na Nigeria kuifufua sekta ya usafiri wa njia za reli.

https://p.dw.com/p/409zU
Guinea Conakry | Videostill von mutmaßlicher Festnahme von Guineas Präsident Alpha Conde durch Militäreinheiten
Picha: AFP

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche ambalo limeandika juu ya matukio ya nchini Guinea ambako wanajeshi wametwaa madaraka. Gazeti hilo linasema nchini Guinea watu wameshangilia kuangushwa kwa utawala wa rais Alpha Conde lakini nje hatua ya wanajeshi hao imelaaniwa.

Kikosi maalumu cha wanajeshi ndicho kilichomwondoa madarakani rais huyo na kumkamata. Hata hivyo gazeti la Süddeutsche linasema iwapo wanajeshi hao wataendelea kudhibiti mamlaka ni jambo lisilojulikana kwa sasa. Linatilia maanani kwamba serikali za Mali, Tchad na Guinea zimeangushwa mnamo muda wa miezi mitano magharibi mwa Afrika.

Gazeti linasema Marekani, Umoja wa Mataifa, Ufaransa, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika zimelaani hatua iliyochukuliwa na wanajeshi nchini Guinea. Süddeutsche linaeleza kwamba hapo awali rais Conde alichaguliwa kwa njia za kidemokrasia na kutumikia mihula miwili lakini baadae aliibadilisha katiba ili kuendelea na muhula wa tatu.

Gazeti la Süddeutsche limemnukulu Kiongozi wa wanajeshi waliotwaa madaraka Mamady Doumbouya akieleza kwamba, wamechukua hatua hiyo ili kupambana na ufisadi na usimamizi mbovu wa uchumi nchini Guinea.   

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatupeleka Afrika Kusini ambako rais wa zamani Jacob Zuma ametolewa jela kutokana na afya yake kuwa mbaya. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba Zuma hakumaliza hata miezi miwili kutumikia adhabu ya kifungo na linatilia maanani kwamba bwana Zuma hakuwamo jela bali aliwekwa hospitalini.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema hakuna taarifa kamili juu ya maradhi yanayomsibu rais huyo wa zamani. Zuma alipewa adhabu ya kifungo cha miezi 15 jela kwa kosa la kudharau amri ya mahakama. Aligoma kutoa ushahidi mbele ya tume ya uchunguzi juu ya madai yaliyohusu ufisadi ulioetendeka wakati alipokuwamo madarakani. Hata hivyo gazeti hilo linatilia maanani kwamba kukamatwa kwa Zuma kulisababisha ghasia nchini Afrika Kusini.

Wafuasi wa Zuma wapata faraja

Maalfu kwa maalfu ya watu walijitokeza kwenye majimbo mawili na kupora mali kwenye maduka, maghala na kwenye maeneo kadhaa ya biashara. Mamia ya watu kadhaa walikufa kutokana na ghasia hizo. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema wafuasi wa Zuma wamepata faraja juu ya kuachiwa kwa rais huyo wa hapo awali.

Gazeti hilo limewanukulu wapinzani wa Zuma wakisema uamuzi wa kumwachia ni njia ya kuleta mwafaka baina ya kambi yake na ile ya rais aliyemo madarakani Cyril Ramaphosa kwa sababu ghasia zilizotokea baada ya hukumu yake kutolewa zimeuchimba zaidi mgawanyiko uliomo ndani ya chama tawala cha African National Congress wakati ambapo uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika mnamo mwezi wa Oktoba. 

Neue Zürcher Zeitung

Gazeti la Neue Zürcher linazungumzia juu ya juhudi za Nigeria za kuifufua sekta ya usafiri wa njia za reli. Linasema fedha kwa ajili ya mradi huo mpaka sasa zimetoka China. Gazeti hilo linatufahamisha kwamba mradi huo ni wa kilometa 4200 za njia za reli. Ni sekta yenye historia ya miaka zaidi ya 120 na hapo awali ilikuwa inatoa ajira kwa watu wengi nchini Nigeria kuliko sekta nyingine. Hata hivyo gazeti linasema sekta hiyo ilipuuzwa na badala yake vitega uchumi viliwekwa katika ujenzi wa barabara na katika usafiri wa anga.

Gazeti la Neue Zürcher linasema serikakli ya sasa inadhamiria kuifufua sekta hiyo ya usafiri. Na kwa ajili hiyo inatumia fedha nyingi na hasa mikopo kutoka China. Dola bilioni 30 zitahitajika kwa ajili ya kuyaunganisha majimbo yote ya nchi.

Frankfurter Allgemeine

Makala nyingine ya gazeti la Frankfurter Allgemeine ni juu ya wakimbizi wa Afghanistan waliokwishawasili nchini Uganda na Rwanda. Hata hivyo gazeti hilo linasema Afrika Kusini haiko tayari kuwapokea wakimbizi hao. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaeleza kwamba wakimbizi hao wa Afghanistan kwa sasa wanatafutiwa mahala pa kufanya kuwa kituo chao cha kwanza. Linasema Uganda na Rwanda zimekubali kuwapa wakimbizi hao wa Aghanistan hifadhi ya muda.

Uganda imewachukua wakimbizi kutoka Afghanistan baada ya Marekani kutoa maombi na tayari 51  wameshawasili kati ya jumla ya watu 2000. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani kwamba Uganda tayari inatoa hifadhi kwa wakimbizi zaidi ya milioni 1.5 hasa kutoka Sudan, Kongo na Burundi. Gazeti linafahamisha kwamba wakimbizi wengine wa Afghanistan 250 wameshawasili nchini Rwanda.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen