1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
6 Agosti 2021

Njaa inatumiwa kama silaha kwenye jimbo la Tigray nchini Ethiopia na athari za mabadiliko ya tabia nchi zinachangia kuchochea ugaidi nchini Mali ni baadhi ya yalionadikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika.

https://p.dw.com/p/3ydKP
Sudan Äthiopien Flüchtlinge
Picha: Nariman El-Mofty/AP/picture alliance

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche linalosema njaa inatumiwa kama silaha kwenye jimbo la Tigray nchini Ethiopia. Gazeti hilo linasema waziri mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed alieingia madarakani na sifa ya kuwa mkombozi sasa amegeuka mmwagaji damu. Gazeti hilo linakumbusha kuwa waziri mkuu Abiy Ahmed alihubiri upendo na amani alipoingia madarakani na maalfu ya wananchi wake walimshangilia. Abiy alizungumzia juu ya kuijenga Ethiopia mpya lakini mambo yamebadilika. Badala ya kuionyesha Ethiopia mpya kwenye uwanja wa Meskel, Abiy aliwaonyesha vijana 3000 walioandikishwa ili kwenda vitani kwenye jimbo la Tigray. Gazeti la Süddeutsche linasema lengo la waziri mkuu huyo ni kuwamaliza wapinzani wake kwenye jimbo hilo.

Gazeti hilo linaeleza kwamba njia mojawapo kwa waziri mkuu Abiy ya kulifikia lengo hilo ni kuzuia misaada ya chakula kuingia Tigray. Gazeti limewanukulu maafisa wa Umoja wa Mataifa wakisema kwamba pana hatari kubwa ya kutokea njaa kwenye jimbo hilo. Watoto zaidi ya laki moja watakuwamo katika hali mbaya sana ikiwa misaada haitafikishwa haraka kwenye jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia.

Der Tagesspiegel

Gazeti la Der Tagesspiegel linasema athari za mabadiliko ya tabia nchi zinachangia katika kuchochea ugaidi nchini Mali. Hata hivyo gazeti linasema suala hilo halitiliwi maanani na jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa nchini humo la askari 13,000 miongoni mwao 900 kutoka Ujerumani.

Gazeti hilo linazungumzia juu ya tathmini iliyofanywa hivi karibuni kwa niaba ya Umoja wa Ulaya inayobainisha kwamba athari za mabadiliko ya tabia nchi zinahatarisha usalama kwenye eneo la Sahel na kwenye upembe wa Afrika. Gazeti la Der Tagesspiegel linasema inapasa kuzifahamu athari hizo zinazosababisha ukame, uhaba wa maji na ardhi ya kilimo ambazo kwa pamoja zinachangia katika kuchochea migogoro ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Linasema hasa kwenye eneo la Sahel ugeugeu wa hali ya hewa unajenga mazingira ya kusambaa kwa jangwa. Hali hiyo inayosababisha uhaba wa ardhi inachochea mivutano kati ya wakulima na wafugaji. Gazeti hilo linasema migogoro hiyo aghlabu hutatuliwa kwa njia ya mabavu kwa sababu ya kupatikana kwa wingi silaha ngodo ndogo na ndipo magaidi na watu wenye itikadi kali za kidini wanapata mianya ya kjiingiza.

Gazeti la Der Tagesspiegel linaeleza kuwa pamoja na juhudi za kulinda amani zinazofanywa na Umoja wa Mataifa nchini Mali, athari za mabadiliko ya tabia nchi zinapaswa kutiliwa maanani.

Neue Zürcher Zeitung

Gazeti la Neue Zürcher linazungumzia juu ya mvutano kati ya mfalme wa Eswatini na wananchi wake wanaopinga vikali tabia yake ya ubadhirifu na utawala wake wa kudhibiti mamlaka yote ya uongozi. Gazeti hilo linasema kwa muda wa miezi kadhaa sasa watu nchini Eswatini wamekuwa wanafanya maandamano dhidi ya mfalme Mswati wa 3 ambaye ameshatawala kwa muda wa miaka 35. Gazeti linasema watu wake wanataka demokrasia ikiwa pamoja na haki ya kumchagua waziri mkuu.Linakumbusha kwamba chanzo cha mvutano huo ni kuuliwa kwa mwanafunzi wa taaluma ya sheria aliyekuwa na umri wa miaka 25.

Gazeti la Neue Zürcher limefahamisha kuwa familia yake inatuhumu kwamba aliuliwa na polisi. Gazeti hilo liansema watu wamefanya maandamano kwenye miji mbalimbali kuonyesha hali ya kutoridhika juu ya kuongezeka kwa umasikini na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wengi. Linasema wakati umasikini unaongezeka mfalme alitumia kiasi cha dola milioni 24 kununua magari aina ya Rolls- Royce kwa ajili yake na wakeze. Watu pia wanadai haki ya kumchagua waziri mkuu. Mfalme Mswati wa 3 anadhibiti mihili yote mitatu ya utendaji, mahakama na bunge.

Handelsblatt

Gazeti la Handelsblatt linazingatia ujumbe uliotolewa na waziri wa Ujerumani wa ushirikiano wa maendeleo bwana Gerd Müller. Waziri Müller ametoa wito wa kutokomeza njaa duniani. Katika wito huo waziri Müller  anazitaka nchi tajiri zitenge kiasi cha dola bilioni 40 kwa mwaka kwa ajili ya kufanikisha juhudi za kujenga dunia ambapo binadamu wote watakuwa na chakula cha kutosha hadi kufikia mwaka 2030. Gazeti la Handelsblatt limemnukulu waziri huyo wa Ujerumani akisema kuwa nchi tajiri zina nyenzo zote za kuweza kufanikisha lengo la kuondoa njaa duniani. Gazeti hilo linasema waziri Müller ametilia maanani kwamba juhudi za kuondoa njaa pia zitachangia katika kuleta amani duniani.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen