1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Zelensky: Vikosi ya Ukraine vyapiga hatua dhidi ya adui

Admin.WagnerD22 Mei 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema vikosi vyake vinaendelea kupiga hatua dhidi ya wanajeshi wa Urusi katika eneo la mapigano la Kharkiv lakini hali katika mstari wa mbele wa vita kwengineko bado ni mbaya sana

https://p.dw.com/p/4g8eW
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wakati wa mkutano na waandishi habari mjini Riga, Latvia mnamo Januari 11,2024
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Gints Ivuskans/AFP

Katika hotuba yake kwa taifa Jumanne jioni, Zelensky amesema vikosi vya nchi hiyo katika eneo la Kharkiv,vinaendelea kupata ufanisi dhidi ya adui lakini akaonya hali upande wa mashariki karibu na miji ya Pokrovsk, Kramatorsk na Kurakhove imesalia kuwa "ngumu sana". Zelensky ameongeza kusema mapigano zaidi yanaendelea katika eneo hilo.

Soma pia:Zelensky anatarajia Urusi itaimarisha mashambulizi yake upande wa kaskazini

Wiki iliyopita, Rais huyo wa Ukraine alionya kwamba uvamizi wa Urusi Kharkiv huenda ukawa wimbi la kwanza na huenda vikosi vya Urusi vinalenga mji wa Kharkhiv, wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine.

Kuleba asema washirika wanaweza kudungua makombora ya Urusi

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba, amesema Jumanne kwamba washirika wa nchi hiyo wanaweza kudungua makombora ya Urusi kutoka maeneo yao katika kile kilichoonekana kuwa ombi linalotokana a na ukosefu mkubwa wa mifumo ya ulinzi wa anga nchini humo.

Wakati wa mkutano na waandishi habari akiwa na mwenzake wa Ujerumani Annalena Baerbock aliyeko nchini humo kwa ziara yake ya nane tangu uvamizi wa Urusi, Kuleba alisema hakuna changamoto ya kisheria, kiusalama au ya kimaadili ambayo inazuia washirika wao kudungua makombora ya Urusi kwenye eneo la Ukraine kutoka maeneo yao.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock (kushoto) na mwenzake wa Ukraine Dmitry Kuleba (kulia) wakati wa mkutano na waandishi habari baada ya mkutano wao mjini Kiev Jumanne, 21.05.2024
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock (kushoto) na mwenzake wa Ukraine Dmitry Kuleba (kulia)Picha: Thomas Trutschel/photothek/IMAGO

Kwa upande wake, Baerbock amesema kuchelewesha msaada kwa Ukraine pia kunahatarisha usalama wa mataifa ya magharibi.

Mazungumzo ya kujiunga kwa Ukraine na Moldova EU yatarajiwa kuanza

Baada ya mkutano wa baraza la mawaziri Jumanne jioni mjini Brussels nchini Ubelgiji, waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji Hadja Lahbib alisema Ukraine na Moldova zinaweza kutarajia kuanza haraka kwa mazungumzo ya kuwa wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Lahbib hakusema iwapo mataifa hayo yametimiza masharti yote ya kujiunga na Umoja huo ila tu kwamba yanaendelea na mchakato wa marekebisho.

Mawaziri wa fedha wa G7 kujadiliana kuhusu mali ya Urusi iliyofungiwa 

Mawaziri wa fedha wa kundi la nchi tajiri kiviwanda G7 watakaokutana Italia wiki hii watajaribu kupata msimamo wa pamoja kuhusu namna ya kutumia mali ya Urusi iliyofungiwa kusaidia juhudi za Ukrainekatika vita vyake na nchi hiyo.

Mawaziri hao watakutana katika mji wa Stresa siku ya Ijumaa na Jumamosi.