1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri:  Grace Patricia Kabogo  
22 Januari 2021

Katika muhtasari wa masuala na matukio ya barani Afrika yaliyozingatiwa na magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na hali ya nchini Uganda baada ya uchaguzi. Hali katika jimbo Tgray nchini Ethiopia na mengineyo.

https://p.dw.com/p/3oHag
Tansania Chato 2020 | Yoweri Museveni, Präsident Uganda
Picha: Tanzania State House/Xinhua News Agency/picture alliance

die tageszeitung

Na tunaanza moja kwa moja na makala ya gazeti la die tageszeitung juu ya hali ya nchini Uganda baada ya kufanyika uchaguzi mkuu. Gazeti hilo linasema Uganda imekuwa kama imelemaa baada ya Yoweri Museveni kutangazwa mshindi wa uchaguzi huo. Wapinzani wanapinga matokeo hayo lakini hakuna wanaloweza kufanya. Kiongozi wao Bobi Wine amezingirwa na polisi na wafuasi wake wanawindwa. Gazeti linasema tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mji wa Kampala umekuwa kimya ambao vinginevyo huwa ni mji uliochangamka.

Gazeti la die tageszeitung linasema haikuwezekana kwa wafuasi wa Bobi Wine kulinda kura zao kutokana na mtandao wa internet kufungwa siku moja kabla ya uchaguzi kufanyika. Baada ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo vijana ambao ni wafuasi wa Bobi Wine hawakuweza kutumia mitandao ya kijamii ili kujiandaa kwa ajili ya kupinga matokeo. Gazeti linasema walioonekana mitaani walikuwa wapanda pikipiki waliovaa mashati ya manjano ambao ni wafuasi wa rais Yoweri Museveni. Bobi Wine amefungiwa nyumbani mwake na hata balozi wa Marekani hakuruhusiwa kumwona. Gazeti linasema hakuna anayejua kitakachofuata bali kila mtu anatumai kwamba amani itarejea nchini Uganda.

Neue Zürcher Zeitung

Gazeti la Neue Zürcher linazungumzia juu ya hali ya jimbo la kaskazini ya Ethiopia la Tigray. Linasema jimbo hilo limo katika hatari ya kukumbwa na njaa. Gazeti linasema wakati mgogoro unaendelea kazi za mashirika  ya misaada zinasuasua. Kwa muda mrefu hali ya maalfu ya wakimbizi wa jimbo hilo haikujulikana. Gazeti  la Neue Zürcher linasema ni mpaka ilipofika mwanzoni mwa mwezi huu ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la misaada kwa wakimbizi UNHCR lilipoweza kuingia kwenye kambi za Mai Aini na Adi Harush. Wakimbizi  zaidi ya 25, 000 wamo kwenye kambi hizo. Gazeti la Neue Zürcher limemnukuu mwakilishi wa shirika hilo la  wakimbizi akieleza kwamba msaada wa chakula uliopelekwa kwa wakimbizi hao mnamo mwezi wa Desemba mwaka uliopita sasa umekwisha. Watu hao wanahitaji msaada mwingine wa haraka na pia pana hatari ya kulipuka magonjwa. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa watu wapatao milioni 4.5 wanahitaji msaada wa haraka kwenye jimbo la Tigray.

Süddeutsche Zeitung

Nalo gazeti la Süddeutsche linasema wimbi la maandamano linaloendelea kusambaa nchini Tunisia linakumbusha vuguvugu la mapinduzi la mwaka 2011. Gazeti linasema wimbi hilo la maandamano linaendelea licha ya hatua zilizochukuliwa na serikali ili kudhibiti maambukizi ya  virusi vya corona. Gazeti la Süddeutsche linasema taarifa na picha juu ya hali ya sasa nchini Tunisia zinakumbusha matukio ya mwaka 2011 ambapo dikteta wa nchi hiyo Ben Ali alitimuliwa.

Süddeutsche linaeleza kuwa mtaa maarufu katika mji mkuu, unaoitwa Habib Bourgiba ulifurika waandamanaji mapema wiki hii waliotoa mwito wa kung'olewa kwa utawala wa sasa ambao kwa mtazamo wao umesababisha hali mbaya ya maisha. Gazeti linasema polisi waliyajibu maandamano kwa kutumia gesi ya kutoa machozi kama jinsi ilivyokuwa katika miaka iliyopita.

Maandamano

Gazeti la Süddeutsche linasema maandamano hayo yanaonyesha hali ya kutoridhika miongoni mwa  wananchi wa Tunisia. Linaeleza kuwa maandamano hayo yalianza wiki iliyopita wakati wa kuadhimisha miaka10 tangu dikteta Ben Ali alipoikimbia Tunisia. Linasema hakuna kilichobadilika nchini humo tangu wakati huo. Hali ya maisha imezidi kuwa mbaya na ukosefu wa ajira umeongezeka hadi kufikia asilimia 30. Na wakati ambapo watu wamezidi kutumbukia katika umasikini serikali imeondoa ruzuku, ili kutimiza masharti ya wakopeshaji wa kimataifa.

Gazeti la Süddeutsche linasema waziri mkuu Hichem Mechichi aliwaambia wananchi kwamba malalamiko yao yatasikilizwa na gazeti linatilia maanani kuwa maneno kama hayo aliyasema pia dikteta Ben Ali, hata hivyo wananchi wanao msemo mwingine "Mfumo wote wa utawala unapaswa kubanduliwa".

die tageszeitung,

Na tunakamilisha kwa makala nyingine ya gazeti la die tageszeitung juu ya mwizi mkubwa wa kura nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Ngoy Mulunda aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi wakati wa  utawala wa Joseph Kabila. Gazeti hilo linasema Ngoy Mulunda sasa amehukumiwa adhabu ya kifungo jela. Katika uchaguzi wa mwishoni mwa mwaka 2011 Joseph Kabila aliibuka mshindi kwa kupata asilimia 48.95 ya kura. Die tageszeitung linasema ushindi huo haukutokana na kura za wafuasi wake bali kazi yote ilifanywa na mwenyekiti wake wa tume ya uchaguzi Daniel Ngoy Mulunda.

Maalfu ya kura za kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi zilipotezwa, die tageszeitung linafahamisha kwamba Mulunda alikamatwa mapema wiki hii kwa kosa la kutoa hotuba ya kuchochea chuki na kuhujumu mamlaka ya nchi kwa kutishia kulitenga jimbo la Katanga. Gazeti la die tageszetung linasema mkasa wa Ngoy Mulunda unaashiria mwanzo wa mchakato wa kisheria wa kuihukumu enzi ya Kabila katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen