1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
8 Machi 2019

Gazeti la die tageszeitung limeandika juu ya mpango wa dharura uliotangazwa na rais mpya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi anaokusudia kuutekeleza katika siku mia moja za  kwanza za muhula wake.

https://p.dw.com/p/3Egf7
DR Kongo  Kinshasa Vereidigung Präsident Felix Tshisekedi
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

die tageszeitung

Licha ya kutotoa maelezo ya kina juu ya mpango huo, kauli aliyotoa rais Tshisekedi ni ya  kutia moyo. Ameahidi kuwasamehe wafungwa wa kisiasa katika muda wa siku kumi na kuwawezesha wapinzani waliokimbilia nje warejee nyumbani. Rais Tshisekedi pia ameahidi kutenga asilimia kumi ya bajeti ya serikali yaani kiasi cha dola milioni 488 kwa ajili ya ujenzi mpya wa nchi na hasa miundombinu ya usafirishaji. Rais huyo ameahidi kujenga kilometa 5000 za  barabara kwenye kipindi cha miaka mitano.

Hata hivyo gazeti la die tageszeitung linatilia maanani kwamba watu watakaoshiriki katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa bwana Tshisekedi ni mawaziri na magavana wa utawala wa rais wa hapo awali, Joseph Kabila. Gazeti hilo linasema uwepo wa watu hao katika utawala wa Tshisekedi unatibua operesheni ya kuurembesha wajihi wake!

Frankfurter Allgemeine

Gazeti hilo limeandika madai ya ufisadi juu ya rais Joao Lourenco na linatufahamishaa kwamba hadi hivi karibuni, Rais Joao Lourenco alizingatiwa kuwa kiongozi aliyetegemewa kuleta matumaini makubwa barani Afrika. Mara tu baada ya kuingia madarakani alichukua hatua thabiti ili kupambana na ufisadi. Aliwaondoa mafisadi waliokuwa wananufaika na utawala wa hapo awali, ikiwa pamoja na binti yake Rais wa zamani, Dos Santos.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linakumbusha kwamba hata Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, alimsifu rais Joao Lourenco kwa kusema kuwa upepo mchanga unavuma nchini Angola! Alisema hayo wakati rais huyo alipofanya ziara nchini Ujerumani. Lakini gazeti hilo linasema utando wa kashfa ya rushwa nchini Msumbiji umemfikia rais huyo wa Angola. Na linaeleza zaidi kwa kusema ikiwa mtu ataamini madai yanayotolewa na kampuni ya Uingereza, EXXAfrica inayoshughulikia  tathmini na utabiri wa biashara, rais wa Angola Joao Lourenco anahusika na kashfa ya ufisadi, inayoanzia nchini Msumbiji.

Mashirika manne ya nchi hiyo yalichukua mkopo wa dola bilioni 2 kutoka benki ya Credit Suisse na benki ya Urusi kwa ajili ya meli za uvuvi na kituo cha rada kwenye pwani ya Msumbiji. Lakini robo ya fedha hizo hazikufika kulikokusudiwa. Kulingana na uchunguzi mikataba ya udanganyifu ilifikiwa nchini Angola wakati Joao Lourenco alipokuwa waziri wa ulinzi. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linauliza iwapo ilikuwa mapema mno kummwagia sifa rais huyo wa Angola?

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche kwenye makala yake linauliza ni kweli Ujerumani inawasaidia wahamiaji kurudi makwao na kujenga maisha ya uhakika. Serikali ya Ujerumani imejenga vituo, katika nchi kadhaa ikiwa pamoja na Ghana, kwa ajili ya kuwasaidia wahamiaji wanaorejeshwa makwao. Lengo la mradi wa serikali ya Ujerumani ni kuwawezesha watu hao kuyajenga upya maisha yao katika nchi zao. Miongoni mwa watu waliopaswa kunufaika na mradi huo ni mama mmoja kutoka Ghana Juliana Ashong na gazeti la Süddeutsche linatueleza iwapo alinufaika.

Mama huyo aliwaacha watoto wake wanne nyumbani Ghana ili kujaribu kuhamia Ujerumani. Lengo lake lilikuwa kufanya kazi yoyote ili kuweza kuwalea watoto wake, baada ya mumewe kufariki dunia. Lakini kazi aliyotafutiwa mama huyo na watu waliomleta Ujerumani kinyemela, ilikuwa chini ya hadhi ya binadamu. Na ndipo alipoamua kuwatoroka watu hao na kuripoti kwenye idara za serikali. Idara husika ilimpa makaazi lakini siyo kazi.

Kipi kilitokea?

Gazeti la Süddeutsche linatufahamisha  kwamba, baada ya miaka sita, Juliana Ashong alirejea nchini Ghana, mwaka jana, chini ya mpango wa serikali ya Ujerumani wa kuwasaidia wahamiaji wanaorudi  nyumbani lakini alichopewa mama huyo ni anuani tu ya ofisi moja ya Ujerumani iliyopo mjini Accra. Gazeti la Süddeutsche linatufahamisha zaidi kwamba ofisi hiyo katika mji mkuu wa Ghana, Accra ni kituo kinachoendeshwa na serikali ya Ujerumani kwa ajili ya kuwatafutia ajira wale waliorudishwa kutoka Ujerumani.

Msaada aliopewa mama huyo Juliana Ashong ulikuwa vifaa vya kufungulia mkahawa, sufuria na jiko la gesi. Miezi kadhaa baadae bango kubwa lilibandikwa kwenye ofisi hiyo kuonyesha mafanikio ya mama huyo. Lakini gazeti hilo linatufahamisha kwamba mpaka leo hajaanza kuuza chochote kwa sababu hajapata wateja. Jee Ujerumani kweli inawasaidia watu hao? linauliza gazeti la Südeutsche. 

Vyanzo: Deutsche Zeitungen