1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Rashid Chilumba
9 Julai 2021

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya Afrika kuhusu mgogoro wa jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia na juu ya adhabu aliyopewa Jacob Zuma, yanasema inaashiria mwisho wa mustakabali wake wa kisiasa na mengineyo.

https://p.dw.com/p/3wGfX
Äthiopien Soldaten in Mekelle
Picha: Minasse Wondimu Hailu/AA/picture alliance

Der Tagesspiegel

Na tunaanza na makala ya gazeti la Der Tagesspiegel juu ya mgogoro wa jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia. Gazeti hilo linasema mgogoro wa jimbo hilo unahatarisha umoja wa shirikisho la Ethiopia. Linasema pana uwezekano wa jimbo hilo kujitenga na shirikisho.

Gazeti la Der Tagesspiegel linasema uongozi wa waziri mkuu Abiy Ahmed ambaye ni mshindi wa nishani ya amani ya Nobel sasa umeanza kutetereka. Linaeleza kwamba matatizo yake yalianza baada ya kujaribu kuwaondoa kwa nguvu viongozi wa jimbo la Tigray wanaotofautiana na uongozi wa serikali yake kuu ya mjini Addis Ababa.

Gazeti la Der Tagesspiegel linasema waziri mkuu Abiy Ahmed yumo hatarini kukabiliwa na mgogoro mkubwa wa kikabila. Hata hivyo gazeti hilo linatilia maanani kwamba waziri mkuu huyo amesema yuko tayari kwa mdahalo wa kitaifa, lakini Der Tagesspiegel linasema Abiy Ahmed alipaswa kuanzisha mdahalo mara tu baada ya kuingia madarakani miaka mitatu iliyopita. Linasema hali katika jimbo la Tigray itaendelea kuyumbayumba kiasi cha kutoweza kutabirika.

Frankfurter Allgemeine Zeitung

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linamzungumzia Jacob Zuma rais wa zamani wa Afrika Kusini aliyehukumiwa adhabu ya kifungo kwa kosa la kudharau mahakama. Gazeti hilo linasema adhabu hiyo ni hatua ya kuelekea kwenye mwisho wa mustakabal wake wa kisiasa. Gazeti linasema ni hatua ya lazima lakini haitoshi, linasema kinachohitajika ni hatua thabiti za kuondoa mfumo wa kupendeleana na kukuza uchumi kwa manufaa ya umma. 

Frankfurter Allgemeine linatilia maaani kwamba  wakati wa utawala wake mali za umma ziliporwa mtindo  mmoja nchini Afrika Kusini na ndiyo sababu rais huyo wa zamani anatumia njia zote za kisheria kuzuia  mashtaka juu ya ufisadi mkubwa uliofanyika wakati wa utawala wake.

Neues Deutschland

Nalo gazeti la Neues Duetschland linatufahamisha kwamba Rwanda imejitosa katika vita vya nchini Msumbiji ambapo nchi hiyo inakabiliana na magaidi wanaofuata itikadi kali. Gazeti linasema kwa muda wa miaka kadhaa magaidi hao wamekuwa wanafanya  mashambulio nchini Msumbiji.

Gazeti hilo linafahamisha kwamba askari 200 wa Rwanda tayari wako kwenye jimbo la Msumbiji la Cabo Delgado. Mwishoni mwa mwezi wa April marais wa Msumbiji Filipe Nyusi na wa Rwanda Paul Kagame walikutana kuzungumzia juu ya mipango ya Rwanda ya kupeleka wanajeshi nchini Msumbiji kwa ajili ya kupambana na magaidi. Mapigano yamepamba moto katika miezi ya hivi karibuni katika jimbo la Cabo Delgado tangu magaidi hao waanze kuliyumbisha jimbo hilo mnamo mwaka 2017.

Gazeti la Neues Deutschland linasema kutokana na mshambulio kuongezeka mradi wa gesi wa kampuni ya Ufaransa,Total wa thamani ya dola bilioni 20 umesimamishwa. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba pia nchi za  jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika pia zinatafakari kuiunga mkono Msumbiji kijeshi. Hata hivyo linasema Tanzania inapinga kushiriki katika juhudi hizo za kijeshi. Waziri wake wa mambo ya nje amesema  haijulikani kwa uhakika ni nani anayepigwa vita! Gazeti la Neues Deutschland linasema askari wapatao 3000 watahitajika kwa ajili ya juhudi za kupambana na magaidi nchini Msumbiji lakini linauliza fedha za kugharimia harakati hizo zitatoka wapi?

Berliner Zeitung,

Gazeti la Berliner Zeitung linakamilisha makala yetu wiki hii kwa kutukumbusha juu ya hatari ya maradhi yanayopuuzwa duniani kama kichocho.Gazeti hilo linasema maradhi hayo yamejitokeza tena  kwa nguvu kwenye maeneo yanayopakana na ziwa Victoria na limeandika juu ya juhudi zinazofanywa na madaktari wa Tanzania na Ujerumani katika kupambana na maradhi hayo.

Gazeti la Berliner linasema Daktari Humphrey Mazigo kutoka Mwanza,Tanzania na mwenzake Andreas Müller kutoka Ujerumani wanaonyesha jinsi inavyowezekana kupambana na maradhi mabaya yaliyosahaulika kama hayo licha ya uhaba wa nyenzo. Ugonjwa wa kichocho unatokana na maambukizi ya vimelea vya minyoo katika maji baridi, hasa kwenye maziwa na mito.

Gazeti linasema watu wengi miongoni mwa milioni 40 kwenye maeneo ya ziwa Victoria wameambukizwa ugonjwa huo wa kichocho yaani Bilharzia. Gazeti linatahadharisha kwamba bila ya kutibiwa, ugonjwa wa kichocho unaweza kusababisha kifo. Limewanukulu madaktari hao wawili wa Tanzania na Ujerumani wakisema kwamba wanafanya juhudi ili kuutokomeza, wamesema ugonjwa huo hujitokeza kwa mtu kuvimba tumbo na kutoa damu katika haja ndogo.

Gazeti la Berliner linakumbusha kwamba kwa sasa watu zaidi ya milioni 200 duniani kote wameambukizwa vijidudu vya kichocho. Licha ya idadi hiyo kubwa gazeti linakumbusha kwamba kichocho ni miongoni mwa  maradhi yanayopuuzwa. Linasema harakati za kupambana na kichocho zinatatizika kwa sababu hata katika nchi tajiri wengi hawajasikia juu ya magonjwa yaliyosahaulika.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen