1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
15 Januari 2021

Katika masuala na matukio ya barani Afrika yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani ni pamoja na mustakabali wa Uganda baada ya kufanyika uchaguzi.na juu ya mgogoro wa jimbo la Tigray nchini Ethiopia.

https://p.dw.com/p/3nxWO
Bildkombo | Yoweri Museveni und Bobi Wine

Neue Zürcher Zeitung

Na tunaanza na makala ya gazeti la Neue Zürcher juu ya mustakabali wa kisiasa nchini Uganda. Gazeti hilo linasema idadi kubwa ya watu wa nchi hiyo wanamjua kiongozi mmoja tu katika maisha yao ya hadi sasa rais Yoweri Museveni ambaye amekuwamo madarakani tangu mwaka 1986. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba Museveni amesimama tena kuwania muhula mwingine madarakani. Hata hivyo gazeti la Neue Zürcher linasema safari hii alikabaliwa na upinzani mkali wa mwanamuziki maarufu Bobi Wine anayewakilisha rika la vijana nchini Uganda.

Gazeti hilo linaeleza kwamba Museveni aliingia madarakani kwa kuashiria matumaini makubwa miongoni mwa watu wa Uganda na hasa baada ya tawala za Iddi Amin na Milton Obote. Neue Zürcher linakumbusha kwamba Museveni aliahidi kurejesha demokrasia na kuheshimu haki za binadamu mara tu baada ya kuingia madarakani. Hata hivyo gazeti linatilia maanani kwamba Museveni alibadilika baada ya muda mfupi. badala ya demokrasia, wapinzani, ikiwa pamoja na Bobi Wine wanatiwa ndani mara kwa mara na amebadilisha katiba kwa manufaa yake mara kadhaa. Gazeti hilo linautilia mashaka uchaguzi uliofanyika Alhamisi.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linazungumzia juu ya mgogoro wa jimbo la Ethiopia la Tigray. Gazet hilo linasema hali bado haijatengemaa katika jimbo hilo tangu majeshi ya serikali kuu yalipoingia kwa lengo kurejesha mamlaka na umoja wa Ethiopia. Linasema kuna taarifa juu ya kukamatwa na kuuliwa kwa watu waliokuwa viongozi wa jimbo hilo. Die tageszeitung limekariri taarifa juu ya kuuliwa kwa viongozi wanne na kukamatwa kwa wengine 9 wa serikali ya TPLF ya jimbo la Tigray.

Gazeti hilo linakumbusha kwamba wiki sita zilizopita serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed ilitangaza ushindi dhidi ya waasi wa Tigray. Hata hivyo limenukuu taarifa za mashirika ya kimataifa juu ya kuendelea kwa mapigano hasa karibu na maeneo ya mji mkuu wa jimbo hilo, Mekelle. Katika kadhia nyingine gazeti la die tageszeitung limezungumzia juu ya uwepo wa majeshi ya nchi jirani ya Eritrea katika jimbo la Tigray taarifa ambazo zimethibitishwa na baadhi ya maafisa wa serikali kuu ya Ethiopia. Gazeti hilo linasema swala jingine linalosababisha wasiwasi ni mvutano kati ya Ethiopia na Sudan baada ya kutokea mgogoro wa jimbo la Tigray.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia jinsi nchi za Afrika Kaskazini zitakavyokuwa muhimu kwa Ujerumani na nchi za Umoja wa Ulaya baada ya kuondoka kwa janga la corona. Gazeti hilo linasema kwa sasa mtu anapozungumzia juu ya nchi za kaskazini mwa Afrika, masuala yanayozingatiwa ni ugaidi na uhamiaji tu lakini gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema nchi hizo zina mengi ya kunadi kwenye soko la dunia. Nchi hizo, ikiwa pamoja na Morocco, Algeria na Tunisia zina misingi mizuri ya maendeleo ya kidijitali ambayo ni muhimu kwa mageuzi ya ikolojia kwa ajili ya nchi za Ulaya.

Frankfurter Allgemeine linatilia maanani kwamba nchi za Afrika Kaskazini zipo umbali wa pua na mdomo na bara la Ulaya. Inachukua muda wa saa mbili na nusu kutoka Frankfurt, hadi Tunis au Algiers. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linauliza jee nani barani Ulaya anajua kwamba wahandisi wa software wenye sifa za kutajika wanahitimu masomo nchini Tunisia? Nchi za Afrika Kaskazini pia zimeonyesha kuwa muhimu katika mfumo wa ugavi wa nyenzo zinazohitajika katika sekta za utengenezaji wa magari na ndege.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazitaka nchi za Ulaya na hasa Ujerumani zifungue macho juu ya nchi za Afrika Kaskazini. Linasema tayari makampuni ya China na Uturuki yameshaingia katika eneo hilo la Afrika na kuwekeza vitega uchumi.  

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche linatupasha habari juu ya mfanyabiashara maarufu wa Israel mwenye mahusiano ya mashaka mashaka barani Afrika. Muisraeli huyo Beny Steinmetz ambaye sasa anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi nchini Uswisi juu ya rushwa kuhusiana na mgodi wa madini wa nchini Guinea anafanya biashara ya madini na malighafi. Gazeti la Süddeutsche linasema ili kuweza kupata ufahamu zaidi juu ya shughuli zake inapasa kutuama kidogo barani Afrika yaani nchini Guinea. Guinea ni nchi yenye utajiri wa madini na mgodi wake maarufu wa malighafi ya kuzalishia chuma upo kwenye mji wa Simandou.

Kampuni ya hapo iliyokuwa inachimba kwenye mgodi huo ilipokonywa leseni na badala yake kampuni ya bwana Beny Steinmetz ilipewa leseni hiyo bila ya kuilipa serikali ya Guinea kiasi cha fedha kilichostahili. Kwa nini serikali ya Guinea ilikubali biashara hiyo? Gazeti linasema waendesha mashtaka wanatuhumu ufisadi ulitendeka. Kulingana na tuhuma hizo, bwana Steinmetz alitoa hongo dola zaidi ya miloni 10. Gazeti la Süddeutsche linatilia maanani kwamba Guinea ni miongoni mwa nchi masikini sana duniani.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen