Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 20.03.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya umuhimu wa nyumba ya makumbusho ya Bardo iliyoshambuliwa katika mji wa Tunis. Magazeti hayo pia yameandika juu ya mafanikio katika kupambana na magaidi wa Boko Haram

Mashambulio ya kigaidi kwenye Makumbusho ya taifa mjini Tunis

Mashambulio ya kigaidi kwenye Makumbusho ya taifa mjini Tunis

Gazeti la "Süddeutsche" limeandika juu ya mashambulio yaliyofanywa na magaidi kwenye nyumba ya makumbusho katika mji mkuu wa Tunisia, Tunis. Gazeti hilo linatufahamisha juu ya umuhimu wa nyumba hiyo ya Makumbusho inayoitwa Bardo . Makumbusho hayo yanaonesha historia ya Warumi waliokuwa tajiri wakubwa katika karne za 2 na nne, wakati ambapo Yesu Kristo alikuwa bado hajazaliwa.

Gazeti la "Süddeutsche" linafahamisha zaidi kwamba Makumbusho ya Bardo ya mjini Tunis yanakumbusha enzi za Punik,wakati wa vita vya mara kwa mara kati ya Roma na Kathargo yaani Tunisia ya zamani.Gazeti la "Südeutsche" linaiita nyumba ya makumbusho ya Bardo ,hazina ya Afrika.

Magaidi wa Boko Haram wabanwa

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limearifu juu ya mafanikio ya jeshi la Nigeria katika juhudi za jeshi hilo za kupambana na magaidi wa Boko Haram.

Gazeti hilo limezikariri habari zilizotolewa na jeshi la Nigeria, zinazosema kwamba mji wa Goniri ambao hapo awali ulitekwa na magaidi wa Boko Haram,sasa umerudishwa katika mikono ya serikali. Kwa mujibu wa taarifa hiyo,wanajeshi wa Nigeria waliukomboa mji huo ulioko katika jimbo la Yobe Jumatatu iliyopita.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limemnukulu msemaji wa jeshi la Nigeria akieleza kwamba majeshi ya serikali pia yameukomboa mji wa Bama katika jimbo la Borno ambao ni wa pili kwa ukubwa katika jimbo hilo.

Gazeti la "Neues Deutschland" linasema katika makala yake kwamba mafanikio ya majeshi ya Nigeria katika mapambano na magaidi wa Boko Haram yanamwongezea Rais Goodluck Jonathan uwezekano wa kushinda katika uchaguzi wa wiki ijayo. Gazeti hilo linaeleza kuwa Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan sasa anaweza kuyaonyesha mafanikio katika juhudi za kupambana na magaidi wa Boko Haram, wakati umebakia muda wa wiki moja tu kufanyika uchaguzi wa rais nchini Nigeria.

Mafanikio ya majeshi ya serikali katika harakati za kuwakabili Boko Haram yanampa RaisJonathan uhakika wa kushinda uchaguzi. Hata hivyo gazeti la "Neues Deutschland" linatilia maanani kwamba mpinzani wa Rais Johathan, Muhammadu Buhari anaungwa mkono na masikini wengi nchini Nigeria. Buhari ametangaza vita dhidi ya rushwa, ambalo limekuwa jambo la kawaida katika utwala wa Jonathan.

Kituo cha wakimbizi kujengwa barani Afrika
Gazeti la "Die Welt" limeripoti juu ya mpango wa mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi za Umoja wa Ulaya juu ya kujenga kituo barani Afrika cha kuwashughulikia wakimbizi kabla ya kufika barani Ulaya. Gazeti hilo limeeleza kwamba idadi ya wakimbizi wanaoingia barani Ulaya haijawahi kuwa kubwa kama sasa, tangu kumalizika vita kuu vya pili.

"Barabara ya Ujerumani"

Gazeti la "Der Spiegel" wiki hii limeripoti juu ya barabara iliyojengwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa msaada wa Ujerumani.

Gazeti hilo linaeleza kwamba Shirika la misaada la Ujerumani ,Welthungerhilfe limesaidia katika ujenzi wa barabara hiyo inayopitia msituni. Barabara hiyo inayoanzia katika mji wa Goma inathibitisha msaada wa kweli wa maendeleo.

Gazeti la "Der Spiegel" linatuarifu kwamba, mwananchi mmoja anaeitwa Georg Dörken anajivunia sana barabara hiyo na anasema kuwa barabara hiyo ni yake.

Dörken alisimamia ujenzi wa barabara hiyo kwa muda wa miaka 9. Gazeti la "Der Spiegel " limefahamisha kwamba sehemu kubwa ya barabara hiyo imejengwa kwa fedha za Shirika la Misaada la Ujerumani-Welthungerhilfe. Dörken anatumai barabara hiyo itaiokoa Kongo Mashariki na itavimaliza vita katika sehemu hiyo.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com