Wolfsburg yaachana na kocha Hecking
18 Oktoba 2016Klabu hiyo imesema uamuzi huo umefikiwa , kwa "makubaliano maalum" kufuatia mkutano baina ya Hecking na mkurugenzi wa spoti Klaus Allofs.
Hecking ameshindwa kupata uungwaji mkono wowote kutoka kwa Allofs kufuatia kipigo siku ya Jumapili cha bao 1-0 nyumbani dhidi ya timu iliyopanda daraja ya RB Leipzig.
Valerien Ismail , kocha wa kikosi cha wachezaji wa akiba wa Wolfsburg , atachukua hatamu za kuifunza timu hiyo kwa muda, klabu hiyo imesema. Ismail ni mchezaji wa zamani wa Werder Bremen na Bayern Munich akiwa mlinzi.
Wolfsburg ilianza msimu huu ikiwa na kikosi kilichofanyiwa mabadiliko na kuwa na matumaini ya kufikia katika mashindano ya Ulaya. Lakini klabu hiyo iko katika nafasi ya 14 baada ya michezo saba licha ya kumpata mchezaji wa kimataifa wa Ujerumani Mario Gomez.
"Licha ya kucheza vizuri katika Champions League , tumeshindwa kufanikiwa kufuzu katika mashindano ya kimataifa ya Ulaya," Allofs alisema katika taarifa. "Na mabadiliko ya kikosi hayakuleta matokeo tuliyotarajia.
"Baada ya matokeo ya hivi karibuni ya kuvunja moyo, tumeamua kuipa timu msukumo mpya kwa kumbadilisha kocha,Allofs alisema. Hecking amesema , amekatishwa tamaa."
Hecking amekuwa kocha wa Wolfsburg muda mfupi kabla ya Krismass mwaka 2012. Mwaka 2015, Wolfsburg ilishinda kombe la Ujerumani na kumaliza ikiwa ya pili kwa Bayern katika Bundesliga, ikipata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya mabingwa hao. Ilifikia robo fainali ya Champions League msimu uliopita, ikishindwa na waliokuja kuwa mabingwa Real Madrid. Hecking ni kocha wa tatu katika Bundesliga kupoteza kazi yake msimu huu , baada ya kocha wa Werder Bremen Viktor Skripnik na Bruno Labbadia wa hamburg.