1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMali

UN yaondoka Mali huku ghasia zikiongezeka

6 Novemba 2023

Waasi wanaopigania kujitenga Kaskazini mwa Mali walichukuwa udhibiti wa kambi ilioachwa na kikosi cha Umoja wa Mataifa ya Kidal, ikiwa ni hatua muhimu katika mapambano yanayoendelea kuwania udhibiti wa maeneo.

https://p.dw.com/p/4YTKV
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMAPicha: Sia Kambou/AFP

Hali inatajwa kuwa ya vurugu huku vikwazo vya utawala wa kijeshi wa Mali vikielezwa kutatiza mipango ya uhamishaji wa wanajeshi na vifaa vya Umoja wa Mataifa.

Kabla ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa kuitelekeza haraka kambi yao mjini Kidal siku ya Jumanne, waliamua kuharibu zana nyeti ili kuepusha zana hizo kuangukia katika mikono isiyo sahihi.

Muda mfupi baada ya msafara wa mwisho wa Umoja wa Mataifa kuondoka, waasi wa kabila la Toureg waliokuwa karibu walitangaza kuchukuwa udhibiti wa kambi hiyo.

Soma pia:Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa waondoka eneo la Kidal

Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumatano, zilionekana wakipakia bidhaa zilizoporwa kwenye malori, ikiwemo matairi, kebo pamoja na viti.

Mnamo mwezi Juni utawala wa kijeshi wa Mali uliuamuru ujumbe wa muongo mmoja wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, MINUSMA, kufungasha wakati uhusiano ukiharibika na washirika wa kimataifa.

MINUSMA imeongeza kasi ya kuondoka katika wiki za hivi karibuni, baada ya Mali Kaskazini kutumbukia katika mapigano kati ya waasi na vikosi vya serikali vinavowania udhibiti wa maeneo yanayoachwa na ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa. Matokeo ya mapigano hayo ni kuenea kwa machafuko.

UN: Yakabiliwa na ugumu kuondoka Mali

Makabiliano makali yamezunguka alau kambi mbili za Umoja wa Mataifa, na mbili pia zimeporwa, kulingana na vyanzo viwili vyenye ufahamu wa moja kwa moja juu ya uondokaji wa MINUSMA.

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: Loey Felipe/UN/dpa/picture alliance

Kulingana na taarifa za Umoja wa Mataifa, walinda amani kadhaa wamejeruhiwa na vifaa vya milipuko vilivyokanyagwa na misafara ya Umoja wa Mataifa kuelekea kusini.

Umoja wa Mataifa umekiri juu ya ugumu katika mchakato wake wa kuondoka.

MINUSMA ilisema katika taarifa kwamba ililaazimika kuharibu vifaa ikiwemo magari, risasi na majenerata ambavyo vikosi vyake visingeweza kuhamisha baada ya serikali kuweka vikwazo juu ya kuhamishwa kwa vifaa hivyo.

Msemaji wa ujumbe huo Fatoumata Sinkoum Kaba aliliambia shirka la habari la Reuters kwamba vifaa vya mamilioni ya dola vimeteketezwa.

Soma pia:Walinda amani 15 wa UN washambuliwa Kaskazini mwa Mali

Mamalaka imekataa kuidhinishwa kwa msaada wa angani kwa misafara inayosafiri katika baadhi ya maeneo yenye hali tete katika eneo la Afrika magharibi.

Kwa mujibu wa vyanzo  vya kuaminika, waliamrisha kusimamishwa kwa uwagizwaji wa  mafuta na vipuri na kwa baadhi ya visa walihatarisha usalama wa walinda amani ambao walikuwa wakiondoka.

Hata hivyo mamlaka nchini Mali haijazungumzia chochote kuhusiana na visa hivyo.

Wachambuzi: Mapigano yanatishia taifa la Mali

Wachambuzi wa masuala ya usalama wanaonya kuwa taifa la Mali linaweza kusambaratika kabisa, hatua itayosababisha kuzidi kuyumbisha eneo hilo la Afrika magharibi ambalo vikundi vyenye itikadi kali na mafungamano na makuindi ya al Qaeda na lile la dola la kiislam yakizidi kupata nguvu.

Vyanzo vya kuaminika vinasema kwamba MINUSMA hapo awali ilipanga kuondoka Kidal katikati ya mwezi Novemba, Umoja wa mataifa ulisema kwamba vifaa vilivyoharibiwa huko na katika vituo vingine viwili vya kaskazini vingeweza kuhamishwa na malori ya Umoja huo, lakini utawala wa kijeshi wa Mali ulizuia ufikiwaji wake.

Kwanini Umoja wa Mataifa unashindwa kumaliza mizozo duniani?

Hali hiyo inaashiria mwisho wenye machungu kwa ujumbe huo wa Umoja wa mataifa nchini Mali, ambako ulitumwa baada ya upande wa kaskazini kuzidiwa na wapiganaji wenye itikadi kali na waasi wa Tuareg mnamo 2012.

MINUSMA ilifaulu kurejesha utulivu, lakini vurugu ziliendelea. Mapigano hayo yamesababisha maelfu ya raia na walinda amani zaidi ya 170 kuuwawa na kuufanya ujumbe huo kuwa mbaya zaidi.

Soma pia:Watu 64 wauawa nchini Mali katika mashambulizi mawili tofauti

Hali ya ukosefu wa usalama ulisababisha mapinduzi ya kijeshi ya 2020 na 2021.

Utawala wa kijeshi uliwafukuza wananjeshi wa Ufaransa waliokuwa wakisaidia kupambana na wapiganaji wenye itikadi kali, wakishirikiana na kundi la mamluki la Urusi Wagner, na kuamuru MINUSMA kuondoka.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa alisema hadi Desemba 31 wanapaswa kufungasha, na hadi sasa wafanyakazi 6000 kati ya 14000wamekwishaondoka Mali.

Hata hivyo wachambuzi wanaonya kuwa ikiwa kambi ya Kidal itaangukia mikononi mwa waasi itakuwa ni madhara makubwa kwa Bamako na kusababisha kuzuka kwa vita.