Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Matukio ya Afrika | DW | 03.09.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ujerumani

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Afrika katika magazeti ya Ujerumani inaangazia hali katika mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mkutano juu ya Afrika wa mjini Berlin na msamaha kwa waliokuwa magaidi wa kundi la Bolo Haram nchini Nigeria.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linalozungumzia juu ya hali ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Linasema tangu mwezi wa Mei wanajeshi wa Kongo wamekuwa wanayasimamia  majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri kwa lengo la kukomesha mauaji na kuleta amani. Hata hivyo juhudi hizo zimeshindikana. Gazeti hilo linaeleza kwamba rais Felix Tshisekedi alitangaza sheria za kijeshi kutumika kwenye majimbo hayo mawili.

Mbunge Kasereka Mangwengwe amesema hali haiwezi kuendelea kuwa ya mauaji, utekaji nyara na ukatili wa kila aina. Amenukuliwa na gazeti hilo akisema ilipasa hatua zichukuliwe. Wanajeshi wanapambana na waasi wa ADF wenye asili ya Uganda. Waasi hao wameshawaua watu zaidi ya 1300  kwenye wilaya ya Beni pekee tangu mwaka 2019.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema mkutano juu ya Afrika uliofanyika mjini Berlin ni miongoni mwa mikutano hiyo maarufu ambayo imekuwa inafanyika kwa miaka mingi tangu ilipoanzishwa wakati Ujerumani ilipokuwa mwenyekiti wa kundi la nchi tajiri 20.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaeleza kwamba mkutano huo wa mjini Berlin ulikuwa wasaa wa kuweka mikakati mipya katika sera ya nje ya Ujerumani. Gazeti linatilia maanani kwamba bara la Afrika ambalo ni jirani wa Ulaya kwa muda mrefu halikutiliwa maanani kwa kiwango kinachostahili. Pamoja na migogoro ya wakimbizi na ugaidi, bara la Afrika linatoa fursa ya uwekezaji vitega uchumi.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema Ujerumani inaweza kufanya mengi kwa ajili ya maendeleo ya bara la Afrika. Gazeti hilo linasema kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliyengoza mkutano wa mjini Berlin alionyesha ari kubwa ya kujihusisha barani Afrika kuliko viongozi wenzake wa hapo awali. 

Hata hivyo gazeti linaeleza kuwa aliyofanya hayatoshi kuipiku China barani Afrika wala kuzuia wakimbizi kutoka Afrika. Na kwa ajili hiyo gazeti linashauri serikali ijayo nchini Ujerumani itilie maanani zaidi bara hilo jirani na wakati huo huo kujifunza kutokana na makosa yaliyofanywa nchini Afghanistan. Kushirikiana na Afrika, maana yake si kupeleka muundo wa kijamii wa kimagharibi kwa waafrika.  

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche linazungumzia juu ya umuhimu wa kupatikana chanjo zaidi kwenye nchi za Afrika. Gazeti hilo linafahamisha kwamba katika miezi ijayo, Ujerumani na kampuni mbalimbali za dawa zinakusudia kuongeza chanjo kwa ajili ya nchi za Afrika. Kansela wa Ujerumani anakusudia kutenga mikopo na fedha za misaada kwa ajili hiyo. Gazeti la Süddeutsche linafahamisha juu ya mipango ya kutengenezwa dawa hizo nchini Senegal, Rwanda na Afrika Kusini. Kwa mujibu wa taarifa zilizopokolewa na gazeti hilo kiwanda cha kujaza au kutengeneza chanjo za corona kitaanza kujengwa nchini Rwanda mapema mwaka ujao.

Gazeti limemnukulu rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini akisema kwamba mfumo wa kibaguzi unatumika katika ugavi wa chanjo za kupambana na maambukizi ya virusi vya corona. Gazeti linasema wakati mazungumzo yanafanyika kwenye shirika la afya dunaini WHO, Umoja wa Ulaya na Ujerumani zinaweka mkazo juu ya kutengenezwa chanjo za corona barani Afrika.

Gazeti la Süddeutsche limemnukulu waziri wa  Ujerumani wa ushirikiano wa maendeleo Gerd Müller akisema kwamba chanjo hizo zitasaidia pia katika kupambana na maradhi mengine kama Surua, Polio na Malaria.

die tageszeitung

Makala nyingine ya gazeti la die tageszeitung inahusu msamaha unaozingitwa kuwa mchungu miongoni mwa watu wa kaskazini mwa Nigeria. Waliokuwa magaidi wa kundi la Boko Haram wataruhusiwa kurudi na kuishi kwenye vijiji vyao kama zamani.

Kwa mujibu wa gazeti la die tageszeitung, maafisa wa serikali ya jimbo la Borno la kaskazini mwa Nigeria wametangaza kwamba wafuasi 3000 waliokuwamo katika kundi hilo la kigaidi watasamehewa na kuruhusiwa kurejea kwenye vijiji vyao. Hata hivyo gazeti hilo linasema changamoto ni kubwa.   

Gazeti linakumbusha kwamba kundi la Boko Haram liliundwa katika mji mkuu wa jimbo la Borno, Maiduguri mnamo mwaka 2002. Na katika kipindi cha miaka 10 cha uwepo wake watu zaidi ya 41,000 wameuliwa. Gazeti la die tageszeitung linazitilia maanani habari za kutia moyo kwamba wafuasi wengi wa kundi la kigaidi la Boko Haram wamekuwa wanajisamilisha kwa jeshi la Nigeria.

Die tageszeitung linaeleza kwamba mabadiliko hayo yametokana hasa na uhasama uliopo baina ya Boko Haram na kundi linalojiita Dola la Kiislamu kwenye eneo la Afrika magharibi, ISWAP. Gazeti linasema baada ya kuuliwa kwa kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau wafuasi wake wengi wanaona ni bora kujisalimisha. Gazeti limemnukulu gavana wa jimbo la Borno, Babagana Zulum akisema uamuzi wa kuwasamehe magaidi wa Boko Haram ni mgumu lakini hapana budi kuchagua kati ya kuendelea damu kumwagika au kujifunza kuwakubali watu hao!

Vyanzo: Deutsche Zeitungen