1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
23 Julai 2021

Yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika ni pamoja na kuanzia mwaka ujao Afrika Kusini itaanza kutengeneza dozi za chanjo za corona na Umoja wa Ulaya waamua kupeleka majeshi Msumbiji.

https://p.dw.com/p/3xuhg
Corona Impfstoff Moderna Biontech Pfizer
Picha: STRF/STAR MAX/IPx/picture alliance

Frankfurter Allgemeine Zeitung 

Habari za kutia moyo zilizoandikwa kwenye gazeti la Frankfurter Allgemeine zinahusu juhudi za kupambana na maradhi ya corona barani Afrika. Gazeti hilo linatufahamisha kwamba kuanzia mwaka ujao Afrika Kusini itaanza kutengeneza dozi za chanjo za corona zaidi ya milioni mia moja kwa mwaka. Gazeti linasema kampuni za BioNTech na mshirika wake Pfizer zimefikia mapatano na Afrika Kusini juu ya mradi huo. Gazeti hilo linafahamisha kwamba nchi nyingine za Afrika pia zitanufaika na mradi huo. Frankfurter Allgemeine limemnukulu mkurugenzi mkuu wa kampuni ya BioNTech Ugur Sahin akisema kwamba lengo la  mradi huo ni kuhakikisha kwamba watu kwenye mabara yote wanapatiwa chanjo.

Neue Zürcher Zeitung

Gazeti la Neue Zürcher wiki hii limechapisha makala juu ya taarifa zinazohusu mambukizi ya corona zinazotolewa na Ethiopia. Linasema kwa mujibu wa taarifa hizo mtu anaweza kuamini kwamba Ethiopia ipo mwazoni mwa janga la corona. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba idadi ya watu waliokufa kutokana na maradhi ya corona mpaka sasa nchini Ethiopia ni nusu ya ile ya watu waliokufa nchini Uswisi licha ya Ethiopia  kuwa na watu zaidi ya milioni 110.

Gazeti la Neue Zürcher linasema takwimu rasmi zinaonyesha ulinganifu wa wastani wa bara zima la Afrika. Linasema mpaka sasa watu milioni sita wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya corona barani Afrika na kati ya hao waliokufa ni laki moja na nusu takriban sawa na idadi ya watu waliokufa nchini Uingereza. Gazeti la Neue Zürcher linakumbusha kwamba bara la Afrika lina watu bilioni 1.3. Hata hivyo gazeti hilo linatilia mashaka takwimu zinazotolewa na serikali za Afrika. Linasema takwimu zinazotolewa barani Afrika ni zile zinazokaribia tu idadi ya kweli. Linasema kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa ni asilimia 40 iliyoorodeshwa ya watu waliokufa kutokana na maambukizi ya virusi vya corona barani Afrika. 

Neues Deutschland

Umoja wa Ulaya waamua kupeleka majeshi Msumbiji. Gazeti la Neues Deutschland linasema katika makala  yake kwamba eneo la kaskazini mwa Msumbiji linaelekea kwenye mgogoro wa kimataifa. Gazeti hilo linasema Umoja wa Ulaya unacheza na karata ya kijeshi kutokana na maslahi ya kiuchumi ya Ufaransa kwenye eneo  hilo. Kampuni kubwa ya Ufaransa Total inaendesha shughuli zake kwenye eneo hilo. Gazeti la Neues Deutschland linasema muda mfupi majeshi kutoka nchi za Umoja wa Ulaya yatangia kaskazini mwa Msumbiji. Gazeti hilo linatufahamisha kwamba tarahe 16 ya mwezi huu baraza la Umoja wa Ulaya lilipitisha uamuzi wa kupeleka wanajeshi nchini Msumbuji na linafahamisha kwamba Ureno tayari imeshapeleka askari 140 nchini humo na Marekani imeshapeleka wakufunzi wa kijeshi.

Lengo la Operesheni

Neues Deutschland linaeleza kuwa lengo la operesheni hiyo ni kupambana na magaidi wa kundi la itikadi kali la Ansar Al-Sunna lenye uhusiano na magaidi wanaojiita dola la kiislamu, IS. Gazeti hilo linafahamisha kwamba Rwanda na jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC pia zimeshapeleka majeshi nchini Msumbiji. Hata hivyo gazeti hilo linatilia maanani tahadhari iliyotolewa na mashirika yasiyo ya kiserikali. Asasi hizo zimeeleza katika barua kwamba hatua za kijeshi pekee hazitafanikisha shabaha inayolengwa.

Gazeti hilo linasema katika barua yao, asasi hizo zimekumbusha juu ya migogoro kama hiyo iliyotokea kwingineko barani Afrika ambako suluhisho la kijeshi lilishindikana. Yametoa mifano ya migogoro ya eneo la Sahel, Somalia na Niger. Juu ya uhusika wa majeshi kutoka nje, gazeti la Neues Deutschland linaeleza kuwa lengo nikulinda maslahi ya kiuchumi na siyo kushirikiana na Msumbiji.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung limeandika juu ya mkasa uliotokea kwenye msikiti nchini Mali ambako rais wa nchi hiyo Assimi Goita aliponea chupu chupu baada ya watu wawili kujaribu kumshambulia. Gazeti linaeleza kuwa mmoja wao alikuwa na kisu. Hata hivyo wanajeshi walifanikiwa kuwazuia watu hao. die tageszeitung linaeleza kuwa washambuliaji hao walijaribu kujitosa mbele kutokea safu za nyuma baada ya sala kumalizika ili kumuua rais Goita ndani ya msikiti huo wa mjini Bamako. Gazeti linasema walinzi waliwahi kumwondoa rais huyo na kumpeleka mahali salama. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba makundi ya magaidi yanaendesha harakati zao kwa nguvu nchini Mali lakini pia linakumbusha kuwa rais Assimi Goita ameingia madarakani kwa njia ya mabavu!

Vyanzo: Deutsche Zeitungen