Abdulla Abdulla adai kushinda Uchaguzi | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.07.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Abdulla Abdulla adai kushinda Uchaguzi

Mgombea kiti cha urais nchini Aghanistan, Abdullah Abdullah amejitangaza mshindi wa uchaguzi ulio na utatata, huku akilaumu udanganyifu wa kura umetumika, kumtupa nyuma ya mpinzani wake Ashraf Ghani.

Mgombea wa urais Abdulla Abdulla

Mgombea wa urais Abdulla Abdulla

Mgombea huyo wa kiti cha urais nchini Aghanistan, Abdulla Abdulla aliwaambia maelfu ya wafuasi wake kuwa yeye ndiye mshindi wa uchaguzi wa mwezi uliopita, akijiweka katika mgongano na mpinzani wake Ashraf Ghani.

"Bila shaka sisi ndio washindi wa hii duru ya pili ya uchaguzi, tunajivunia hili, tunaheshimu kura za wananchi, sisi ni washindi. Hatutakubali matokeo yaliochakachuliwa, sio leo wale kesho" Alisema Abdulla Abdulla mbele ya wafuasi wake waliokuwa wakimshangiria.

Ashraf Ghani anayeongoza katika matokeo ya uchaguzi

Ashraf Ghani anayeongoza katika matokeo ya uchaguzi

Misimamo hii ya matokeo ya uchaguzi, imeongeza wasiwasi wa kutokea ghasia za kikabila na kurejea tena kwa mgogoro kati ya wababe wa kivita walioivuruga Afghanistan kuanzia mwaka wa 1992 hadi mwaka 1996 katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hata hivyo Abdulla amewataka wananchi wa Afghanistan kuungana pamoja katika kipindi hiki kigumu cha kubadilishana madaraka kutoka kwa utawala wa miaka 12 wa Hamid Karzai na wakati wanajeshi wa Marekani takriban 50,000 wakikaribia kumaliza jukumu lao la kupigana na waasi wa Taliban.

Ghani aongoza kwa asilimia 56 ya kura

Matokeo ya awali yameonesha, Ashraf Ghani aliyewahi pia kuwa waziri wa fedha akiongoza kwa asilimia 56 ya kura huku Abdulla akijipatia asilimia 44. Msemaji wa tume huru ya uchaguzi Noor Mohammad Noor, amekiri kuwepo kwa udanganyifu wa kura. Amesema masanduku ya kura 7000 kati ya 23,000 yatachunguzwa.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ameonya kuwa yeyote atakayejaribu kuchukua madaraka kinyume na sheria, hatua hiyo itaigharimu Afghanistan kutopokea msaada kutoka Marekani.

Shambulizi katika eneo la Kijeshi, Afghanistan

Shambulizi katika eneo la Kijeshi, Afghanistan

Wakati huo huo maafisa wa Aghanistan wamesema watu 16 wameuwawa wakiwemo wanajeshi wanne wa Jamhuri ya Czech katika shambulizi la kujitoa muhanga Mashariki mwa Afghanistan.

Wizara ya ulinzi ya Jamhuri ya Czech imethibitisha kuuwawa wanajeshi wake wanne na kuongeza kwamba wengine wanne wamejeruhiwa vibaya. Wizara hiyo imesema itatoa habari zaidi baadaye hii leo.

Wahid Seddiqi, msemaji wa gavana wa mkoa wa Parwan amesema wanajeshi, raia 10 pamoja na polisi wawili, waliuwawa wakati mshambuliaji alipojiripua karibu na eneo wanalokaa wanajeshi wa Afghanistan na wale wa kigeni. Kundi la waasi wa Taliban limedai kuhusika na shambulizi hilo.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com