1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 200 wauawa katika miripuko ya Sri Lanka

Bruce Amani
21 Aprili 2019

Miripuko mitatu iliyotokea mnamo Jumapili ya Pasaka kwenye makanisa matatu na hoteli nne nchini Sri Lanka imewauwa watu zaidi ya 200 na kuwajeruhi karibu 450

https://p.dw.com/p/3HBRR
Sri Lanka Batticaloa  Explosion in Zion Kirche
Picha: AFP/L. Wanniarachchi

Hayo ni mashambulizi mabaya kabisa ya kwanza kuwahi kutokea kwenye kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka 10 iliyopita.

Watu saba wamekamatwa na polisi watatu wakauawa wakati wa uvamizi uliofanywa na vikosi vya usalama kwenye nyumba moja katika mji mkuu wa Sri Lanka, Colombo saa chache baada ya mfululizo wa mashambulizi hayo, mengine ambayo maafisa wamesema yalikuwa mabomu ya kujitoa muhanga.

Sri Lanka Razzia der Special Task Force (STF) in Colombo
Vikosi vya usalama vilivamia nyumba ya baadhi ya washukiwaPicha: AFP/I. S. Kodikara

Serikali imetangaza amri ya kutotoka nje mjini Colombo na kufunga mitandao yote ya kijamii na tovuti za kutuma ujumbe, ikiwa ni pamoja na Facebook na WhatsApp. Haijafahamika haraka ni lini amri hiyo ya kutotoka nje itaondolewa.

"kwa jumla, tuna habari za vifo vya watu 207 kutoka hospitali zote. Kwa mujibu wa habari hiyo mpaka sasa tuna watu 450 waliojeruhiwa na wamelazwa hospitali,” alisema msemaji wa polisi Ruwan Gunasekera. Karibu watu 27 miongoni mwa waliokufa ni raia wa kigeni.

Hakuna yeyote au kundi lililojitokeza kudai kuhusika na mashambulizi hayo katika nchi ambayo ilikuwa vitani kwa miongo mingi na wapiganaji waliotaka kujitenga wa Tamil Tigers hadi mwaka wa 2009. Watu kadhaa waliuawa katika mojawapo ya mripuko katika kanisa Katoliki la Katuwapitiya, kaskazini mwa Colombo.

Jeshi limewekwa katika miji

Sri Lanka Colombo Explosion in St. Sebastian Kirche
Mojawapo ya makanisa yaliyoshambuliwaPicha: picture-alliance/AP Photo/C. Karunarathne

Hoteli zilizoshambuliwa mjini Colombo ni Shangri-La, Kingsbury, Cinnamon Grand na Tropical Inn karibu na makazi ya wanyama pori. Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe ameitisha mkutano wa baraza la usalama nyumbani kwake baadaye leo.

"Nina laani vikali mashambulizi haya ya uwoga dhidi ya watu wetu leo. Ninawaomba Wasri Lanka wote wakati huu mgumu kuungana na kuwa imara,” alisema kwenye ujumbe wa mtandao wa Twitter.

Rais Maithripala Sirisena amesema ameamuru kikosi maalum cha polisi na jeshi kuchunguza aliyehusika na mashambulizi hayo pamoja na kiini chake. Msemaji wa jeshi amesema askari wametumwa kuweka ulinzi na usalama umeimarishwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Colombo.

Viongozi wa serikali kuu za ulimwengu wamelaani mashambulizi hayo

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Marekani imetuma salamu za dhati za rambirambi kwa watu wa Sri Lanka na iko tayari kwa msaada, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amesema hakuna mahali ambako unyama wa aina hiyo unaruhusiwa katika jimbo hilo, na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema milipuko hiyo ya bomu ni shambulizi kwa ubinadamu wote.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis akiwahutubia maelfu ya watu waliomiminika katika Kanisa la Mtakatifu Petro kusikiliza ujumbe wake wa Pasaka: "Ningependa kuelezea ukaribu wangu wa dhati kwa jamii ya Kikristo, iliyolengwa wakati wa maombi, na kwa wahanga wote wa mashambulizi ya aina hiyo ya kikatili.