1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yingluck Shinawatra azuiliwa na jeshi

Mjahida24 Mei 2014

Waziri Mkuu wa zamani wa Thailand Yingluck Shinawatra, amezuiliwa na jeshi la nchi hiyo kufuatia mapinduzi yaliotangazwa na jeshi hilo siku ya Alhamisi(22.05.2014) wiki hii.

https://p.dw.com/p/1C61M
Waziri Mkuu wa zamani wa Thailand Yingluck Shinawatra,
Waziri Mkuu wa zamani wa Thailand Yingluck Shinawatra,Picha: Reuters

Baadhi ya familia ya waziri mkuu huyo wa zamani pamoja na wanasiasa kadhaa wa Thailand wamepelekwa katika maeneo ya kijeshi. Bado mpaka sasa haijajulikana ni wapi waziri mkuu huyo wa zamani alikopelekwa.

Duru ndani ya chama chake cha Puea Thai zimethibitisha jeshi kumkamata Shinawatra.

Mmoja wa wanachama wake amesema alikuwepo wakati Waziri Mkuu huyo wa zamani alipopokea simu ya kumuita jeshini siku ya Ijumaa. "Hatujui mahali aliko mpaka sasa kwa sababu jeshi lilichukua simu zake zote za mkononi pamoja na za watu wake wa karibu," zilisema duru hizo.

Akizungumza na shirika la habari la AFP, msaidizi wa Yingluck Wim Rungwattanajinda amesema siku ya Ijumaa Waziri mkuu huyo wa zamani aliaminika kupelekwa katika kambi moja ya kijeshi ilioko nje ya mji mkuu Bangkok.

Mkuu wa Majeshi jenerali Prayuth Chan-ocha alitangaza jeshi kuchukua madaraka kwa kile alichokiita kuwa ni hatua ya kuleta utulivu. Kwa sasa maafisa kadha waandamizi wa jeshi wameteuliwa kuiongoza Thailand.

Yingluck nduguye waziri mkuu wa zamani aliyetoroka baada ya mapinduzi ya mwaka 2006 Thaksin Shinawatra, aliondolewa uongozini mapema mwezi huu, kufuatia uamuzi uliokuwa na utata uliotolewa na mahakama moja nchini humo, hali iliotoa nafasi kwa jeshi kuchukua madaraka siku ya Alhamisi wiki hii.

Gari linaloaminika kumbeba Waziri Mkuu wa Zamani wakati alipoitwa jeshini
Gari linaloaminika kumbeba Waziri Mkuu wa Zamani wakati alipoitwa jeshiniPicha: Reuters

Wengi walioitwa jeshini ni wanachama wa Puea Thai waliopigwa marufuku ya kusafiri nje ya nchi ambapo wachambuzi wanasema hatua hiyo imelenga kuzuwiya kuundwa kwa serikali uhamishoni.

Hatua ya jeshi yakashifiwa

Huku hayo yakiarifiwa makundi ya kutetea haki za binaadamu yamelaani vikali hatua ya jeshi yakuyazuwiya makundi ya wanasiasa wa Thailand pamoja na wanaharakati.

Siku ya Ijumaa baraza la jeshi la kudhibiti amani na utulivu liliwaita wanasiasa 155 akiwemo Waziri Mkuu wa zamani Niwattumrong Boonsongpaisan ambaye pia alitolewa madarakani kupitia mapinduzi, na kuwapa amri ya kujisalimisha au wakamatwe kwanguvu.

Aidha shirika la habari la Reuters lilimnukuu afisa mmoja wa ngazi ya juu jeshini akisema,"Tumemkamata Yingluck, dada yake na shemeji yake."

Mkuu wa Majeshi jenerali Prayuth Chan-ocha
Mkuu wa Majeshi jenerali Prayuth Chan-ochaPicha: imago

Jamaa zake hao wawili walikuwa na nyadhifa za juu serikalini. Afisa huyo wa kijeshi alisema Yingluck Shinawatra hatazuiliwa kwa zaidi ya wiki moja na kuongeza wanahitaji muda huo ili kusawazisha hali ya mambo nchini.

Kwa sasa kumekuwa na amri ya kutotoka nje kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi na moja Alfajiri.

Tayari serikali ya Marekani imetangaza kusimamisha kwa muda msaada wa euro milioni 2.5 kwa Thailand ambayo ni sawa na thuluthi moja ya msaada jumla wa nchi hiyo.

Kulingana na sheria ya Marekani inakubalika kusimamisha msaada dhidi ya jeshi la kigeni linalofanya mapinduzi kwa serikali ilioteuliwa kuingia madarakani. Marekani kwa sasa inataka kurejeshwa mara moja utawala wa kiraia, demokrasia na kuheshimu haki za binaadamu katika wakati huu wa msukosuko.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri: Sekione Kitojo